Mwenyekiti
wa Halmashauri ya Moshi Moris Makoi ameipongeza na kuishukuru taasisi isiyo ya
kiserikali ya Ako Tanzania Support kwa msaada wao walioutoa kuzikarabati Shule
za Msingi Sungu na Uchau zilizopo Kibosho huku akitoa wito kwa watanzania
kuunga mkono juhudi za wahisani hao.
Makoi
ameyasema hayo tarehe 19 Aprili 2023 wakati wa ziara yake ya siku moja kukagua
kazi iliyofanyika baada ya wahisani hao Ako Tanzania Community Support kwa
ushirikiano na Ako Community Support kutoka Ujerumani kufanikisha ujenzi na
ukarabati wa majengo za shule hizo.
Akiwa na
timu ya elimu kutoka katika halmashauri hiyo Makoi amesema shule hizo
zimejengwa muda mrefu lakini zimekuwa na changamoto mbalimbali ikiwamo vyoo,
vyumba vya madarasa, majiko hali ambayo imekuwa ikisababisha mazingira magumu
kwa wanafunzi wanaosoma humo walimu wanaowafundisha.
“Tumefika
Sungu na Uchau na tumeona kazi kubwa waliyoifanya kwa gharama kubwa, baada ya
mazungumzo nao kwa kina wameniahidi sasa watakarabati na madarasa karibu matano
na ofisi za mwalimu; kikubwa katika ziara hii ilikuwa ni kutambua mchango wao
katika jamii hii, kuwashukuru na kuonyesha kwamba serikali iko nao katika shughuli
hizi ambazo wanafanya,” amesema Makoi.
Hata hivyo
Makoi amesema haikua rahisi kukubali msaada wa kufanyiwa ukarabati katika shule
hizo kwani sio kila msaada ni wa kuukubali kutokana na hofu iliyotanda ya
misaada ambayo imekuwa ikienda kinyume na utamaduni wa Watanzania.
“Kama
mwenyekiti wa halmashauri nimefika hapa kwa ajili ya kujiridhisha kama msaada
unakidhi vigezo vya msaada; misaada tunayoitaka kama nchi sasa isije ikawa misaada
ya kigeni ambayo inakuja kuingilia utamaduni, mila na desturi zetu,
nimejiridhisha kwamba Ako Tanzania Community Support wako tu kwa ajili kusaidia
na sio kuja kutuingiza katika mambo yasiyofaa,” ameongeza Makoi.
Pia Makoi
ameitaka jamii inayozunguka shule hizo kuwa walinzi huku akiwataka walimu kuhakikisha
rasilimali hizo inatunzwa kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Akizungumza
na JAIZMELA mwakilishi wa AKO Community Support ya Ujerumani Dieter Jaenicke
katika program ya ujenzi wa jiko, ukumbi wa chakula na ukarabati wa vyumba vya
madarasa katika Shule ya Msingi Uchau amesema elimu ndio tumaini pekee kwa kila
jamii hapa ulimwenguni.
“Kwa niaba
ya Ako, nataka kueleza kwa nini tupo hapa, tunaamini kwamba watoto ni
mustakabali wa nchi, na elimu kwa watoto ni muhimu zaidi kwa kila nchi duniani
na tuna furaha kubwa tunaweza kukusaidia kidogo. kidogo kwa nguvu na vyanzo
vyetu kufanya elimu ya watoto kuwa nzuri iwezekanavyo,” amesema Jaenicke.
Mwakilishi
huyo aliongeza kuwa alipofika na kuyaona mazingira ya shule alihisi kugusw
akufanya kitu kwa ajili ya watoto wa Kitanzania
“Niliona
shule hii haiko katika hali nzuri na nikaona ni lazima tufanye kitu… na
kipaumbele cha kwanza wanahitaji jiko la shule na sasa jiko lipo…”amesema
Jaenicke
Kwa upande
wake Mkuu wa Shule ya Msingi Sungu Redempta Assey amesema wanaushukuru uongozi
na wahisani AKO Community Support pande zote mbili ya Tanzania na Ujerumani kwa
kuwaona na kuleta misaada ambayo ina nia ya maendeleo kwani watoto watasoma
katika mazingira bora na Tanzania itajengeka.
“Tunawashukuru
sana wafadhili kutoka Ako Ujerumani kwa msaada wao kwa kutukarabati shule hii ilikuwa
na changamoto ya madarasa kuwa mabovu sana tunaahidi tutayatunza, huu ukarabati
utasaidia taaluma itazidi kupanda juu,” amesema Assey.
Mkuu wa
Shule ya Msingi Uchau Agnes Mbwambo amesema kuwajengea jiko linalotunza
mazingira, ukumbi wa chakula na ukarabati unaotarajiwa kuanza wa vyumba vya
madarasa ni jambo zuri la lenye faida kwa watanzania.
“Tunawashukuru
sana, sana, sana tunaomba waendelee kuwa karibu nasi na Mungu awabariki,”amesema
Mbwambo.
Miradi hiyo imegharimu kiasi cha Shilingi mil. 340 za Tanzania kati ya hizo mradi wa Sungu umegharimu kiasi cha shilingi mil. 100 na wa Uchau umegharimu kiasi cha shilingi mil. 240
Mwonekano wa mojawapo ya majengo ya Shule ya Msingi Uchau. Shule hiyo ilijengwa mnamo mwaka 1948 na wamisionari kutoka Ujerumani. |