Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Masumbeni wakiwa katika viunga vya shule yao kabla ya kuzuia kuhudhuia masomo kutokana na mgogoro wa shule, kijiji, na mwekezaji. |
Wanafunzi wa Shule ya Msingi
Masumbeni iliyopo Kata ya Kifula wilayani Mwanga, Kilimanjaro wameshindwa
kuhudhuria masomo katika vyumba vya madarasa shuleni hapo kwa takribani siku
100 kutokana na mgogoro wa eneo baina ya shule, kijiji na mwekezaji.
Hayo yalijiri kwenye mkutano wa
kawaida wa baraza la madiwani wa halmashauri
ulioketi katika ukumbi wa mikutano wa shule ya sekondari Mwanga, kwa
ajili ya kujadili shughuli mbalimbali za
maendeleo kwa kipindi cha robo ya tatu ya mwaka 2022/23.
Akizungumza katika mkutano huo Diwani
wa Lembeni Alex Mwaipopo aliwasilisha hoja yake binafsi ya kutaka kufahamu ni
kwa namna gani serikali inasaidia ili eneo la shule linabaki kuwa mali ya shule
hiyo.
“Kwa kipindi kirefu kumekuwepo na mgogoro hususani kwenye eneo la shule ya msingi Masumbeni iliyopo kata ya Kifula kumegwa na kupewa taasisi ya Islamic Development Foundation , mgogoro huu ambao serikali ya kijiji bila ya kuishirikisha shule, au halmashauri ya wilaya, kijiji kilimega eneo la shule kwa taasisi binafsi , taasisi hii ilipeleka shauri mahakamani na kushinda shauri hilo,” alisema Diwani Mwaipopo.
Diwani huyo aliongeza kuwa IDF
ilipolipeleka shauri hilo mahakamani na kushinda, Mahakama Kuu iliikabidhi
taasisi hiyo eneo ambalo ndani yake lina madarasa , myumba moja ya mwalimu.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu
Dina Ezekiel wa Shule ya Msingi Masumbeni aliyeitwa katika mkutano huo alisema,
“Eneo hili ni mali ya shule limeporwa na watu wanaojiita ni IDF na mgogoro huu
ulianza tangu mwaka 2014 , tulienda Mahakama ya Mwanzo Mwanga, na hukumu
ikatoka tukawa tumeshinda kesi hiyo.”
Mwalimu Mkuu huyo aliongeza
kuwa mwekezaji huyo hakukata rufaa ya shauri hilo akaenda katika mahakama kuu
mkoa wa Kilimanjaro na kufungua mashtaka mapya kuhusu eneo hilo ikiwa ni pamoja
na kuishtaki serikali ya kijiji.
“Serikali ya kijiji ndiyo
waliohusika kumpa hilo eneo la shule kinyemela bila kuishirikisha kamati ya
shule wala uongozi wa wowote. Mali zilizochukuliwa na mwekezaji huyo ni pamoja
na vyumba viwili vya madarasa ya wanafunzi wa shule ya awali, nyumba ya
mtumishi yenye vyumba vitatu na sebule,
miti , ofisi ya mwalimu,” alisema Mwalimu Mkuu.
Aidha Mkurugenzi wa Halmashauri
ya Wilaya ya Mwanga Mwajuma Nasombe
alikiri kuwepo kwa wanafunzi ambao wameshindwa kuingia madarasani kwa miezi
mitatu baada ya kufungwa utepe na kusimamisha shughuli zote zilizokuwa
zikifanyika katika eneo hilo ambalo taasisi ya IDF ililichukua.
“Watoto wa darasa la awali
hawana madarasa ya kusomea kwa sababu mwekezaji huyo alifunga utepe, na ni
marufuku kuingia eneo hilo, madarasa hayo…kwa sasa hayawezi kutumika, mali
mbalimbali za shule ikiwemo miti, imechukuliwa, pamoja na nyumba ya mtumishi,
imechukuliwa,” alisema Nasombe
Akitoa ufafanuzi wa kisheria,
Mwanasheria wa Halmashauri hiyo Edwin Rusa alisema baada ya taarifa kupatikana
kwa eneo la shule kumegwa shule walianza kufanya ufuatiliaji ambapo walizuia
IDF kuingia katika eneo hilo.
“Ilipofika mwaka 2018 Taasisi
ya Islamic Develompment Foundation ilipeleka shauri mahakama kuu ikiishtaki
serikali ya kijiji pamoja na Bw. George Mfagavo na ilipofika mahakamani kwa
bahati mbaya kijiji hakikuitaarifu halmashauri kwamba kuna kesi ambayo
inaendelea mahakamani,” alisema mwanasheria huyo.
Aidha Rusa aliongeza kuwa mnamo
mwaka 2019 mahakama ilitoa maamuzi kwamba eneo hilo ni mali ya IDF na baada ya
halmashauri kupata taarifa hizo ilipeleka maombi mahakama kuu (objection
proceeding) na mahakama iliyakataa
maombi hayo.
“Baada ya kuwa imekataa maombi
hayo taasisi ya IDF ilipeleka maombi ya kutekeleza hukumu, ilipofika mwaka 2022
tulirudi tena mahakamani kama halmashauri tukapeleka maombi ya kupinga eneo
hilo kukabidhiwa kwa taasisi hiyo, lakini kwa mara ya pili tena maombi yetu
yakawa yameshindikana,” alifafanua mwanasheria huyo.
Hadi sasa haijajulikana ni lini
zuio hilo litaondolewa ili wanafunzi waendelee na masomo yao kama kawaida
katika shule ya Msingi Masumbeni.