Wakati dunia ikitoa machozi kwa kuondokewa na Papa Francis mnamo Jumatatu ya Aprili 21, 2025; kuna mtu asiyefahamika sana na maelfu ya wafuatiliaji wa masuala ya dini ya Katoliki mwenye asili ya Ireland aliyeishi muda mwingi nchini Marekani kabla ya kurudishwa makao makuu ya kanisa hilo jijini Vatican.
Baada ya kutangaza kuwa Papa Francis “amerudi nyumbani kwa Baba” Kadinali Kevin Farell ilikuwa ni habari mpya kabisa miongoni mwa wafuasi wa kanisa katoliki duniani kwamba kwa sasa atakuwa Camerlengo wa kanisa hilo ikiwa na maana kuwa atashikilia majukumu ya kuliongoza kanisa hilo mpaka atakapochaguliwa Papa mwingine.
Papa Francis alimtangaza kuwa kadinali mnamo mwaka 2019 na kwamba kwa sasa Kadinali Farell atasalia katika nafasi hiyo “Apostolica Sedes Vacans ambapo neno "Apostolica Sedes Vacans" hutumika wakati wa kipindi cha mabadiliko baada ya kifo cha Papa au wakati ambapo Papa amejiuzulu, na wakati huu ni muhimu kwa ajili ya mchakato wa uchaguzi wa Papa mpya kupitia Konklave.
Pia Camerlengo Kadinali Kevin Farell anahudumu katika matukio yote kwa kipindi chote cha maombolezo.
Farell alizaliwa jijini Dublin mnamo mwaka 1947, alisoma katika Chuo Kikuu cha Salamanca nchini Hispania pia katika chuo kikuu cha Pontifical Gregorian jijini Rome.
Utumishi wake katika kanisa katoliki duniani alianza huduma za kiroho katika Chuo Kikuu cha Monterrey huko Mexico pia katika Parishi ya Bethesda, Maryland.
Kadinali huyo mwenye umri wa miaka 77 sasa amehudumu katika makanisa ya katoliki kwa miaka 30 nchini Marekani, ambapo mwaka 2007 atangazwa kuwa Askofu wa Dallas hadi mwaka 2016 wakati ambao Papa Francis alimtaka kurudi Vatican kama kiongozi wa Idara mpya ya Uangalizi wa Familia na ndio mwaka ambao alipandishwa hadi kuwa Kadinali.
Mnamo mwaka 2023 Kadinali Farell alitajwa kama Camerlengo, pia alitangazwa na Papa Francis kama Rais wa Mahakama ya Juu ya Vatican City State na kuwa Rais wa Kamati ya Masuala ya Siri ya Kanisa Katoliki.
Kadinali Farell atasimamia katika mkutano wa makadinali unaojulikana kama Konklave kwa ajili ya kumchagua Papa mpya wa kanisa hilo.
Vilevile kama ulikuwa hufahamu hili; Camerlengo anaweza kuchaguliwa kuwa Papa kama ilivyofanyika kwa Papa Leo wa XIII mnamo mwaka 1878 na Papa Pius XII mnamo mwaka 1939.
Camerlengo ina maana gani?
Camerlengo ni cheo cha juu kabisa katika Kanisa Katoliki kinachohusiana na uongozi wa Vatikani, Neno hili linatokana na maneno ya Kilatini "camerarius" (mtoa huduma au msimamizi wa chumba), na linahusiana na jukumu muhimu alilokuwa nalo Camerlengo katika kusimamia mali za Kanisa, hasa wakati wa kipindi cha mabadiliko baada ya kifo cha Papa au wakati ambapo Papa hayupo.
Camerlengo ni kiongozi ambaye anachukua nafasi muhimu wakati wa kipindi cha mpito katika Kanisa Katoliki na kuhakikisha kwamba mchakato wa uongozi na uchaguzi wa Papa mpya unakwenda kwa usahihi.
0 Comments:
Post a Comment