Mpaka mwaka 1882 katika bara la Ulaya mtu mmoja kati ya watu saba alikuwa anakufa kwa ajili ya ugonjwa wa Kifua Kikuu ambapo tarehe 4 Machi 1882 Mjerumani wa Chuo Kikuu cha Gottingen Dkt. Robert Koch alitangaza kugundua kimelea kinachosababisha ugonjwa huo na kukipa jina la “Mycobacterium tuberculosis” MTB.
Hatua ya kubaini kinachosababisha ugonjwa wa kifua
kikuu ilikuwa ni ugunduzi mkubwa kuwahi kutokea ulimwenguni kwani kwa miaka
kenda rudi watalaamu mbalimbali waliketi chini kubaini kimelea kinachosababisha
ugonjwa huo kama ni bakteria, protozoa, minyoo au ectoparasaiti.
Mwaka 1848 Mmishionari wa Kijerumani Johannes
Rebmann aliandika rekodi ya kuwa mzungu wa kwanza kutoka barani Ulaya kuuona
Mlima Kilimanjaro na baadaye walifuata wengine Richard Burton na John Hanning Speke mnamo mwaka 1858 ambao walifanikiwa
kuchora ramani ya Ziwa Tanganyika.
Mnamo mwaka 1884 kulifanyika Mkutano wa Berlin
ambao ulikuwa maalum kwa ajili ya kuligawa bara la Afrika ambapo Tanganyika
iliangukia mikononi mwa Ujerumani ambao walichukua na maeneo mengine kama Togo
na Namibia. Walikaa Tanganyika kutoka miaka hiyo ya 1880 hadi waliposhindwa
vita vya kwanza vya dunia mnamo mwaka 1919.
Tanganyika ilichukuliwa na Waingereza ambao
walikaa hadi kupata uhuru mnamo tarehe 9 Desemba 1961; hivyo mambo mengi
waliendeleza ikiwamo miradi mbalimbali ya kilimo;
Katika ardhi ya Tanganyika kanda ya kaskazini
walianza utafiti wa mazao ya kahawa katika mkoa wa Kilimanjaro na Arusha; hata
hivyo walivutiwa na eneo la Kibong’oto ambalo waliamua kuweka kituo chao cha
utafiti wa zao la kahawa.
Hata hivyo baadaye walikuja kubaini wafanyakazi
waliokuwa wakifanya kazi katika mashamba ya utafiti walikuwa wakikabiliwa na
matatizo ya vifua na mapafu pia vikohozi visivyoisha na baridi hata wengine
kupoteza maisha.
Zaidi anasimulia Dkt. Peter Daud ambaye ni
Mtafiti wa Magonjwa ya Kuambukiza wa Hospitali ya Maalum ya Taifa ya Magonjwa
Ambukizi Kibong’oto
“Hospitali
ya Kibong’oto ni hospitali yenye historia ndefu sana, Imekuwepo toka mwaka 1926
ilianzishwa kama kituo kidogo. Kilichoanzishwa na wakoloni, kilikuwa ni kituo
cha utafiti wa mabo ya kahawa. Kwa nchi za Afrika Mashariki chini ya Mjerumani,
Mjerumani alianzisha kama kituo kidogo cha utafiti wa kahawa; kadri muda
uliuvyoenda wale waliokuwa wakifanya kazi katika mashamba ya kahawa wakaanza
kuona, Kama wana ugonjwa ambao haueleweki; wanabanwa na mapafu, wanakohoa;
kwasababu Mjerumani alikuwa anashirikiana na wenzao waliowaacha huko ndio
wakajakugundua kuwa ulikuwa ni kifua kikuu. Ukiangalia kwenye memo walizokuwa
wanaandikiana zilionyesha ni ugonjwa wa TB. Kwa hiyo wakahamisha kutoka kituo
cha utafiti wa kahawa hadi kuwa sanatorium kuhudumia wagonjwa wanaopata ugonjwa
kifua kifuu. Kwa hiyo ikaendelea hivyo mpaka tunafika kupata uhuru; pia
tunafahamu kuwa baada ya vita ya dunia Tanganyika ilikuwa chini ya koloni la
Waingereza; lakini wakaendeleza kuwa wanatibu wagonjwa wote waliokuwa chini ya
makoloni ya Wajerumani na Waingereza. Baada ya kupata uhuru tunafahamu hali ya
afya ilivyokuwa nchini; vituo vilikuwa vichache na vingine vilikuwa ni vya
taasisi za kigeni; ilivyoendela hivyo; Kibong’oto ikaendelea kuwa ni hospitali
ya kutibu wagonjwa wa Kifua Kikuu,” alisema Dkt. Peter Daud
Wakati inaanzishwa kama Sanatorium ya Kibong’oto
mnamo mwaka 1926 Dkt. Norman Davies aliweka rekodi ya kwanza ya kuwa Mganga
Mfawidhi akifuatiwa na Dkt. Allen Yatera. Mnamo mwaka 1978 Dkt. John Jacob
Kifaruka alikuwa Mganga Mfawidhi hadi mwaka 1986, kisha Dkt. James Salekwa
alihudumu katika wadhifa huo hadi mwaka 1992.
Dkt. Cathbert Kiwia alishika wadhifa huo hadi
mwaka 1998 alipoukabidhi kwa Dkt. Liberate John Mleah ambaye alihudumu kwa
miaka 10 hadi mwaka 2014 akiweka
rekodi ya kwanza tangu Tanganyika ipate uhuru kuwa Mganga mfawidhi aliyekalia
kiti hicho kwa muda mrefu.
Dkt. Riziki Kisonga aliushika kwa miaka saba hadi
tarehe 14 Oktoba mwaka 2021 pale Dkt. Leonard Subi alipokabidhiwa hadi sasa
akiwa katika wadhifa wa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo Maalum ya Taifa ya
Magonjwa Ambukizi Kibong’oto.
“Jambo
la Msingi katika Hospitali yetu ni kwamba hii ni hospitali ya kihistoria
kwasababu ni moja ya chimbuko la sayansi ya matibabu ya ugonjwa wa Kifua Kikuu nchini; Mwaka 1926
ndiyo ilianza kama hospitali ambapo ilianza kama kituo cha kutenga wagonjwa wa
Kifua Kikuu. Lakini mwaka 1952 ikapandishwa hadhi na kuwa hospitali kamili ya
Taifa ya Kifua Kikuu. Na ikumbukwe kwamba ilichukua takribani miaka 60 kugundua
dawa za kutibu Kifua Kikuu tangu vimelea vya Kifua Kikuu vilivyogundulika mwaka
1882 na mwanasayansi mahiri wa Kijerumani Dkt. Robert Koch;”
alisema Dkt. Leonard Subi
Mchango wa Hospitali Maalum ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi
Kibong’oto baada ya uhuru wa Tanganyika mnamo mwaka 1961 ni mkubwa hasa
ikizingatiwa wakati ule juhudi za kulikabilli janga hili la kifua kikuu
lilikuwa bado katika kiwango cha chini ikilinganishwa na sasa
“Sisi kama Hospitali
ya Kibong’oto tunayo michango mikubwa sana na mpaka sasa tunaitwa Hospitali
Maalumu ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto; Hii kufuatia Tangazo la Serikali NA. 8828 la
Novemba 2010 ambapo tulitangazwa kuwa Hospitali Maalum ya Taifa ya Magonjwa
Ambukizi. Na kwa muda mrefu tumekuwa tukitoa huduma za kimatibabu hususani
matibabu ya kibingwa hususani katika magonjwa ya Kifua Kikuu lakini tangu
tutangazwe sasa tumepanua wigo na kuyafikia magonjwa mengineyo;” aliongeza Dkt.
Leonard Subi
Kibong’oto pia inatoa taswira ya athari za Ukoloni katika sekta ya afya, kwani wakati wa
utawala wa kikoloni hospitali hii ilikuwa pekee kwa ajili ya matibabu ya kifua
kikuu licha ya kwamba baada ya uhuru serikali ya Tanzania ilijitahidi kufanya
mabadiliko katika utoaji wa huduma za afya.
Mtafiti wa Magonjwa ya Kuambukiza wa Hospitali Maalum
ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto Dkt. Peter Daud anatupitisha katika
eneo la vifaa na rekodi mbalimbali ambazo zilikuwa zikitumika wakati huo kabla
ya mabadiliko makubwa yaliyofanywa na serikali ya Tanzania.
![]() |
“Mbele yenu
vitu mnavyoviona, hizi ni malikale sehemu ya kumbukumbu ya historia ya
Hospitali ya Kibong’oto kama tunavyofahamu Hospitali imekuwepo tangu mwaka 1926
ikiwa inatoa matibabu ya kifua kikuu, ina maana kabla ya uhuru. Kwa hiyo hapa
vitu tunavyoviona, hivi ni baadhi tu ya kumbukumbu za wagonjwa zinazoonyesha
taarifa za wagonjwa waliowahi kutibiwa hapa kama inavyoonekana kuanzia mwaka
1923. Na hii hapa ndiyo rejista au leja ya wagonjwa wote waliokuwa wanafanyiwa
upasuaji. Kama tunavyofahamu kabla ya dawa kuwepo, Hospitali ya Kibong’oto; ni
ya kwanza Tanzania kufanya upasuaji wa mapafu; hii ni mojawapo ya kumbukumbu za
wagonjwa waliokuwa wanafanyiwa upasuaji wa mapafu, moja ya sehemu ya matibabu
ya Kifua Kikuu. Na hii kama inavyoonekana ni mihuri iliyokuwa inatumika kwamba
mgonjwa alipokuwa akija; baada ya kuwa Daktari ameshampima kifua chake alikuwa
anagonga muhuri sehemu alipoandika taarifa zake na sehemu ambayo imeharibika ya
kifua. Na hiyo ilikuwa kwa ajili ya mwendelezo na kuonyesha wapi alipotoka na
wapi anaelekea mgonjwa husika. Hiki pia kilikuwa ni kifaa kilichokuwa
kikitumika katika upasuaji wa mapafu, kwasababu tunafahamu kwamba; wataalmu wa
enzi hizo kabla ya uhuru walikuwa wakijaza hewa kwenye mapafu. Unajaza hewa kwa
ajili ya kwenda kuua hivyo vijidudu kenye mapafu waliojificha. Kama unavyojua,
upasuaji wa mapafu ni lazima uweze kuchana mbavu na hivi ni mojawapo ya vifaa
vilivyotumika enzi za ukoloni kufanya upasuaji wa mapafu pia ni sehemu ya
matibabu ya Kifua Kikuu. Kama tunavyoona vifaa vyote vilivyokuwa vikitumika katika
kufungua mapafu, vingine vya sehemu za kujazia hewa na hewa hiyo ilikuwa inapimwa
na mitambo. Mbele yenu huu ni mtambo, ulikuwa unatumika kwa wale wagonjwa
waliokuwa wanakuja baada ya madaktari wameshawaona na vipimo vimefanyika kuwa
wamejaa maji au usaha au kitu kingine ambacho kinahitaji kuvutwa na hii
ilitumika wakati huo kufyonza, kwa sasa zipo za kisasa. Ilikuwa inatumika
kuvuta damu, uchafu pia wakati wa upasuaji kwa mfano upasuaji wa mapafu, damu
nyingi zilipokuwa zinatoka hii ilikuwa inatumika. Na hii ilikuwa sehemu ya
mitungi ya Oksijeni, mgonjwa baada ya kufanyiwa upasuaji alikuwa anapelekwa
katika chumba cha uangalizi maalum huku akiendelea kupata hewa ya Oksijeni. Hii
hapa ni Mashine ya kuchomelea na sisi huku kwenye udaktari kuna sehemu huwa
tunachomelea, wakati wa upasuaji unapokuwa unafungua kifua; ile mishipa midogo
midogo ya damu inayovujisha damuili uwezekuona eneo lako la upasuaji vizuri;
hii ndiyo mashine iliyokuwa inatumika kuchomelea kwa ajili ya kuziba ile
mishipa ya damu isiweze kuchafua eneo ambalo daktari anafanyia upasuaji. Ni mashine
ya zamani lakini bado ni mashine nzuri sana, kwa sasa bado inafanya kazi lakini
kuna mashine za kisasa ambazo hatuwezi kutumia tena;” alifafanua Dkt. Peter
Daud
Baada ya Uhuru serikali ya Tanzania imeendelea
kujikita katika mfumo wa afya wa kidemokrasia na unaohudumia watu wote wenye
changamoto za kifua kikuu; Kibong’oto imekuwa mfano na alama muhimu ya
utekelezaji wa sera za afya na kuonyesha
umuhimu wa kuhakikisha kuwa huduma za afya zinapatikana kwa watu wote bila
kujali hali zao za kijamii na kiuchumi.
“Jina la
Kibong’oto; yeyote Yule anayekuja hapa; ndiyo hospitali pekee inayotoa huduma kwa
wagonjwa wa kifua kikuu ndiyo maana unaona sisi tunapokea wagonjwa wote nchi nzima.
Na wengine wanatoka nchi za jirani hizi za maziwa makuu; (Kibong’oto) imekuwa ni chachu ya kutoa
matibabu kwa viwango vya kimataifa. Mgonjwa anayetibiwa hapa TB hata angeenda
Ujerumani ataweza kutibiwa vilevile. Kwa hiyo kuna mwingine yuko Shinyanga,
labda yupo Kazuramimba, Kigoma anavyoanza kujiona hapa nipo aua akawa anahisi
naweza kuwa na TB; wengine wamekuwa wakipanda basi wenyewe, wanajileta wenyewe
Kibong’oto na wanapata matibabu kasha kurudi majumabni kwao kuendelea na
shughuli zao;” alongeza Dkt. Peter Daud
Dkt. Peter Daud kama mwajiriwa katika
Hospitali Maalum ya Taifa ya Magonjwa
Ambukizi Kibong’oto anafunguka kuhusu namna ambavyo mapambano dhidi ya Kifua
Kikuu katika hospitali hiyo yalivyoacha kumbukumbu isiyofutika katika maisha
yake pia yameacha matokeo chanya kitaifa na kimataifa.
“Ilikuwa ni
kuhamisha wagonjwa kutoka kwenye matibabu ya sindano na kuwahamisha moja kwa
moja kwenye matibabu ya vidonge
Kwasababu
tunafahamu hapo zamani tulikuwa tunatumia sindano kwani ilikuwa sehemu ya
matibabu; kuna mgonjwa alikuwa anachomwa miezi nane na mwingine zaidi ya miezi
nane; Unaweza ukafikiria kwamba kila siku ya Mungu anachoma sindano, sindano,
sindano, sindano zaidi ya miezi nane lilikuwa siyo jambo la kawaida. Lakini kutokana
na mabadiliko ya kiteknolojia sisi Kibong’oto tumekuwa sehemu ya kushiriki mabadiliko,
tumeweza kushiriki kushiriki kuwahamisha
wagonjwa kutoka matumizi ya sindano hadi kwenye matumizi ya vidonge pekee. Hilo
na jambo ambalo limenifurahisha sana, na sisi Kibong’oto ilikuwa ni sehemu ya mabadiliko
na kuchangia kuwahamisha kutoka matumizi ya sindano hadi kwenye matumizi ya
vidonge pekee;” alisema Dkt. Peter Daud
Kwa upande wake Dkt. Subi anasisitiza kuwa
mabadiliko makubwa yanayofanywa hospitalini hapo ikiwamo kukamilika kwa maabara
ya Utafiti na Teknolojia ya Afya unaonyesha juhudi za kujenga uwezo wa utafiti
na matumizi ya teknolojia za kisasa katika
kugundua na kutibu magonjwa.
“Nikianza
na matumizi ya ardhi; tumeandaa Master Plan. Kwamba hii ardhi tunaitumiaje?
Kwasababu ni Hospitali ya Magonjwa Ambukizi; Master Plan yetu tumeigawanya
katika maeneo, katika zones. Kwa mfano kuna zone ya maabara; maabara ya afya ya
jamii, usalama wa kibaiolojia daraja la tatu; Na maabara hiyo ina kazi zake maalum za
uchunguzi wa magonjwa. Siyo maabara ya Kibong’oto peke yake lakini itatoa
huduma za mapambano dhidi ya magonjwa ya kuambukiza hususani yale yenye umuhimu
wa kipekee katika jamii; Lakini pia itatoa huduma za uchunguzi wa magonjwa
mengine ya tiba ya kawaida; yakiwemo ya kuambukiza na yasiyokuwa ya kuambukiza.
Na maabara ile ukiiangalia imejengwa na serikali makusudi. Na ndiyo uwekezaji
mkubwa wa maabara katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; ambayo ina kila kitu kinachotakiwa
duniani. Kwa maana kwamba, inaweza kuchunguza vimelea hatarishi duniani, vya
ebola, Marburg, na vinginevyo; lakini inatumia teknolojia za kimolekyuli katika
ugunduzi wa magonjwa. Lakini maabara hiyo pia inamwangalia binadamu kama yeye
na pia itatumika katika tafiti mbalimbali;” alisema Dkt. Leonard Subi
Kwa ujumla Hospitali Maalum ya Taifa ya Magonjwa
Ambukizi Kibong’oto inatoa taswira ya mabadiliko katika sekta ya afya, athari
za ukoloni na juhudi za taifa katika kujenga mifumo ya afya baada ya uhuru pia
inasimama kama kielelezo cha historia ya matibabu ya kifua kikuu na mchango
wake katika maendeleo ya afya nchini
Tanzania.
Credit
to:
Johnson Jabir/JAIZMELA/ Kibong’oto Hospital; Barua Pepe: johnsonjabir@gmail.com
0 Comments:
Post a Comment