Sunday, December 1, 2024

Walanguzi wa Ndizi wanavyowaumiza Wakulima Uru Kusini

Credit to: JAIZMELA News
Wakulima wa ndizi Uru Kusini wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro wametakuwa kuungana kwa pamoja katika utaratibu unaofaa ili kuhakikisha soko la zao hilo halichezewi na wachache wanaotaka kujinufaisha kupitia wakulima hayo.

Akizungumza katika mkutano wa Wanawake na Wanaume wa Uchumi wa Viwanda Tanzania (WAWAUVITA) uliofanyika Kimanganuni, Uru Kusini mnamo Novemba 30, 2024 Diwani wa Kata ya Uru Kusini Wilhard Kitali amesema changamoto ya bei kwa wakulima wa zao la ndizi ni mizigo mzito unaotakiwa kutatuliwa mapema.

Hali iliyopo kwa sasa kwa wakulima wa ndizi wa Uru Kusini Mkungu mmoja wa ndizi umekuwa ukinunuliwa shambani kwa shilingi 3,000/=  hadi shilingi 5,000/= kisha unauzwa kwa zaidi ya shilingi 15,000/= kwenye masoko makubwa nchini baada ya walanguzi kuchukua shambani hatua ambayo imekuwa mwiba kwa wakulima

Mbali na hilo Kitali ameweka bayana kuhusu namna wakulima hao wa Uru Kusini wanavyoweza kujikwamua kiuchumi kwa ufugaji wa mbuzi wa maziwa badala ya ng’ombe ambao mtaji mkubwa huhitajika.

Katika semina hiyo ya siku moja ya Wawauvita Mwenyekiti Mariam Muhandeni amewataka wajasiriamali hao kutambua kuwa msingi mzuri wa biashara ni utunzaji wa kumbukumbu.

Akifundisha katika semina hiyo Meneja wa Benki ya Azania tawi la Moshi Yusuf Lenga amewataka wakazi hao wa Uru Kusini kuachana na utaratibu wa kujiunga katika vikundi kwa nia ya kutaka fedha.

Kwa upande wake Katibu wa Wawauvita Joseph France Aloyce ameweka bayana mafanikio na changamoto za wajasiriamali hao na mwarobaini wa baadhi ya changamoto.

Wengine waliopata fursa ya kufundisha ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MUCO) Beatrice Kimaro ambaye amewataka wajasiriamali hao kujitahidi kuwa na matumizi mazuri .

Washiriki wa semina hiyo ya Wawuvita wamesema wamejifunza mengi kuhusu elimu ya fedha na kwamba semina hizo zitakuwa msaada mkubwa wa kujikwamua kiuchumi katika eneo la Uru Kusini.

Mbunge wa Viti Maalum Asha Raymond alipata fursa ya kuzungumza na wajasiriamali hao wa Uru Kusini na kuongeza kuwa Wakulima wenye elimu ya fedha wanaweza kuelewa na kuchagua mikopo bora kutoka kwa taasisi za kifedha kama vile benki na vikundi vya kifedha. Mikopo hii inaweza kutumika kupanua shughuli za kilimo.

Wakati watu wanapokuwa na elimu ya fedha, wanakuwa na tabia bora za kifedha kama vile kuwekeza, kulipa kodi, na kuchangia katika uchumi wa taifa. Hii inaongeza ustawi wa jamii na taifa kwa ujumla.

Credit to: Jabir Johnson; jabirjohnson2020@gmail.com; +255 693 710 200

















0 Comments:

Post a Comment