Monday, December 28, 2020

Matukio 5 yaliyotikisa mkoa wa Kilimanjaro 2020

 

Miili ya marehemu wa tukio la Mwamposa muda mchache kabla ya kuagwa katika viwanja vya Mashujaa mjini Moshi

Kulingana na Wikipedia, Maisha ni muda ambao kiumbe hai anajaliwa kuishi. Ni hali tofauti kabisa na uzima wa milele, kwa kuwa uhai wake una mwanzo na mwisho.

Hasa mwisho unasababisha maswali: kama kila chenye mwanzo kina mwisho, ya nini kuwepo kwake? Kukosa lengo, kuwepo bure, kutokuwa na maana kunamfanya mtu ajisikie mnyonge, pengine akate tamaa ya kuishi, la sivyo ajitose kufurahia mazuri yanayopatikana maishani, lakini bila uwezo wa kuondoa moyoni ule utupu wa maana unaomtia huzuni ya dhati.

Ndiyo sababu maana ya maisha ni mojawapo kati ya masuala makuu ya binadamu duniani: hawezi kukwepa maswali ya kutoka moyoni mwake kuhusu thamani, madhumuni na umuhimu wa maisha yake.

Mwaka 2020 ulikuwa ni miongoni mwa muda ambao viumbe hai walipewa kuishi, lakini katika kuishi kwake kiumbe huyu alikutana na mengi.

Mengine  yalimfanya afurahie pia ahuzunike kwa namna moja au nyingine.

Katika makala haya tutaangazia mkoani Kilimanjaro ambako nako kulikuwa na mengi yaliyochomoza na kusalia kama kumbukumbu ya maisha kwa wakazi wa mkoa huo uliopo Kaskazini mwa Tanzania.

1.     VIFO VYA WATU KATIKA IBADA YA MWAMPOSA

Haikutarajiwa kutokea hivyo, Februari mwaka huu watu 20 walifariki dunia baada ya kukanyagwa na wenzao wakati wakitoka katika lango moja waliloelekezwa kupita ili kukanyaga mafuta ya upako katika Ibada ya Kanisa la Inuka Uangaze linalosimamiwa na Mtume Boniface Mwamposa.

Katika tukio hilo watu 16 walijeruhiwa. Tukio la kuagwa kwa miili ya marehemu hao ilifanyika katika viwanja vya Mashujaa mjini Moshi na kuhudhuriwa na wakazi wa mkoa huo. Rais John Pombe Magufuli alitoa salamu za rambirambi kwa wafiwa wote.

2.     MLIMA KILIMANJARO KUWAKA MOTO

Mlima Kilimanjaro ni mrefu kuliko yote barani Afrika na ukiwekwa katika tunu za ulimwengu ukiwa na urefu wa mita 5,895. Mnamo Oktoba mwaka huu mlima huo uliwaka moto na kudumu kwa siku saba hadi kuzimwa kwake. Miale ya moto ilikuwa ikionekana kutoka mji wa Moshi umbali wa makumi ya kilomita kutoka eneo la mlima kulikotokea tukio hilo. Hifadhi ya Taifa nchini (TANAPA) ilisema kuwaka kwa moto katika mlima huo hakutaathiri shughuli za utalii ambapo watalii zaidi ya 50,000 hukwea mlima huo kila mwaka. 

Zoezi la uzima wa moto likiendelea katika mlima Kilimanjaro

 3.     TAHADHARI YA COVID-19

Kilimanjaro ni mkoa ambao unapakana na Kenya na kumekuwa na mahusiano ya muda mrefu baina yake na watu waliopo Kenya na Tanzania hususani Kilimanjaro katika Wilaya ya Rombo.

Wakati janga la Corona lilipoanza na kutakiwa kila taifa lichukue tahadhari, kulikuwa na wimbi kubwa la raia wa Kenya waliotaka kujipenyeza kuingia Kilimanjaro kuepuka kusalia majumbani kwa kipindi kisichojulikana.

Hiyo ilitokana na kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli kutangaza kuwa Tanzania haina corona hivyo nchi yake haitakuwa na lockdown lakini tahadhari zaidi ziendelee kuchukuliwa.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Dkt. Anna Mghwira aliwataka wananchi wake kuwa walinzi wa kwanza katika hilo kutoruhusu mwingiliano huo. Hadi mwishoni mwa mwaka huu Tanzania ndiyo nchi pekee ulimwenguni inayoendelea na shughuli zake kama kawaida.

4.     UCHAGUZI ULIVYOWAACHA SOLEMBA WAPINZANI

Mbunge wa Moshi Mjini Priscus Tarimo wakati wa kampeni Oktoba 2020

Oktoba 28, 2020 ulifanyika uchaguzi wa Rais, Wabunge na madiwani ambapo mzizi wa upinzani nchini uling’olewa. Mkoa wa Kilimanjaro ndio kitovu cha siasa za upinzani tangu mwaka 1995 mfumo wa vyama vingi ulipoanzishwa.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), NCCR-Mageuzi na vingine vilishindwa kufurukuta katika uchaguzi huo na kujikuta wakiambulia patupu kwenye uchaguzi huo.

Gumzo kubwa ilikuwa ni wilayani Hai ambako mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe alishindwa na kijana mdogo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Saashisha Mafuwe. Mbowe aliambulia kura 27,684 huku Mafuwe akipata ushindi wa kishindo wa kura  89,786.

Kwa mara ya kwanza jimbo la Moshi lilirudi mikononi mwa CCM kwa kijana Priscus Tarimo kuwa kinara kwa kura 31,169 dhidi ya Raymond Mboya wa Chadema aliyepata kura 22,555. Licha ya wapinzani kupinga matokeo hayo lakini hakuna chochote kilichotokea.

5.     UZINDUZI WA UTOAJI WA VYETI VYA KUZALIWA WATOTO

Waziri wa Katiba na Sheria Mwigulu Nchemba alifanya uzinduzi huo. Zoezi hilo lililofanyika Agosti 2020 lilipokewa vizuri na wakazi wa mkoa huo.
 

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) ilikuja na Mpango Mkakati wa kuhakikisha kila mtoto anayezaliwa sasa na wale ambao tayari wamezaliwa chini ya umri wa miaka mitano wanapata Vyeti vya Kuzaliwa kwa mfumo mpya wa Wakala (RITA) kupeleka huduma hiyo ya utoaji vyeti katka ngazi ya Vituo vya Afya pamoja na ngazi ya Ofisi za Watendaji wa Kata.

Mkoani Kilimanjaro uzinduzi wake ulifanyika katika viwanja vya Mandela, Pasua mjini Moshi ambapo Waziri wa Katiba na Sheria Mwigulu Nchemba alifanya uzinduzi huo. Zoezi hilo lililofanyika Agosti 2020 lilipokewa vizuri na wakazi wa mkoa huo.

0 Comments:

Post a Comment