Sunday, December 15, 2024

Mangi Gilbert Gilead Shangali Asimikwa Isaleni, Wari-Machame; Kilimanjaro

Mangi Gilbert Gileadi Shangali akiinua ngao kwa mkono wa kulia ikimaanisha ulinzi wa jamii ya Kimachame, mkono wa kushoto akiwa na mkuki baada ya kusimikwa na Chifu Frank Marealle (wa kwanza kushoto) lililofanyika Isaleni, Wari-Machame wilayani Hai mkoani Kilimanjaro mnamo Desemba 14, 2025. (Picha na Jabir Johnson/JAIZMELA News)

Shauku Kubwa waliyokuwa nayo Wamachame ya kumsimika Mangi wa 52 wa jamii hiyo imetimizwa baada ya Mangi Gilbert Gilead Shangali kusimikwa rasmi kuiongoza jamii hiyo baada ya miongo mitano ya kusubiri hafla hiyo.

Mwenyekiti wa Machifu nchini Tanzania Frank Marealle ndiyo aliyeongoza hafla ya kumsimika Mangi Gilbert Shangali iliyofanyika katika eneo la Isaleni, Wari-Machame wilayani Hai mkoani Kilimanjaro.

Tukio hilo la lililokuwa na mvuto wa aina yake kulishuhudiwa viongozi wa serikali, dini na wanasiasa mbalimbali wakihudhuria hafla hiyo ambayo ilionyesha utamaduni halisi wa jamii hiyo.

Akizungumza katika hafla hiyo ambayo Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu alikuwa mgeni rasmi, Mkufunzi wa Chuo Kishiriki cha KCMC Tumaini University Harold Shangali alisema mchango wa Rais Samia Suluhu Hassa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  aliyepewa na machifu jina laChifu Hangaya ni mkubwa katika kuendeleza utamaduni wa Mtanzania.

Chifu Marealle alimpaka mafuta ya Simba, Mangi Gilbert Shangali pia alimvika vazi la ngozi ya Chui kisha kumkalisha katika kiti cha asili cha Umangi wa Machame, huku wazee wengine wa koo za Kimachame walimkabidhi mkuki na usinga.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu alimkabidhi Mangi Gilbert Shangali chombo cha asili cha kuweka chakula ikiwa ni ishara ya utoshelevu katika masuala ya lishe kwa Wamachame.

Hafla hiyo ilisindikizwa na unywaji wa Supu, mbege na nyama choma ya ng’ombe na mbuzi. Takribani ng’ombe 10 zilichinjwa kwa ajili ya kumsimika Mangi Gilbert Shangali.

Mbali na uwepo wa watu mbalimbali, jamii ya wanyamwezi wa Tabora, wahangaza kutoka magharibi mwa ziwa Victoria, Wamasai kutoka Arusha na Manyara walihudhuria hafla hiyo kuonyesha umoja na mshikamano wa kiutamaduni wa Kitanzania unaoundwa na jamii 123.

Kwa upande wao Rebeka Matayo Ndalishao alisema hafla ya kumsimika Mangi Gilbert Shangali linawakumbusha kuwa utamaduni wa Wamachame wa kuwa na kiongozi thabiti anayesimamia maadili na mwenendo mzima wa jamii hiyo.

Yunisi Munisi anaanza kwa kuimba Kimachame akielezea wito wa jamii kutunza mazingira na maadili ya jamii yao.

Simbo Jacob Salema anasema Mangi katika jamii ya Kimachame walikuwa na kazi kubwa ya kulinda jamii na kutunza maadili.

Mangi katika jamii ya Wachagga ni viongozi wa jamii na mara nyingi huwa na jukumu la kusimamia amani, utulivu, na utawala katika jamii zao. Wanatoa maamuzi ya kisheria na kijamii kuhusu migogoro, urithi, ndoa, na haki za jamii. Pia Mangi huhakikisha kuwa tamaduni za asili hazipotei na kwamba vizazi vipya wanajua na kuenzi urithi wao.

Utamaduni na maisha ya watu wanavyoishi Machame kwa kiasi kikubwa ni matokeo ya uongozi wa Mangi. Aliruhusu dini ya Ukiristo iingie Machame. Alilazimisha watu wa Machame kwenda kukamata ardhi sehemu za tambarare, aliruhusu shule zianzishwe, n.k

Credit to: Jabir Johnson, +255 693 710 200



0 Comments:

Post a Comment