Monday, July 24, 2017

Kagame kusalia madarakani hadi 2034?

Wakati Rwanda ikiwa katika hatua za mwisho  kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Agosti 4, mwaka huu kama hakutakua na jambo lolote lingine litakalojitokeza basi ni dhahiri kuwa Rais  wa nchi hiyo Paul Kagame atashinda.
Paul Kagame
Hali  inaonesha kuwa upinzani hauna nafasi ya kushinda uchaguzi huo huku pia vyombo vya habari vya nchi hiyo ambavyo vingi vinadhibitiwa na serikali vikionesha kuegemea zaidi kwa Rais Paul Kagame pamoja na chama chake cha RFP.

 Wagombea  wengine wawili  wameruhusiwa kuwania urais katika kinyan'ganyiro hicho ambao ni Frank Habineza, mwenyekiti wa chama cha Green Party  na mgombea mwingine anayewania kama mgombea anayejitegemea na ambaye pia anafahamika kwa kiwango kidogo Philippe Mpayimana mwandishi wa habari wa zamani aliyerejea hivi karibuni nchini Rwanda baada ya kuishi miaka kadhaa uhamishoni katika Jamhuri ya Afrika ya Kati na nchini Ufaransa.

Wagombea wengine waliojitokeza wakiomba kupitishwa kuwania nafasi hiyo waligonga mwamba baada ya kushindwa kutimiza masharti kadhaa ikiwa ni pamoja na kushindwa kufikisha idadi  inayohitajika ya sahini za kudhaminiwa.  Mgombea mwingine alilazimika kujiengua baada ya picha zake za siri kuchapishwa mtandaoni.

Kagame alilazimika kubadilisha katiba
Ili Rais Kagame aweze kuwania muhula wa tatu wa uongozi alilazimika kufanya mageuzi kadhaa kwani  katiba ya Rwanda awali haikuruhusu Rais kuhudumu muhula wa tatu madarakani.

Mwezi Oktoba 2015 bunge la nchi hiyo liliridhia marekebisho ya katiba  yaliyompa nafasi Kagame kuwania tena nafasi hiyo katika uchaguzi wa mwaka 2017, 2024 na 2029. Kinadharia inaonesha kuwa atasalia madarakani kama Rais hadi mwaka 2034.

Bunge la Seneti nchini humo lilipiga kura kuridhia mabadiliko hayo ya katiba ambayo pia yaliungwa mkono na umma katika kura ya maoni.

" Kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo Rwanda ni nchi ya kidemokrasia  lakini imekuwa ikiongozwa na utawala wa kiimla chini ya Rais Paul Kagame  na ni nchi yenye viashiria vya utawala wa kiditeta" anasema Hankel mchambuzi wa siasa za Rwanda.

Rais Kagame awali alitangaza hapo kabla kuwa atastaafu baada ya kumalizika  muhula wake wa tatu mwaka 2024. 

Hata  hivyo Henkel  bado anaamini kwamba bado Kagame anaweza akaingia majaribuni akaendelea kubakia madarakani.

CHANZO: DW


0 Comments:

Post a Comment