Monday, March 6, 2017

Hospitali ya Taifa Muhimbili na changamoto zake

NA MWANDISHI WETU
Mkurugenzi wa Tiba wa MNH, Dkt. Hedwiga Swai akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari (hawapo pichani), kushoto ni Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji Dkt. Julieth Magandi

Imeelezwa upungufu wa rasilimali watu katika maeneo ya ubobezi na ubingwa wa juu kwenye Hospitali ya taifa ya Muhimbili ni miongoni mwa changamoto zinazoikabili hospitali hiyo kwa sasa.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari leo Mkurugenzi wa Tiba wa hospitali hiyo Dkt. Hedwiga Swai amesema wamepata mafanikio makubwa hadi sasa ikiwamo upanuzi wa eneo la wagonjwa wa dharula ambao wameongezeka kutoka 100 hadi 300 kwa siku huku vikifungwa vifaa vya kisasa kuhudumia.
Aidha Dkt. Swai amesema hospitali hiyo imefanikiwa kupeleka wataalamu nje ya nchi kwa ajili ya kujifunza upandikizaji wa figo wakifikia 19 walio tayari kuanza kazi hiyo.
Hata hivyo Dkt. Swai amesisitiza kuwa ufanisi huo unapaswa kuungwa mkono licha ya uhitaji wa maeneo mengine kuwa mkubwa na kuongeza kuwa wameomba kibali cha kuajiri wauguzi na madaktari wa kada mbalimbali ili kuongeza ufanisi.
Mbali na changamoto hiyo uchache wa vifaa tiba na uchakavu wa miundombinu  nao umekuwa ukipunguza kasi ya utoaji wa huduma licha ya kuendelea kutafuta mbinu mbalimbali za kupunguza. 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji Dkt. Julieth Magandi amesema hospitali hiyo ina mpango wa kuendelea kuongeza mapato ya ndani kutoka Shilingi Bilioni 4.5 miezi sita iliyopita hadi Shilingi Bilioni 5 kwa mwezi ili kuimarisha maeneo mbalimbali kwa ukuaji wa huduma hiyo.
Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji Dkt. Julieth Magandi (kushoto) na Ofisa Uhusiano John Stephen

0 Comments:

Post a Comment