Tuesday, July 18, 2017

Shahidi wa nane kesi ya Scorpion ‘afunguka’

Mahakamani-Ilala-Dar es Salaam-Julai 18, 2017 Mshtakiwa Salum Njwete 'Scorpion' akiwa chini ya ulinzi mkali katika  mahakama ya Wilaya ya Ilala baada ya shahidi wa nane kutoa ushahidi wake kuhusu mashtaka yanayomkabili.
Shahidi wa nane wa kesi ya Salum Njwete maarufu Scorpion ametoa ushahidi wake kuwa mlalamikaji Said Mrisho alitobolewa macho kwa kutumia vidole na sio kisu kama inavyodaiwa.

Mbele ya Hakimu Mkazi wa mahakama ya Ilala Flora Haule, ilidaiwa na mwendesha mashtaka Nassoro Katuga kuwa ‘Scorpion’ alitenda unyang’anyi wa kutumia silaha alioutenda Septemba 6, 2016 Buguruni Shell kisha kumchoma na kisu mlalamikaji Said Ally Mrisho machoni, mabegani na tumboni.

Shahidi huyo ambaye ni mpelelezi wa Jeshi la Polisi Tanzania Koplo Bryson alidai wakati wa mahojiano katika kituo cha polisi Njwete alikiri kujeruhi katika tukio hilo.

Aidha shahidi aliongeza kumtafuta mshtakiwa ilianza mara moja baada ya Meneja wa Bada ya Kimboka kutoa ushirikiano mzuri kuwa Salum hayupo chini yake ila ana kiongozi wake anayefahamika kwa jina la Pamba D. Deus.

Koplo Bryson alidai kumtafuta mshtakiwa ilifanyika Septemba 12, 2016 na mahojiano walifanya naye siku hiyo saa 3:30 asubuhi.

Baada ya kutoa ushahidi wake upande wa utetezi kupitia kwa Wakili Msomi Nassoro Salum ulidai kuwa unaupinga ushahidi huo kwa maelezo kuwa mshtakiwa alikubali kosa kutokana na kupewa mateso makubwa kinyume na sheria ya uchukuaji wa maelezo.

Upande wa Jamhuri ulioongozwa na Katuga ulidai hoja za utetezi hazina mashiko kwani maelezo yalichukuliwa kwa hiari. Kesi iliahirishwa hadi Agosti 2, 2017.
Mahakamani-Ilala-Dar es Salaam-Julai 18, 2017 Mshtakiwa Salum Njwete 'Scorpion' akiwa chini ya ulinzi mkali katika  mahakama ya Wilaya ya Ilala baada ya shahidi wa nane kutoa ushahidi wake kuhusu mashtaka yanayomkabili.

0 Comments:

Post a Comment