Ukweli na Kuheshimiana ni kiini ujenzi wa jamii zetu

Ulimwenguni kwa sasa kumejaa habari potofu na upotoshaji, ni muhimu kuhakikisha kwamba ukweli na kuheshimiana vinakuwa kiini kwa ujenzi wa jamii zetu.

Mapambano dhidi ya Habari za Uongo hayapaswi kukoma

Habari za uongo, habari za uongo zinazosambazwa kwa lengo la kumdhuru mtu au jambo fulani, huifanya jamii kuwa na sintofahamu. Zinaweza kutumika kwa madhumuni ya kiitikadi, kisiasa au hata uhalifu, kama vile ulaghai mtandaoni unaolenga kuiba data ya kibinafsi.

Utandawazi na Athari zake katika Uandishi wa Habari

Katika jamii yetu ya kisasa, ambapo habari ziko kila mahali na zinaweza kupatikana kwa kila mtu, mara nyingi ni ngumu kutofautisha kati ya vyanzo vya kuaminika na habari bandia.

Uandishi wa Habari nguzo msingi mkuu kwa ujenzi wa jamii inayojitambua

JAIZMELA blog ni miongoni mwa vyanzo vya habari, zilizochakatwa kwa kuzingatia miiko ya uandishi wa habari.

Mila na Desturi ni nguzo muhimu

Mila na desturi ni nguzo muhimu sana katika utamaduni wa jamii yoyote ile; mila ni sawa na sheria zisizoandikwa. Mila ni taratibu za maisha na mwenendo zinazofuatwa na jamii fulani katika utendaji kulingana na historia na utamaduni wao. Mila zinatambulisha maadili ya jamii husika, huelezea namna jamii inavyoendesha mambo yake.

Monday, September 18, 2017

'Team Work' ni kila kitu katika mafanikio

Unapokuwa unafanya kazi mahali popote pale duniani, ni vema kuwa na kile kinachofahamika ‘Nguvu ya Pamoja’. Nguvu ya Pamoja haiwezi kuja pasipokuwa na marafiki na wafanyakazi wazuri wanaojitambua. Ndivyo ilivyo kwa wafanyakazi hawa wa Mpakasi ambao wanaamini katika nguvu hiyo au unaweza kusema ni waamini wa ‘Team Work’.
Kutoka kushoto Mwasiti Mussa, Kassim Mpeta, Bernard Kalonga, Flora Raphael na Gerald Nyang’ali wakitoka kazini maeneo ya Oysterbay jijini Dar es Salaam. (Picha zote na Jabir Johnson)






Flora Raphael na Bernard Kalonga maeneo ya Oysterbay jijini Dar es Salaam. 

Monday, July 31, 2017

Taxi mbili zagongana Mango Garden, Dar

Taxi mbili zimegongana katika ajali mapema Julai 30 mwaka huu kwa kile kinachodaiwa uzembe wa madereva wa vyombo hivyo vya usafiri. Katika tukio hilo hakuna aliyepoteza maisha isipokuwa uharibifu wa magari hayo. Mashuhuda wa tukio hilo walisema madereva walikuwa wamelewa pombe.


TAZAMA PICHA



Monday, July 24, 2017

Kagame kusalia madarakani hadi 2034?

Wakati Rwanda ikiwa katika hatua za mwisho  kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Agosti 4, mwaka huu kama hakutakua na jambo lolote lingine litakalojitokeza basi ni dhahiri kuwa Rais  wa nchi hiyo Paul Kagame atashinda.
Paul Kagame
Hali  inaonesha kuwa upinzani hauna nafasi ya kushinda uchaguzi huo huku pia vyombo vya habari vya nchi hiyo ambavyo vingi vinadhibitiwa na serikali vikionesha kuegemea zaidi kwa Rais Paul Kagame pamoja na chama chake cha RFP.

 Wagombea  wengine wawili  wameruhusiwa kuwania urais katika kinyan'ganyiro hicho ambao ni Frank Habineza, mwenyekiti wa chama cha Green Party  na mgombea mwingine anayewania kama mgombea anayejitegemea na ambaye pia anafahamika kwa kiwango kidogo Philippe Mpayimana mwandishi wa habari wa zamani aliyerejea hivi karibuni nchini Rwanda baada ya kuishi miaka kadhaa uhamishoni katika Jamhuri ya Afrika ya Kati na nchini Ufaransa.

Wagombea wengine waliojitokeza wakiomba kupitishwa kuwania nafasi hiyo waligonga mwamba baada ya kushindwa kutimiza masharti kadhaa ikiwa ni pamoja na kushindwa kufikisha idadi  inayohitajika ya sahini za kudhaminiwa.  Mgombea mwingine alilazimika kujiengua baada ya picha zake za siri kuchapishwa mtandaoni.

Kagame alilazimika kubadilisha katiba
Ili Rais Kagame aweze kuwania muhula wa tatu wa uongozi alilazimika kufanya mageuzi kadhaa kwani  katiba ya Rwanda awali haikuruhusu Rais kuhudumu muhula wa tatu madarakani.

Mwezi Oktoba 2015 bunge la nchi hiyo liliridhia marekebisho ya katiba  yaliyompa nafasi Kagame kuwania tena nafasi hiyo katika uchaguzi wa mwaka 2017, 2024 na 2029. Kinadharia inaonesha kuwa atasalia madarakani kama Rais hadi mwaka 2034.

Bunge la Seneti nchini humo lilipiga kura kuridhia mabadiliko hayo ya katiba ambayo pia yaliungwa mkono na umma katika kura ya maoni.

" Kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo Rwanda ni nchi ya kidemokrasia  lakini imekuwa ikiongozwa na utawala wa kiimla chini ya Rais Paul Kagame  na ni nchi yenye viashiria vya utawala wa kiditeta" anasema Hankel mchambuzi wa siasa za Rwanda.

Rais Kagame awali alitangaza hapo kabla kuwa atastaafu baada ya kumalizika  muhula wake wa tatu mwaka 2024. 

Hata  hivyo Henkel  bado anaamini kwamba bado Kagame anaweza akaingia majaribuni akaendelea kubakia madarakani.

CHANZO: DW


Thursday, July 20, 2017

Watangazaji wa Kiss FM Dar es Salaam

Watangazaji wa Kiss FM studio za Dar es Salaam wakiwa katika kikao Julai 20, 2017
Kikao cha watangazaji na wanahabari wa Kiss FM wamekutana katika kikao cha pamoja kujadili masuala kadha wa kadha kuhusu programu mbalimbali Morning Kiss, Kiss Drive Time na Kiss Most Wanted.

Watangazaji 17 waliopo jijini Dar es Salaam walijadili kwa ajili ya kuboresha vipindi vyao.

Mwenyekiti Ramadhani Khalifan a.k.a Bplus Watangazaji waliokuwepo ni Pendo Michael, Phonia Bundala, Yusta Msowoya, Angel Doto, Stella Joseph, Herman Kihwili, Mbwana Shomari, Said Msumi, John Lupokela, Ruba, Abdul Nyaulingo, Edward Fabian, Sempanga Ramadhani a.k.a King Sempa na Salehe Juma. 

Ruba na Stella Joseph


Said Msumi na Edward Fabian

Sempa na Pendo Michael

Tuesday, July 18, 2017

Shahidi wa nane kesi ya Scorpion ‘afunguka’

Mahakamani-Ilala-Dar es Salaam-Julai 18, 2017 Mshtakiwa Salum Njwete 'Scorpion' akiwa chini ya ulinzi mkali katika  mahakama ya Wilaya ya Ilala baada ya shahidi wa nane kutoa ushahidi wake kuhusu mashtaka yanayomkabili.
Shahidi wa nane wa kesi ya Salum Njwete maarufu Scorpion ametoa ushahidi wake kuwa mlalamikaji Said Mrisho alitobolewa macho kwa kutumia vidole na sio kisu kama inavyodaiwa.

Mbele ya Hakimu Mkazi wa mahakama ya Ilala Flora Haule, ilidaiwa na mwendesha mashtaka Nassoro Katuga kuwa ‘Scorpion’ alitenda unyang’anyi wa kutumia silaha alioutenda Septemba 6, 2016 Buguruni Shell kisha kumchoma na kisu mlalamikaji Said Ally Mrisho machoni, mabegani na tumboni.

Shahidi huyo ambaye ni mpelelezi wa Jeshi la Polisi Tanzania Koplo Bryson alidai wakati wa mahojiano katika kituo cha polisi Njwete alikiri kujeruhi katika tukio hilo.

Aidha shahidi aliongeza kumtafuta mshtakiwa ilianza mara moja baada ya Meneja wa Bada ya Kimboka kutoa ushirikiano mzuri kuwa Salum hayupo chini yake ila ana kiongozi wake anayefahamika kwa jina la Pamba D. Deus.

Koplo Bryson alidai kumtafuta mshtakiwa ilifanyika Septemba 12, 2016 na mahojiano walifanya naye siku hiyo saa 3:30 asubuhi.

Baada ya kutoa ushahidi wake upande wa utetezi kupitia kwa Wakili Msomi Nassoro Salum ulidai kuwa unaupinga ushahidi huo kwa maelezo kuwa mshtakiwa alikubali kosa kutokana na kupewa mateso makubwa kinyume na sheria ya uchukuaji wa maelezo.

Upande wa Jamhuri ulioongozwa na Katuga ulidai hoja za utetezi hazina mashiko kwani maelezo yalichukuliwa kwa hiari. Kesi iliahirishwa hadi Agosti 2, 2017.
Mahakamani-Ilala-Dar es Salaam-Julai 18, 2017 Mshtakiwa Salum Njwete 'Scorpion' akiwa chini ya ulinzi mkali katika  mahakama ya Wilaya ya Ilala baada ya shahidi wa nane kutoa ushahidi wake kuhusu mashtaka yanayomkabili.

Wednesday, July 12, 2017

Yousafzai Malala ni nani?

Yousafzai Malala
Malala Yousafzai ni mwanaharakati wa nchini Pakistan katika masuala ya elimu na mshindi wa tuzo ya Nobel aliyepata akiwa na umri mdogo. 

Anafahamika kwa harakati zake za uwakili wa haki za binadamu hususani katika masuala ya elimu kwa wanawake kwa wenyeji wa bonde la Swat huko Khyber Pakhtunkhwa Kaskazini Magharibi mwa Pakistan
Malala na tuzo yake
Kundi linalodaiwa la kigaidi na ulimwengu wa magharibi la Taliban liliwazuia wasichana katika eneo hilo wasihudhurie masomo. Uwakili wake wa kuwatetea wasichana wa eneo hilo ulikua hadi kufikia medani ya Kimataifa. 

Yousafzai alizaliwa katika mji wa kibiashara wa Mingora huko Pakistan. Familia yake ilikuwa na shule katika eneo hilo. Binti huyo alidai kuwa Jinnah na Benazir Bhutto ni role-models wake katika harakati zake. Aidha Yousafzai alisema mawazo ya baba yake na kazi zake za kiutu zilimmwongezea hamasa. 

Mapema mwaka 2009 akiwa na kati ya miaka 11-12 aliandika katika blogu ya BBC kwa lugha ya Urdu akielezea maisha yake na ukandamizwaji unaofanywa na Taliban katika bonde hilo la Swat. Msimu uliofuata mwandishi wa habari Adam B. Ellick wa New York Times alitengeneza makala kuhusu maisha yake baada ya Jeshi la Pakistan kuingia katika eneo hilo.  

Alionekana katika runinga na majarida mbalimbali na baadaye akapata fursa ya kuwa mshiriki wa Tuzo ya Kimataifa ya Amani kwa Watoto iliyotolewa na Mwanaharakati Desmond Tutu. Mchana wa Okotoba 9, 2012 Yousafzai alijeruhiwa katika jaribio la kutaka kumuua lililolengwa na Taliban. Binti huyo alipoteza fahamu na kupelekwa hospitalini kwenye Taasisi ya Cardiology ya Rawalpindi lakini baadaye alipata ahueni kisha kupelekwa katika Hospitali ya Queen Elizabeth iliyopo Birmingham nchini Uingereza. 

Kitendo hicho cha Talibani cha kutaka kumuua binti huyo kiliibua vuguvugu la kimataifa la kumuunga mkono Yousafzai. Januari 2013 Deutsche Welle iliandika katika makala na taarifa zake kuwa  Yousafzai ni chipukizi anayefahamika zaidi ulimwenguni. Majuma machache baada ya jaribio la kutaka kumuua Yousafzai  kundi la Waislamu 50 nchini Pakistan liliongoza ibada ya fatwā kwa waliotaka kufanya jaribio la mauaji kwa binti huyo. 

Tuzo mbalimbali alipokea ikiwamo ya Sakharov mwaka 2013 na mwaka 2014 alipokea Tuzo ya Amani ya Nobel.  Mwaka 2017 ametunukiwa uraia wa heshima wa Kanada.


Tuesday, July 11, 2017

Stella Joseph ni nani?

Keki ya Stella Joseph ya kutimiza miaka 23

Stella Joseph (katikati), Grace (kushoto) na Abeid (kulia).

Seda (katikati), Grace (kushoto) na Stella (kulia)

Stella akimlisha keki dada yake kipenzi Seda, Abeid akishuhudia tukio hilo

Stella na Seda waliamua kuwaliza watu pale walipolishana keki ya upendo ka midomo yao huku wafanyakazi wenzao wakishuhudia

Ramadhani Sempangala a.k.a King Sempa alimpaka Stella keki katika uso wake, lilikuwa tukio la kushtukiza ambalo Stella hakutegemea
Stella Joseph ni mtangazaji na mwandishi wa Redio Kiss FM ambaye analitumikia Kampuni la Sahara Media Group jijini Dar es Salaam

Makao makuu ya Sahara Media Group yapo jijini Mwanza. Jijini Dar es Salaam ni studio namba mbili. Vyombo vya Habari Star TV, Radio Free Africa (RFA), Kiss FM na gazeti la Msanii Afrika vinamilikiwa na kampuni hilo. 

Stella ni miongoni mwa watangazaji wa vipindi vya Habari na Burudani katika Kiss FM. Julai 11, 2017 alikuwa akisheherekea siku ya kuzaliwa kwake. Stella alikuwa akitimiza miaka 21. Alizaliwa mwaka 1996.
Ilikuwa zamu ya Agatha Kisimba katika birthday hiyo.

Phonia Bundala kwa hisia alikula kipande cha keki kutoka Stella

Mzee Ali naye hakucheza mbali kwenye suala la keki

Pendo Michael a.k.a Mama mchanganyiko, Mamaa Tenga naye akachukua kipande cha keki. Ilivutia sana

Bplus na Stella Joseph

Stella Joseph na Anastazia

Wednesday, June 28, 2017

Machinjio ya punda yafunguliwa Kenya

Nyama ikiwa katika machinjio 
Machinjio ya tatu punda nchini Kenya imefunguliwa katika eneo la Nakwaalele mjini Lodwar,katika kaunti ya Turkana. Machinjio hiyo ya kampuni ya Zilzha kutoka China itasindika nyama ya punda pamoja na ngozi kwa ajili ya usafirishaji hadi China na nchi nyingine za mashariki ya mbali.

Kufunguliwa kwa machinjio hiyo utaleta ushindani wa machinjio nyingine mbili  za Maraigushu,mjini Naivasha katika kaunti ya Nakuru,na ile iliyopo Mogotio katika kaunti ya Baringo.

Shu Jing Long,mmojawapo wa wachina wanaoendesha kichinjio cha Zilzha cha Turkana amesema machinjio hicho itatoa ajira kwa wenyeji zaidi ya 200. Aidha Long amesema hamu yao hasa ipo katika ngozi ya punda ambayo ina soko kubwa nchini China.

Afisa wa Afya kutoka Wizara ya Mifugo nchini Kenya Dkt Jonathan Tanui msimamizi wa shughuli za uchinjaji katika machinjio cha Zilzha amesema machinjio hiyo imefikia viwango vinavyotakiwa na kuongeza kuwa wanyama hao kabla ya kuchinjwa ni lazima wapimwe ili kuhakikisha kuwa ni salama kwa kuliwa.

Punda mmoja anauzwa katika ya shilingi 8,000 hadi 10,000 za Kenya.


Sunday, June 25, 2017

Dereva bodaboda agongwa na gari afariki dunia

Mwili wa dereva bodaboda ambao haukutambulika mara moja ukiwa umelazwa pembezoni mwa barabara mita chache kutoka kituo cha Mabasi yaendayo kwa haraka cha Morocco jijini Dar es Salaam Juni 25, 2017
Dereva wa bodaboda ambaye hajafahamika jina lake na mahali anapotoka amefariki dunia baada ya kugongwa na gari maeneo ya Kinondoni Kanisani jijini Dar es Salaam mita 200 kutoka kituo cha mabasi yaendayo kwa haraka cha Morocco.

Mashuhuda wa tukio hilo walisema ajali hiyo ilitokea saa 1:30 usiku wa Jumapili ya Juni 25 mwaka huu wakati dereva huyo akiwa na wenzake watatu wakiwa katika pikipiki iliyosajiliwa kwa Na. MC 861 AHE alipogongwa na gari ambalo lilikimbia baada ya tukio hilo.

Aidha mashuhuda hao walisema aliokuwa amewapakiza wametokomea kusikojulikana kutokana na sheria kukataza kupakiza ‘mshikaki’ yaani watu zaidi ya wawili.

Dereva wa bodaboda hiyo anakadiriwa kuwa na kati ya miaka 23-30 ilishuhudiwa dimbwi la damu barabarani hapo kutokana na kupasuka kichwa.

Jeshi la Polisi mkoa wa Kinondoni lilifika yapata dakika tano baadaye baada ya raia wema kutoa taarifa kuhusu tukio hilo. Baada ya kuandika maelezo waliuchukua mwili wa marehemu na kuupeleka hospitalini kuuhifadhi huku uchunguzi zaidi ukiendelea.

Hata hivyo Maofisa wa Jeshi hilo walisikika wakiwataka madereva wa bodaboda kuvaa kofia za kujikinga pamoja na abiria wao ili kupunguza madhara zaidi inapotokea ajali.
Gari la Jeshi la Polisi mkoa wa Kipolisi Kinondoni PT 4012 likiwa katika eneo la ajali Juni 25, 2017

Mashuhuda wa tukio hilo katika eneo la ajali Juni 25, 2017

Ofisa wa Jeshi la Polisi akichukua maelezo kutoka kwa mashuhuda wa tukio la ajali maeneo ya Kinondoni Kanisani Juni 25, 2017

Wasamaria wema wakisaidia kuupakia mwili wa marehemu katika gari la Polisi, Kinondoni Juni 25, 2017

Monday, June 19, 2017

SAA yaisaidia familia ya Mzee Sixtus Mhagama

Wanachama wa Chama cha Washehereshaji Tanzania (SAA) katika picha ya pamoja na familia ya Mzee Sixtus Mhagama Juni 19, 2017 maeneo ya Boko inapoishi familia hiyo inayougua ugonjwa wa ajabu.

Wanachama wa SAA katika kuwatia moyo familia ya Mzee Sixtus Mhagama.

Mzee Sixtus Mhagama akipokea fedha taslimu kutoka kwa wanachama wa SAA.

Mtoto wa kwanza wa Mzee Sixtus Mhagama, Schola ambaye hajaathirika na ugonjwa huo akiwashukuru SAA kwa msaada walioutoa.

Schola akiwa na mama yake ambaye kwa sasa haoni kutokana na matatizo yaliyomkuta.
Chama cha Washereheshaji Tanzania (SAA) kimetoa msaada wa shilingi milioni mbili zikiwamo fedha taslimu shilingi milioni 1.3 jana kwa familia moja inayougua ugonjwa wa ajabu uliothibitishwa na madaktari kuwa haiwezekani kutibika.

Familia hiyo watu sita ya Mzee Sixtus Mhagama ya kijiji cha Litoho kutoka Wilayani Mbinga mkoani Ruvuma iliyohamia jijini Dar es Salaam imepatwa na ugonjwa wa ajabu unaowafanya watoto wao kila wanapofikisha miaka mitano huanza kupata ulemavu.

Katika ushuhuda wake wakati akikabidhiwa msaada huo vikiwamo vitu mbalimbali kama nguo, mafuta, sukari Mzee Mhagama amesema walitoka kijijini kwao Litoho mwaka 2006 na kuja Dar es Salaam katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya matibabu kutokana na hospitali zote mkoani humo kukosa suluhisho la watoto wao.

Aidha Mzee Mhagama amesema miongoni mwa watoto hao mmojawapo alishafiriki dunia huku wengine wakiendelea kukumbwa na ugonjwa huo ambao unawafanya wote magamba pindi wanapokuwa katika maeneo ya baridi na maumivu makali na mifupa yao kushindwa kuimarika hali inayosababisha ulemavu.

Akipokea msaada huo Mzee Mhagama ameishukuru jamii kwa kumjali kwani hata nyumba anayoishi huko Boko jijini Dar es Salaam amepewa na msamaria mwema ili aweze kujisitiri katika hali ngumu ambapo mkewe pia amepatwa na ugonjwa huo ambao umemfanya ashindwe kuona.

Hata hivyo amesema changamoto bado ni kubwa kwani anapaswa kwenda kila siku Muhimbii na watoto wake ili waweze kufanyiwa mazoezi lakini kuna wakati anashindwa kutokana na ukosefu wa fedha za kuwasafirisha wagonjwa hao.

Kwa upande wake wakati akikabidhi msaada huo Mwenyekiti wa SAA Emmanuel Urembo amesema wamekuwa wakisaidia jamii kwa mwaka mara moja lakini safari hii waliiona familia hiyo inayopata mateso makubwa japokuwa ni kiasi kidogo lakini wanaamini msaada huo utaweza kuwafariji.


Tuesday, June 13, 2017

Korea Kaskazini yamwachilia Otto Warmbier

Otto Warmbier
Korea Kaskazini imemwachilia huru mwanafunzi Mmarekani Otto Warmbier ambaye alikuwa amefungwa jela katika taifa hilo la bara Asia. Warmbier, 22, alihukumiwa kufungwa jela miaka 15 na kazi ngumu Machi 2016 baada ya kupatikana na hatia ya kujaribu kuiba bango la propaganda kutoka kwenye hoteli moja. Tillerson amesema Bw Warmbier sasa yuko njiani kurejea Marekani ambapo ataungana tena na jamaa zake Cincinnati, Ohio. Gazeti la Washington Post limemnukuu babake Fred akisema mwanawe wa kiume amesafirishwa kama mgonjwa kwa sababu hana fahamu. Gazeti hilo linasema wazazi wa Warmbier waliambiwa mwana wao wa kiume alianza kuugua ugonjwa wa botulism, ugonjwa nadra ambao humfanya mtu kupooza, muda mfupi baada ya kesi yake kumalizika miezi 15 iliyopita. Otto Warmbier, mwanafunzi aliyekuwa amehitimu na shahada ya uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Virginia, alikuwa amezuru Korea Kaskazini kama mtalii akiwa na shirika la Young Pioneer Tours alipokamatwa 2 Januari 2016.

Rais Magufuli awafunda wakuu wa mikoa

Rais Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na wakuu wa mikoa yote katika Ikulu jijini Dar es Salaam Juni 13, 2017.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewaagiza Wakuu wa Mikoa kusimamia kwa ukaribu utekelezaji wa mpango wa ujenzi wa viwanda katika maeneo yao ili kuwawezesha wananchi kuongeza thamani ya mazao yao na kuzalisha ajira.
Magufuli ametoa agizo hilo jana Ikulu Jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Wakuu wa Mikoa ya Tanzania Bara,  kuwa kila Mkuu wa Mkoa anapaswa kufanyia kazi fursa za uanzishaji wa viwanda katika eneo lake na kuhakikisha anashawishi wawekezaji kuzitumia fursa hizo kama inavyofanyika katika Mkoa wa Pwani.
Aidha Magufuli amewaagiza Wakuu wa Mikoa kuongeza juhudi za utatuzi wa migogoro ya ardhi ikiwa ni pamoja na kuharakisha mchakato wa kuwanyang’anya hati za umiliki wa mashamba makubwa ambayo yanashikiliwa na watu pasipo kuyaendeleza.
Hata hivyo amewatahadharisha Wakuu wa Mikoa hao dhidi ya watu wanaofanya njama za kujimilikisha maeneo makubwa ya ardhi na kusababisha wakulima na wafugaji kukosa maeneo ya kilimo na malisho na ametaka wote watakaobainika kufanya njama hizo wafichuliwe na kunyang’anywa maeneo hayo.

Ndugai atishia kuwaongezea adhabu Mdee na Bulaya

Spika wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai
Spika wa Bunge Job Ndugai amewapa onyo tena wabunge Halima Mdee na Ester Bulaya akisema kuwa wanapaswa kutambua kuwa Bunge bado lina uwezo wa kuwaita na kuwahoji na kuwapa adhabu kali zaidi ya hiyo walionayo sasa.
Onyo hilo linakuja ikiwa ni siku moja baada ya spika huyo kusifiwa na Rais John Pombe Magufuli kuwa anafanya vizuri kuwadhibiti wabunge waropokaji bungeni na kumtaka aendelee na kasi hiyo.
Ndugai amesema kuwa ameamua kutoa onyo hilo kufuatia wabunge hao kufanya malumbano na bunge huku wengine wakitumia maneno ambayo sio mazuri hivyo amewashauri kuwa wamewavumilia kwa mengi lakini kama bado huko waliko wanaendelea na tabia hizo wanaweza kuwaita na kuwapa adhabu kali zaidi ya hiyo waliyonayo sasa.
Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge imewaadhibu wabunge kutohudhuria vikao vyote vya Bunge linaloendelea hadi Bunge la Bajeti 2018/2019 baada ya kuwakuta na hatia ya kudharau mamlaka ya Spika wa Bunge.
Wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Ester Bulaya na Halima Mdee



Monday, June 12, 2017

Acacia yamjibu JPM

Mgodi wa North Mara


Kampuni ya Madini ya Acacia imeona matokeo ya kushtua ikiwa ni saa chache baada ya Kamati ya Pili ya Rais iliyoundwa na Rais John Pombe Magufuli kuwasilisha ripoti ambayo imeangazia nyanja za historia ya kiuchumi na kisheria ya mauzo ya nje ya makanikia ya madini.
Ripoti ya Tume iliyoundwa mwezi Machi mwaka huu na Rais John Magufuli iliyojikita kueleza kiasi cha madini na fedha ambazo Tanzania hupoteza kutokana na usafirishaji wa mchanga wenye madini imedai kuwa Kampuni ya madini yenye makazi yake nchini Canada, Acacia ambayo ni kampuni kubwa zaidi ya madini haikuwahi kusajiliwa nchini, hivyo imekuwa ikifanya kazi kinyume cha sheria.
Katika matangazo ya moja kwa moja ya Televisheni kutoka Ikulu, Rais Magufuli amesema Tanzania imepoteza takriban shilingi trilioni 188 katika kipindi cha miaka 19 kati ya mwaka 1998 na mwaka 2017 kupitia usafirishaji wamakinikia ya dhahabu na shaba.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari Acacia imesema kwa mujibu wa data za zaidi ya miaka 20 tulizonazo ni vigumu kuoanisha matokeo yao na yaliyokutwa na kamati, kwani kamati imetoa thamani ya juu kwa zaidi ya mara 10 kuliko thamani halisi ya makanikia.
Tume hiyo imetoa mapendekezo imefanya ikiwamo ya Acacia kulipa kodi inayodaiwa na mirahaba, kufanya majadiliano upya ya mikataba mikubwa ya uchimbaji madini, umiliki wa Serikali katika migodi, na muendelezo wa marufuku ya kuuza nje tuhuma ambazo imekanusha vikali.
Aidha Acacia imesema imekuwa ikifanya biashara kwa kufuata utaratibu na sheria za Tanzania na kuongeza kuwa tangu kuanza kwa uchimbaji wa madini wamekuwa wakilipa mirahaba yote inayotakiwa kulipwa na kukaguliwa kila mwaka kwa viwango vya Kimataifa.

Hata hivyo Acacia imekaribisha mazungumzo na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mgodi wa Bulyahulu

Tanzania yapoteza Trilioni 188 makanikia dhahabu na shaba

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akionesha Ripoti hiyo ya Kamati ya pili ya Uchunguzi wa Madini yaliyo kwenye makontena yenye mchanga unaosafirishwa nje ya nchi kutoka kwenye machimbo ya madini sehemu mbalimbali hapa nchini mara baada ya kukabidhiwa Ikulu jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan na kulia ni Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakishuhudia.
Tanzania imepoteza takriban shilingi trilioni 188 katika kipindi cha miaka 19 kati ya mwaka 1998 na mwaka 2017 kupitia usafirishaji wamakinikia ya dhahabu na shaba.
Ripoti ya Tume iliyoundwa mwezi Machi mwaka huu na Rais John Magufuli iliyojikita kueleza kiasi cha madini na fedha ambazo Tanzania hupoteza kutokana na usafirishaji wa mchanga wenye madini imedai kuwa Kampuni ya madini yenye makazi yake nchini Canada, Acacia ambayo ni kampuni kubwa zaidi ya madini haikuwahi kusajiliwa nchini, hivyo imekuwa ikifanya kazi kinyume cha sheria.
Katika matangazo ya moja kwa moja ya Televisheni kutoka Ikulu, Rais Magufuli amemtaka Waziri wa Sheria Profesa Paramagamba Kabudi kupitia mikataba yote ya madini.
Ripoti iliyopita ilisababisha Waziri wa nishati na madini Prof. Sospeter Muhongo kusimamishwa kazi.


Tuesday, June 6, 2017

Mama Mghwira rasmi mkuu wa Mkoa Kilimanjaro, ala kiapo Ikulu

Mama Anna Mghwira Juni 6, 2017 katika Ikulu jijini Dar es Salaam
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemwapisha Anna Elisha Mghwira kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro leo Ikulu jijini Dar es Salaam. 
Mama Anna Mghwira akila kiapo cha Uadilifu wa Viongozi
Mghwira amekula kiapo cha Uadilifu wa Viongozi mbele ya Rais Magufuli na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa. Kiapo hicho kinafuatia uteuzi alioufanya Rais Magufuli kwa Mwenyekiti huyo wa chama cha ACT – Wazalendo kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro mapema mwezi huu. Kutokana na uteuzi huo Mama Mghwira alilazimika kujiuzulu nyadhifa zake zote ndani ya chama chake pamoja na kujivua uanachama. Mara baada ya kiapo hicho, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Anna Elisha Mghwira alipanda gari lake la kazini na kuelekea Mkoani Kilimanjaro kuanza kazi rasmi. Mama Anna Mghwira anachukua nafasi ya Said Meck Sadiq ambaye aliomba kujiuzulu na kukubaliwa na Rais Dk John Magufuli. Mkoa wa Kilimanjaro umepata kuongozwa na wakuu wa mkoa watatu katika kipindi cha miaka miwili, Leonidas Gama ambaye ni mbunge wa Songea Mjini, Said Meck Sadick na Anna Elisha Mghwira. Kabla ya hapo Mkuu huyo mpya wa mkoa alikuwa Mgombea wa Urais kwa tiketi ya Chama cha ACT-Wazalendo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010. Uteuzi wa kushika wadhifa huo umeacha maswali lukuki miongoni mwa wafuatiliaji wa masuala ya kisiasa kitaifa na kimataifa.