Monday, December 18, 2023

Uhamiaji Tanzania, Uhamiaji China zatiliana saini kuimarisha uhusiano wa kibiashara na ulinzi

Naibu Kamishna wa Jeshi la Uhamiaji la China (NIA)  Li Junjie na mwenyeji wake Jenerali Kamishna wa Uhamiaji Tanzania Dkt. Anna Makakala wakionyesha hati za makubalino baada ya kusaini, kwenye hafla iliyofanyika katika Chuo cha Kikanda cha Uhamiaji (TRITA)  Mosi mnamo Desemba 18, 2023.


Jeshi la Uhamiaji Tanzania na Jeshi la Uhamiaji la Jamhuri ya Watu wa China zimetilia saini hati za makubaliano ili kuimarisha uhusiano wa kibiashara, ulinzi na Uhamiaji baina ya mataifa hayo mawili.


Utilianaji saini baina ya majeshi hayo umefanyika katika Chuo cha Kikanda cha Uhamiaji Tanzania (TRITA) mjini Moshi ambako Naibu Kamishna wa Jeshi la Uhamiaji la China (NIA)  Li Junjie na mwenyeji wake Jenerali Kamishna wa Uhamiaji Tanzania Dkt. Anna Makakala walitilia saini hati hizo za makubaliano.


Akizungumza na vyombo vya habari Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Jumanne Sagini amesema baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuzuru China kilichokuwa kimebaki ni jukumu la wizara husika kufuatilia kwa karibu namna inavyoweza kufaidika na uwekezaji huo wa China nchini Tanzania.


Aidha Dkt. Makakala amesema hati ya makubaliano baina ya Uhamiaji wa mataifa yote mawili ni mwanzo wa mpango thabiti wa kubadilisha uzoefu kwa Nia ya kujenga uchumi.


Kwa upande wake Li Junjie amekaririwa akisema ni hatua adhimu kuwekeza katika Taifa la Tanzania.


Utilianaji saini huo unajiri baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuzuru nchini China ambako alikutana na Xi Jinping kuhusu uwekezaji katika nyanja mbalimbali nchini Tanzania.


Rais wa Jamhuri ya Watu wa China Xi Jinping aliweka bayana kuwa Taifa lake haliwekezi katika mataifa ya Afrika kwenye miradi isiyo na maana bali katika miradi ambayo itayasaidia mataifa hayo ikiwamo Tanzania.










0 Comments:

Post a Comment