|
Vijana wakifuatilia ratiba ya mechi kwa ajili ya ubashiri
|
Ubashiri katika michezo nchini
umekuwa maarufu kwa jina la ‘mkeka’ au katika maeneo mengine umekuwa
ukifahamika ‘Kwa Mhindi’; itakumbukwa kwamba mkeka ni kitu kama jamvi
kinachoshonwa kutokana na kili na hutumika kwa kazi mbalimbali kama vile
kukalia au kutandika kitandani.
‘Sports Betting’ iliitwa mikeka kutokana na karatasi zinazobandikwa katika
ukuta wa matangazo katika kituo cha michezo ya kubahatisha ikionyesha mechi
mbalimbali zinazotarajiwa kuchezwa. Lakini tangu mwaka 2013 ilipoanza kushika
kasi michezo hiyo katika medani ya soka hadi sasa imekua kwa kiasi kikubwa.
Hivyo ukisikia ‘Mbuzi kala
mkeka’ au ‘ukisikia mhindi amenichania mkeka’ ujue mhusika aliyeweka pesa kwa
ajili ya mchezo husika basi ndio ameshindwa kutabiri vizuri na pesa aliyoweka
imekwenda na maji;
Kwa sehemu kubwa ya watu
duniani, michezo ya kubahatisha ni burudani maridhawa isiyo na madhara, yaani
kwao ni njia moja ya kujifurahisha au kupitisha muda.
Msingi wa makala haya ni kutaka kuangazia kama sheria kanuni na taratibu za
michezo hii ya kubahatisha zinafuata na kusimamiwa kikamilifu, hususani kwa
washiriki wa michezo hiyo. Hii inatokana na ukweli kwamba maendeleo makubwa ya
simu yamekuwa makubwa ambapo mshiriki anaweza ku-beti hata akiwa nyumbani
kwake, au kichochoroni.
Jambo la kuzingatia hapa ambalo
litaufanya mjadala huu uendelee zaidi je, watanzania wanaelewa kuwa ‘mikeka’
ni maalumu kwa ‘leisure’ na ‘entertainment’ au wao wanaelewa nini kuhusu
hili hususani kwa vijana walio chini ya umri wa miaka 18.
Pia majina ya wahusika
yatahifadhiwa hususani wale walio chini ya umri wa miaka 18. Aidha kinachovutia
zaidi ni kwamba hata serikali inatambua kuwa michezo ya kubahatisha ni chanzo
kikubwa cha mapato.
MAMLAKA YA MAPATO TANZANIA INAZUNGUMZIAJE ?
Katika taarifa yake kwa
umma, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Maapto Tanzania (TRA) Dkt. Edwin Mhede anaweka
bayana kuhusu namna ambavyo michezo hii ya kubahatisha inaongeza mapato,
anasema, “kodi ya michezo ya kubahatisha ni
kodi inayotozwa kwenye
mapato yatokanayo na michezo ya kubahatisha. Kodi hizi ni za aina mbili; Kodi
ya Michezo ya Kubahatisha (Gaming Tax) - Hii ni kodi anayotozwa mwendeshaji wa
mchezo wa kubahatisha kutokana na mapato yake yatokanayo na michezo ya
kubahatisha.”
Pia Dkt. Mhede anaongeza,
“Kodi ya Michezo ya Kubahatisha kwenye Zawadi (Gaming Tax on Winnings), Hii ni
kodi anayotozwa mchezaji baada ya kushinda zawadi ya mchezo wa kubahatisha.”
Kwa mujibu wa TRA aina ya
michezo inayotozwa kodi ya aina hiyo ni Kasino (Casino), Kasino ndogo (Mini
Casino/Forty machines sites), Michezo ya Kubashiri Matokeo (Sports Betting), Michezo
ya Machine (Slots machines/route operations), Bahati Nasibu ya Taifa (National
lottery) na Bahati nasibu ya kutumia ujumbe mfupi wa simu.(SMS lottery)
BODI YA MICHEZO YA KUBAHATISHA TANZANIA INATOAJE
LESENI?
Bodi ya michezo ya
kubahatisha Tanzania (Gaming Board of Tanzania), inatoa maelekezo ya utoaji wa
leseni kuwa leseni/vibali vya kuendesha shughuli za michezo ya kubahatisha
hutolewa na gaming board of tanzania baada ya mwombaji kukidhi vigezo
vilivyoainishwa kisheria ikiwa ni pamoja na kufanyiwa upekuzi wa kina
(background check).
Marekebisho ya Sheria ya
Leseni (Business Licensing Act no. 25 of 1972) yaliyofanyika mwaka 2003 kupitia
Finance Act No. 15 ya mwaka 2003, kifungu 5(1)(f), yaliondoa michezo ya
kubahatisha katika orodha ya uhitaji wa leseni za biashara, isipokuwa leseni
inayotolewa na Gaming Board.
WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO TANZANIA INACHUKULIAJE MICHEZO YA
KUBAHATISHA?
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha
Mawasiliano Serikalini wa Wizara ya Fedha na Mipango, Benny Mwaipaja katika
taarifa yake kwa umma aliweka bayana ongezeko la maduka ya michezo ya
kubahatisha na namna inavyoongeza pato la taifa.
“Serikali imetolea
ufafanuzi juu ya suala la michezo ya kubahatisha kuwa ni moja ya shughuli za
kiuchumi, zinazoendeshwa kwa mujibu wa sheria kama shughuli zingine. Michezo
yote ya kubahatisha ikiwemo Kamari (slots machines) inaendeshwa kwa mujibu wa
Sheria ya Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Namba 4 ya mwaka 2003, Sura 41 pamoja
na Kanuni zake,” alisema Mwaipaja.
Katika Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, aliwahi
kujibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Asha Abdullah Juma, aliyetaka kujua
mpango wa Serikali wa kudhibiti michezo ya kubahatisha ambao alisema umekuwa ukiwakosesha
amani wazazi na jamii nzima, kwa kuchangia uvunjifu wa maadili na nguvu kazi ya
vijana inayopotea kwa kucheza michezo hiyo badala ya kushiriki katika
uzalishaji.
Dkt. Kijaji alisema sheria
inakataza watoto wenye umri chini wa miaka 18 kushiriki, kuingia, kukaa au
kuzururazurura karibu na maeneo ya michezo ya kubahatisha.
“Mtu yeyote atakaye ruhusu
mtoto chini ya miaka 18 kushiriki, kuingia au kukaa karibu na eneo la Mchezo wa
Kubahatisha, anahesabika kafanya kosa na anastahili kulipia faini ya shilingi
500,000/- au kifungo kisichopungua miezi mitatu au vyote kwa pamoja” aliongeza
Dkt. Kijaji
“Endapo kosa hilo
litafanywa na mwendesha mchezo wa kubahatisha, Bodi ina mamlaka kisheria
kumfutia leseni. Hivyo basi, wajibu wa Serikali ni kuzuia watoto na vijana
walio chini ya miaka 18 kucheza michezo ya kubahatisha. Natoa rai kwa wazazi na
walezi kuwazuia wao kucheza michezo hiyo” alisisitiza Dkt. Kijaji
VIJANA CHINI YA UMRI WA MIAKA
18
Mnamo mwaka 2015 katika
kupitapita kwangu nilikutana na kijana huyu aliyejitambulisha kwa jina Justin
ukimuangalia ana umbo la miaka 18 lakini katika uhalisia wake ana miaka 16
hivi. Nilijuaje?
Nilimuuliza swali hili,
ulizaliwa lini akakataa kuniambia, nikabadilisha swali umesoma hadi kidato cha ngapi?
Justin akasema ameishia darasa la saba.
Nikaongeza swali jingine, lini
ulimaliza darasa la saba akasema 2013 na hakufanikiwa kwenda sekondari kutokana
na ugumu wa maisha ikabidi aendelee kufanya kazi mbalimbali za kujitafutia
kipato.
Justin ambaye kazi yake kubwa wakati
huo ilikuwa ni kuuza maandazi na chai majira ya asubuhi katika maeneo ya
Zakheim, jijini Dar es Salaam aliniambia kuwa ‘ku-beti’ yaani kucheza mikeka
hakujamsaidia kwani tangu aanze kujiingiza katika suala hilo ameshinda mara
mbili.
Kwa uchungu mwingi kijana huyo
alisema kwamba ametumia kiasi kikubwa cha fedha kuwekeza ili atoke
kimaisha kwani aliwaona wenzake wakijishindia zaidi ya shilingi 100,000/=
za Tanzania.
Kibaya zaidi Justin alisema
kiwango alichoshinda kilikuwa ni shilingi 2,000/= akilinganisha na kiasi cha
fedha zaidi ya shilingi 30,000/= alichotumia katika ‘ku-beti’.
Alipoulizwa anakozitoa fedha
hizo Justin hakutaka kuweka bayana lakini kwa uchunguzi wa haraka haraka
nikagundua kuwa amekuwa akitumia mtaji wake wa maandazi na chai kwenda kucheza.
Mambo hayo!
Bado
niliendelea kuzunguka zunguka katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam
mnamo mwaka 2018 wakati wa Kombe la Dunia lililofanyika Russia nilishuhudia
jinsi ambavyo vijana wakichakarika ‘Ku-beti’ nani ataibuka mshindi wa mchezo
huu na ule na hata bingwa wa fainali hizo ambayo ilikuwa ni timu ya taifa ya
Ufaransa likiwa ni taji lake la pili baada ya lile la mwaka 1998.
Nilikuwa nikiishi Tandale kwa
Tumbo, duka la ‘Ku-beti’ halikuwa mbali sana na nilipokuwa nikiishi umbali wa
mita 300 hivi tukiwa katika duka hilo kila mtu alikuwa bize na kutazama mechi
zitakazochezwa huku akiwa na kikaratasi na peni, binafsi nilikuwa sichezi ila
nilikuwa maarufu sana eneo hilo wakiiniita ‘Jeshi la Mtu Mmoja’
Sababu ya kuniita ‘Jeshi la Mtu
Mmoja’ ni kutokana na uwezo wa kubashiri matokeo ya mechi husika ya Kombe la
Dunia, sasa nikajifunza jambo mara baada ya kijana mmoja mwenye umri wa miaka
17 kunifuata na kuniambia, “Kaka yaani leo umenipiga tafu kwelikweli, ilikuwa
nife pale yaani Mhindi angenichania mkeka wangu, usingetabiri mechi zile mbili
yaani buku tano langu lingeniuma hatari. We bro jeshi la mtu mmoja.”
Nilicheka sana baada ya maneno
ya kijana yule nikamuuliza, “Una umri wa miaka mingapi? Usinifiche.” Kijana
yule akawa na wasiwasi mkubwa kwamba ninaweza kumharibia, nikamtia moyo kuwa
sitaweza kufanya hivyo, akasema, “Ukweli bro mimi nina miaka 17 mimi nilizaliwa
mwaka 2001…”
Kijana yule wa kiume akasema, “Ku-beti
mi alinifundisha rafiki yangu mmoja wa kitaa ambaye yeye alikuwa mzoefu wa ku-beti,
nilikuwa nikimuona akiwa na fedha kibao, lakini kuna siku unamkuta hana akienda
ku-beti ana mpunga wa elfu 20, au zaidi kulingana na mechi alizobeti.”
“Nimekuwa nikishinda sio mara
kwa mara lakini naona inanisaidia kinyama, si unajua tena familia zetu bila
hela mambo hayaendi, shuleni utaendaje wakati mzazi kila siku anakwambia hana
hela, so lazima utafute namna ya kupata pesa sasa ku-ti licha ya kwamba sio
rahisi inategemea na bahati yako lazima uvumilie kwa hali zozote zile,”
alisema.
Je, wazazi wanasemaje kuhusu
michezo hii ya kubahatisha maarufu kama ‘Ku-beti’. Tutaendelea katika makala
yajayo.
Imetayarishwa na Jabir Johnson,
mwandishi wa habari nchini Tanzania. Baruapepe: jabirjohnson2020@gmail.com
MAKALA ZINAZOHUSU SPORTS BETTING au KU-BETI
Ku-beti kunatupeleka wapi?-2
Ku-beti kunatupeleka wapi?-3
Ku-beti kunatupeleka wapi?-4