Tuesday, December 24, 2024

AMEC Kilimanjaro yawatoa hofu waumini kuhusu uhuru wa kuabudu

Mkuu wa Jimbo la Kilimanjaro wa Kanisa la Africa Mission Evangelism (AMEC) Mchungaji Wilson Kawiche amewataka waumini wanaojiunga na kanisa hilo kutambua kuwa Katiba ya Jamhuri  ya Muungano wa Tanzania inawalinda kwa uamuzi wao wa kufuata Imani ya dini wanayoitaka kuitumikia.

Akizungumza katika Hafla ya kumsimika Mchungaji Paul Assey wa AMEC Usharika wa Kileo, wilayani Mwanga iliyofanyika mnamo Desemba 22, 2024 Mchungaji Kawiche alisema Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua uhuru wa mtu kuabudu Imani ya dini anayotaka bila kikwazo chochote.

Mchungaji Kawiche alisema haki hiyo inapatikana katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hasa katika Ibara ya 19, ambayo inasema kwamba kila mtu ana haki ya kuwa na uhuru wa kutafuta, kupokea na kutoa maoni na habari, pamoja na uhuru wa kuamini na kutekeleza dini au imani anayotaka, bila kujali dini, kabila, au hali nyingine yoyote ya kibinafsi.

Aidha Mkuu huyo wa Jimbo la AMEC Kilimanjaro aliyasema hayo wakati akitoa nasaha kwa waumini walioamua kurudi kuhudumu na kanisa hilo  ambapo Mchungaji Kawiche aliwatoa hofu kuhusu uamuzi wao wa kumrudia Mungu wao.

Waliorudi hemani mwa Bwana walitoa shukrani zao za dhati kwa kanisa la AMEC Kileo kuwapokea na kuwafanya wapya tena ndani ya Yesu Kristo.

Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Kanisa la Furaha Tanzania Mchungaji Jones Mollah aliyealikwa kwenye hafla hiyo ya kumsimika Mchungaji Assey aliwata waumini hao waliorudi kundi kutambua kuwa walikuja kwa miguu yao wenyewe na kwamba wasitishwe na hila za adui shetani kwamba hawatafanikiwa hemani mwa Bwana.

Katika hafla hiyo Mchungaji Assey alikula kiapo cha kulitumia Kanisa la AMEC Kileo kwa uaminifu wote na kulihudumia kusanyiko la watu wa Mungu

Askofu Mkuu wa AMEC Tanzania Mchungaji Baltazar Kaaya alimsimika Mchungaji Assey kwa sheria za kanisa hilo ambapo hafla hiyo ilisindikizwa na Uimbaji kutoka kwaya ya Mtiini Mungu ya AMEC Ulshoro mkoani Arusha.

Kwa ujumla, uhuru wa imani nchini Tanzania ni haki muhimu inayotambuliwa na Katiba na sheria, na inalinda haki ya kila mtu kuamini na kutekeleza imani yake kwa huru, ingawa kwa baadhi ya nyakati, kuna mipaka ili kulinda utawala wa sheria na haki za wengine.

AMEC inaundwa na takribani makusanyiko 100 ya Wakristo wa Kilutheri katika eneo la Kaskazini mwa Tanzania. Limesambaa zaidi katika eneo la chini ya Mlima Meru mkoani Arusha na sasa linaendelea kuongezeka kuzunguka Mlima Kilimanjaro na tambarare kuelekea Upareni.

Credit to: Jabir Johnson, +255 693 710 200 jabirjohnson2020@gmail.com

0 Comments:

Post a Comment