Tuesday, September 13, 2022

JAMES MMANDA: Milioni 70 zilivyofuta ndoto zake baada ya kukatwa miguu-1

Hiki ni kisa cha kweli kilichomkuta kijana James mkazi wa mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro…Nani alimsaliti kijana huyu mwenye umri wa miaka 37 afike hapo alipofikia? ANKO TUNUNU anaanza katika sehemu ya kwanza ya makala haya…

 

Tulipokuwa shuleni tulikuwa tukifundishwa methali, vitendawili, misemo na mambo kadha wa kadha. Katika kipengele cha methali miongoni mwao ilikuwa ni “Hujafa, Hujaumbika”.

Maana yake halishi ni kwamba mwili wa binadamu unaweza kubadilika kimaumbile wakati wowote angali akiwa hai.

Hivyo basi haifai kwa sababu yoyote ile kumcheka, kumdhihaki au kumkejeli mtu ambaye ana ulemavu wa kiungo mwilini mwake.

Aliyekufa ndio amekamilika, safari yake imefika mwisho. Mfuatiliji wa makala haya utakubaliana name na methali hii kwa asilimia mia moja, utapofuatilia kisa hiki cha kweli kilichompata kijana anayefahamika kwa jina la James Severin Mushi (37) mkazi wa Moshi katika mkoa wa Kilimanjaro.

Watu wengi hupewa sifa na heshima wanazostahili wakishakufa.

Wakati wa uhai wao watu huwachukulia "poa", hawautambui au kuuthamini mchango wao mpaka wakishakufa na pengo lao kuonekana.

Watu wachache sana katika historia walifanikiwa "kuumbika" angali wakiwa hai.

Kwa haraka watu wanaokuja kichwani ni kama Nelson Mandela, Michael Jackson, Steven Hawkings, Muhammad Ali na wengineo.

Wapo pia wenye bahati zaidi ambao wanapewa tuzo za heshima sana au kupendwa na mamilioni ya watu angali wakiwa hai kama Barak Obama, Pele, Beyonce na kadhalika.

Kisa hiki cha kweli cha kijana James kinaanzia katika kivuko cha waenda kwa miguu cha Karanga-Magereza mjini Moshi mnamo Aprili 2003 majira ya saa 11 jioni wakati akitoka shule.

Wakati huo alikuwa akisomea katika shule ya Ufundi ya Moshi  masuala ya ufundi bomba (Plumbing).

James anasema, “Nakumbuka ilikuwa siku ya Ijumaa mida ya saa 11 jioni katika kivuko cha waenda kwa miguu eneo la Karanga nikiwa na baiskeli basi lilinigonga.”

Muathirika huyo ambaye kwa sasa hana miguu yake ya asili, alijikuta akiwa katika Hospitali ya KCMC iliyopo mjini Moshi akiwa kwenye vitanda vya hospitali hiyo huku maumivu makali yakiendelea katika mwili wake.

James anasema machozi yalizidi kutoka baada ya kugundua kuwa maumivu makali sio pekee yamesababishwa na ajali kama ajali bali ni baada ya taa ya mwili (macho) kuangaza katika mwili wake na kujikuta hana miguu yote miwili.

“Baada ya kupelekwa hospitalini na kufika huko miguu ilikuwa haina uwezo tena wa kutibika isipokuwa kukatwa…machozi yalinitoka sikujua la kufanya,” anasimulia James.

ITAENDELEA…

 

0 Comments:

Post a Comment