Sunday, December 15, 2024

Wahitimu 3,246 watunukiwa shahada mbalimbali Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi

Wakati, Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), kikifikisha umri wa miaka 10 tangu kupewa ithibati ya kuwa chuo kikuu kamili, Spika mstaafu wa Bunge, Anne Makinda, amewatunuku kwa mara ya kwanza wahitimu 3,246 shahada mbalimbali.

Kati ya wahitimu hao wa fani mbalimbali, wamo wanataaluma sita waliotunukiwa Shahada ya Udaktari wa Falsafa (PhD).

Idadi hiyo ya wahitimu inazidi kuongezeka mwaka hadi mwaka, tangu Makinda aliporithi mikoba ya aliyewahi kuwa Katibu Mkuu Mtendaji wa kwanza wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. Pius Msekwa na Msaidizi wa karibu wa Hayati, Mwalimu Julius Nyerere.

Akizungumza Novemba 13, 2024 katika mahafali ya 10 ya chuo hicho, Mwenyekiti wa Baraza la chuo hicho, George Yambesi, amemweleza Makinda kuwa, kati ya wahitimu hao, atawatunuku astashahada, stashahada, shahada za awali, stashada za uzamili, shahada za umahiri na shahada ya uzamivu.

Wanataaluma waliotunukiwa Shahada hiyo ya PhD, ni pamoja na Dkt. Alex Nyagango, Mtawa Dkt. Bernadette Temba, Dkt. Emmanuel Mkilia, Dkt. George Budotela, Dkt. Julieth Koshuma na Dkt. Pamela Liana.

Naye, Makamu Mkuu wa Chuo hicho cha MoCU, Prof. Alfred Sife, alimweleza Spika mstaafu Makinda, wanazuoni hao na wahitimu wengine, ni alama tosha ya mafanikio ya kujivunia katika maisha yao, kwani inatokana na juhudi na maarifa waliyowekeza.

Credit to: Elizabeth Mkumbo, Freelancer; Jaizmela News



0 Comments:

Post a Comment