Ukweli na Kuheshimiana ni kiini ujenzi wa jamii zetu

Ulimwenguni kwa sasa kumejaa habari potofu na upotoshaji, ni muhimu kuhakikisha kwamba ukweli na kuheshimiana vinakuwa kiini kwa ujenzi wa jamii zetu.

Mapambano dhidi ya Habari za Uongo hayapaswi kukoma

Habari za uongo, habari za uongo zinazosambazwa kwa lengo la kumdhuru mtu au jambo fulani, huifanya jamii kuwa na sintofahamu. Zinaweza kutumika kwa madhumuni ya kiitikadi, kisiasa au hata uhalifu, kama vile ulaghai mtandaoni unaolenga kuiba data ya kibinafsi.

Utandawazi na Athari zake katika Uandishi wa Habari

Katika jamii yetu ya kisasa, ambapo habari ziko kila mahali na zinaweza kupatikana kwa kila mtu, mara nyingi ni ngumu kutofautisha kati ya vyanzo vya kuaminika na habari bandia.

Uandishi wa Habari nguzo msingi mkuu kwa ujenzi wa jamii inayojitambua

JAIZMELA blog ni miongoni mwa vyanzo vya habari, zilizochakatwa kwa kuzingatia miiko ya uandishi wa habari.

Mila na Desturi ni nguzo muhimu

Mila na desturi ni nguzo muhimu sana katika utamaduni wa jamii yoyote ile; mila ni sawa na sheria zisizoandikwa. Mila ni taratibu za maisha na mwenendo zinazofuatwa na jamii fulani katika utendaji kulingana na historia na utamaduni wao. Mila zinatambulisha maadili ya jamii husika, huelezea namna jamii inavyoendesha mambo yake.

Saturday, September 29, 2018

Kanisa Katoliki kufanya maombi mwezi mzima

Papa Francis
Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis amewaomba waumini bilioni 1.3 wa Kanisa hilo duniani kuchukua muda wao katika mwezi mzima wa Oktoba kufanya sala maalum ya kuliombea kanisa hilo linalokumbwa na kashfa. 

Taarifa kutoka makao makuu ya Kanisa Katoliki mjini Vatican iliyosomwa na Father Fernando Karadima, (88) imesema, Papa ameamua kuwaomba waumini wote kote duniani kusali rosari kila siku kupitia kwa Bikira Maria katika mwezi huu wa Oktoba katika kile alichokitaja kulilinda Kanisa dhidi ya shetani. 

Aidha waumini wa Kanisa Katoliki wametakiwa kuzingatia katika sala hizo kutambua dhambi, makosa na madhila yaliyofanywa katika kipindi cha nyuma na sasa ili kuweza kupiga vita maovu. 

Sala hizo maalum zinasadifiana na mkutano wa kilele wa maaskofu wa Kikatoliki watakaokutana kuanzia tarehe 3 Oktoba hadi 28 kujadili kashfa ya baadhi ya mapadri na maaskofu kuadiwa kuwanyanyasa kingono waumini wao hasa watoto, katika nchi kadhaa ikiwemo Marekani, ujerumani, Chile na Uholanzi.

Tanzania rasmi mwenyeji michuano ya CAF U17 2019


Nchi zilizofuzu CAF U17 2019
-Angola
-Cameroon
-Guinea
-Morocco
-Nigeria
-Uganda
-Senegal
-Tanzania (Host)

Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF)imeithibitisha rasmi Tanzania kuwa wenyeji wa Fainali za Afrika za Vijana zitakazofanyika mwakani.

Kikao hicho cha Kamati ya Utendaji kimekutana kwa siku mbili huko Sharm El Sheikh,Misri. Kupitia sauti ya Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa,Serikali ya Tanzania ilimthibitishia Rais wa CAF Ahmad Ahmad utayari wa kuwa wenyeji wa mashindano hayo na kwamba tupo tayari kufanya juhudi kubwa za maandalizi.

Michuano hiyo itafanyika kuanzia April 14 mpaka April 28, 2019. Timu zilizofuzu kucheza fainali hizo ni Angola, Cameroon, Guinea, Morocco, Nigeria, Uganda, Senegal na wenyeji Tanzania. Droo kwaajili ya mashindano hayo itafanyika Desemba 20 nchini Tanzania.

Wakati wa michezo ya kufuzu kucheza fainali hizo nchini Tanzania UEFA walihusika katika upande wa fedha na ufundi ambapo wataalamu wa ufundi wa UEFA walishirikiana kwa karibu na wale wa CAF.  Zoezi la kupima umri(MRI) katika michezo hiyo ya kufuzu imefanya shindano hilo kuwa na thamani zaidi.

Thursday, September 27, 2018

Nyambui aendelea kuinoa Brunei


Kocha wa timu ya taifa ya riadha ya Brunei Suleiman Nyambui akiwa na wachezaji wake baada ya mazoezi hivi karibuni. Nyambui ni katibu mkuu wa zamani wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), akiwa na rekodi ya kutwaa medali ya olimpiki katika mita 5,000 jijini Moscow mwaka 1980.

Wasifu wa Suleiman Nyambui
Nyambui alizaliwa Februari 23, 1953 Majita, Musoma mkoani Mara. Aliacha shule na kuanza kazi ya uvuvi katika  Ziwa Victoria wilayani Ukerewe mkoani Mwanza. Baadaye alijiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ambako alijifunza mambo mbalimbali ya kulisaidia taifa. 

Pia aliwahi kuwa mwalimu katika Shule ya Bukumbi iliyopo kilometa 32 kutoka jijini Mwanza kabla ya kukwea pipa kwenda nchini Marekani.  Akiwa nchini Marekani alisoma katika Chuo Kikuu cha Texas El Paiso (UTEP) shahada ya kwanza na uzamivu. Baada ya kumaliza mkataba wake na Bahrain alirudi Tanzania na kushika wadhifa wa Katibu Mkuu wa RT hadi alipoachia Juni mwaka huu.

Muda mzuri aliowahi kukimbia
Mita 1500:  dakika 3:35.8
Maili:  dakika 3:51.94
Maili 2:  dakika 8:17.9
Mita 5000:  dakika 13:12.29
Mita 10,000: dakika 27:51.73
Marathon:  saa 2:09:52



SULEIMAN NYAMBUI

Ujerumani kuwa mwenyeji wa Euro 2024


Rais wa Shirikisho la Soka la Ulaya (UEFA). Aleksander Ceferin ametangaza fainali za mwaka 2024 za mataifa ya Ulaya zitachezwa nchini Ujerumani. Ceferin alitangaza uamuzi huo jijini Nyon nchini Uswisi mbele ya mataifa mawili yaliyokuwa yakiwania nafasi hiyo. 

Katika kura iliyopigwa na wajumbe 17  wa Kamati Kuu ya UEFA ilithibitisha ushindani miongoni mwa mataifa mawili yaliyokuwa yakiwania nafasi hiyo Ujerumani na Uturuki. Ujerumani ilipata kura 12 huku Uturuki ikiambulia kura tatu na moja ikiharibika. Ceferin alizipongeza nchi.

Nyota ya Usain Bolt yaanza kung'ara A-League




Safari ya soka ya Usain Bolt imeanza akicheza dakika 45 za kwanza akiwa na North Shore Mariners kwenye mchezo wa kirafiki ambao haukuwa na mashabiki dhidi ya Newcastle Jets. 

Nyota huyo aliyestaafu riadha alianza na Mariners Agosti mwaka huu akicheza dakika 20 za mwisho. Emile Heskey anaamini Bolt atang'ara katika ligi kuu nchini Australia.

Ozil anogesha kinyang'anyiro cha uenyeji Euro 2024



Kamati kuu ya Shirikisho la Soka la Ulaya (UEFA) itakaa baadaye hii leo kuchagua mwenyeji wa fainali za UEFA Euro 2024. 

Tukio hilo litafanyika katika makao makuu ya shirikisho hilo mjini Nyon nchini Uswisi. Septemba 10 mwaka huu shirikisho hilo lilitangaza kuwa leo itakuwa siku muhimu kuamua nani atakuwa mwenyeji wa fainali hizo. 

Aprili mwaka huu shirikisho la soka la Ujerumani (DFB) na lile la Uturuki (TFF) yalifikisha maombi yao ya kutaka kuziandaa fainali hizo. Ujerumani wakati huo ikiitwa Ujerumani Magharibi iliandaa fainali za Euro mwaka 1988 ambazo mabingwa walikuwa Uholanzi, Uturuki hawajawahi kuandaa. 

Shirikisho la Soka la Ujerumani linamnyoshea kidole mchezaji wake aliyetangaza kustaafu Mesut Ozil kuwa kitendo cha kwenda nchini Uturuki na kuzungumza na Rais Tayyip Erdogan kabla ya Kombe la Dunia kimechangia mchuano huo kuwa mkali.
Ozil na Erdogan

Wednesday, September 26, 2018

Watanzania watakiwa kutumia Unga wa Muhogo


Unga wa Muhogo uliofungashwa vizuri
Watanzania wametakiwa kutumia Unga wa Muhogo kwa ajili ya kuzalisha bidhaa zikiwamo chapati, vinywaji na chakula cha mifugo. 

Rai hiyo ilitolewa katika semina ya waandishi wa habari na Afisa Mshauri wa Maendeleo ya Biashara kutoka Mradi wa CAVA 11 Tito Mhagama. 


Mhagama alisema wananchi wanapaswa kubadili mtazamo na kuanza kutumia unga wa muhogo kwani unaweza kutumika Kuoka bidhaa mbalimbali za chakula kama Mikate, Keki, Maandazi na Utengenezaji wa Tambi. 

Pia Unga wa Muhogo unawafaa kwa watu wasiotumia unga wa ngano, au wenye mzio na protini inayopatikana kwenye bidhaa za ngano. Mbali na hilo Mhagama alisema unga wa muhogo unawafaa kwa watu wanaopunguza uzito, au wenye ugonjwa wa kisukari. Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Ukiriguru Simon Jeremiah aliwataka wakulima kuzalisha zao hilo kwa wingi ili kuwezesha viwanda kupata mali ghafi ya kutosha. 

Katika semina hiyo Maafisa Ugani kutoka mikoa ya Mwanza, Mara, Kagera, Mtwara na Pwani pamoja na Mameneja wa Sido na Wakurugenzi wa Vituo vya Utafiti wa Kilimo wamehudhuria.

Chapati ni miongoni mwa vyakula ambavyo vinapendwa sana nchini Tanzania, mara nyingi hutengenezwa kwa unga wa ngano. Unga wa Muhogo nao unaweza kutumika kutengeneza chakula hicho

Tuesday, September 25, 2018

Chadema yazindua Sera za Chama toleo la Mwaka 2018

Mweneyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Sept 25, 2018
Uzinduzi wa Sera za Chama toleo la Mwaka 2018 umefanyika leo jijini Dar es salaam na kuhudhuriwa na  vingozi mbalimbali katika tukio hilo lililoandaliwa na CHADEMA likiongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe na kuziweka wazi sera zao ambapo wamejikita zaidi katika maeneo 12 huku wakieleza wazi namna sera hizo zitavyoweza kusaidia Watanzania.

“Mwanzoni mwa mwaka 1990 waasisi wa chama hiki, mimi nikiwa ni mmoja wao na ndio nilikuwa mdogo kuliko wote, tuliona siasa za ujamaa ambazo ndiyo ilikuwa sera ya CCM, hazifai na haziwezi kuwapelekea maendeleo Watanzania. 

Kwa pamoja tukaamua njia pekee ni kuanzisha vuguvugu la vyama vingi tukiamini kama serikali itakubali, basi tuanzishe chama cha siasa ambacho kitakuwa na sera mbadala ya ile ya ujamaa.

“Kwa hiyo mfumo wa vyama vingi ulikubaliwa, haraka tulisajili chama cha siasa cha CHADEMA na ilipofika mwaka 1993, mara tu ya kupata cheti cha usajili, tuliandaa Sera mbadala ya taifa ya mlengo wa kati ambayo ilikuwa inatofautia na ile ya ujamaa,” alisema Mbowe.


Mwenyekiti huyo ambaye ni Mbunge wa jimbo la Hai, amesema baada ya kuiandaa sera ya chama chao, walimpelekea Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere ambaye baada ya kuisoma aliikubali na kusema kuwa sera hiyo ndiyo hasa italeta maendeleo kwa Watanzania.


Akizungumza mbele ya wajumbe wa kamati kuu ya Chadema wakiwemo Mawaziri wakuu wastaafu, Frederick Sumaye na Edward Lowassa, Wabunge wanaotokana na chama hicho, wageni waalikwa wakiwemo mabalozi wa nchi mbalimbali na wananchi wa kawaida, Mbowe alisema baada ya miaka 25, chama chake kimeamua kuandaa tena sera mbadala ya taifa.


“Chama changu kimeamua kuandaa tena Sera hizi ambazo tumegusia Nyanja 12 ambazo tuna Imani zina tija kwa maslahi mapana ya wananchi na taifa kwa ujumla wake.


“Tumegusia Katiba, Utawala, Uchumi wa Soko Jamii, Siasa za ndani, Siasa za Kijamii na Afya. Lakini pia tumeangazia kwenye masuala ya Usimamizi wa ardhi, Kilimo, Miundombinu, Mazingira na mambo ya nje. Na hii sera yetu tunaiweka wazi kwa umma ili Watanzania wajue nini tunachokipigania kwenye hii nchi,” aliongeza Mbowe.


Baada ya kuzindua Sera hiyo, Mbowe amesema chama chake kimefungua rasmi milango ya kupokea maoni na ushauri juu ya sera hiyo kutoka kwenye vyama vya siasa, mashirika ya umma, taasisi mbalimbali na raia wa kawaida.


 

Merson: Sanchez alipotea kwenda Manchester United

Alexis Sanchez
Mchezaji wa zamani wa Arsenal na mchambuzi wa kandanda nchini England Paul Merson amesema mshambuliaji wa Manchester United Alexis Sanchez alipotea kutua klabuni hapo. 

Merson amesema staili ya kocha Jose Mourinho haijafanikiwa kumwonyesha Sanchez katika ubora wake. Tangu aliposajiliwa katika dirisha dogo la Januari mwaka huu ameonekana dimbani mara 17 katika Ligi Kuu na akifunga mabao mawili. 

Merson alikumbushia wakati Mourinho alivyomzima Hazard asikae kwenye ubora wake na kuongeza kuwa Sanchez alipokuwa Arsenal alikuwa mchezaji mwenye kiwango kutokana na kuwa na uhuru wa kufanya vitu tofauti na ilivyo sasa. 

Merson aliitumikia Arsenal katika nafasi ya kiungo mshambuliaji kuanzia mwaka 1985 hadi 1997 akicheza mechi 327 akifumania nyavu mara 78 na baadaye aliwahi kuhudumu katika vilabu mbalimbali vikiwamo Aston Villa na Portsmouth.

Chadema kuzindua sera za chama toleo 2018 leo


Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, Freeman Mbowe anatarajiwa kuongoza tukio la kuzindua sera za chama hicho toleo la mwaka 2018 hii leo jijini Dar es Salaam. 

Tukio hilo linatarajiwa kufanyika asubuhi ya leo huku wadau mbalimbali wakialikwa zikiwemo sekta na taasisi mbalimbali za umma, sekta binafsi, taasisi na asasi za kimataifa, balozi mbalimbali,vyombo vya habari, taasisi za dini na taasisi za kitaaluma. 

Taarifa ya chama hicho imebainisha katika tukio hilo vyombo na taasisi mbalimbali za Serikali kama Mkuu wa Jeshi la Polisi, Gavana wa Benki Kuu, Msajili wa Vyama vya siasa na taasisi nyingine zimealikwa. 

Katika uzinduzi huo Chadema itaweka hadharani misimamo ya kisera kwenye maeneo mbalimbali ya uchumi, afya, elimu na sayansi, miundombinu, maji, mfumo wa Utawala, Katiba na haki za binadamu, Masuala ya Muungano,  Mambo ya Nje na Uhamiaji, Siasa za ndani, Usimamizi wa Ardhi na Kilimo pamoja na Mazingira.    

Leo ni siku ya Wafamasia duniani

Mfamasia akimhudumia mteja wake
Imeelezwa Wafamasia wanatarajiwa kuongezeka kufikia asilimia 40 ifikapo mwaka 2030.

Rais wa Shirikisho la Kimataifa la Wafamasia (FIP) Dkt. Carmen Peña katika taarifa yake iliyotolewa kupitia wavuti ya hilo katika kuadhimisha siku ya Mfamasia Duniani imesema Wafamasia wamekuwa wakiongezeka mwaka na kwamba kuanzia 2016 na ifikapo mwaka  2030 inatarajiwa kufikia asilimia 40.


Aidha taarifa ya shirikisho hilo imesema Septemba 25 ambayo ni leo ni maalum ya Wafamasia wote ulimwenguni kuitumia kwa kutoa elimu na ushauri kuhusu utoaji wa madawa kwa madhumuni ya kuboresha afya za watu.


Hata hivyo ripoti iliyotolewa mwanzoni mwa mwezi huu jijini Glasgow, nchini Scotland katika Kongamano la 78 la Dunia katika Ufamasia na Sayansi ya Ufamasia imeweka bayana kuwa nchi zenye uchumi mdogo zimekuwa zikipambana na ukuaji mdogo wa Wafamasia.


Zaidi ya Wafamasia milioni nne ulimwenguni kote wanaadhimisha siku hii ambayo ilianzishwa mwaka 2009 jijini Istanbul nchini Uturuki na Shirikisho la Kimataifa la Wafamasia (FIP).

Sunday, September 23, 2018

Zitto Kabwe amvaa Waziri Mkuu ajali ya MV Nyerere


Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amemshukia Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa kushindwa kuwaadhibu viongozi wote waliohusika na kuzama kwa kivuko cha MV Nyerere.

Kivuko hicho kilizama Septemba 20 mwaka huu wilayani Ukerewe, Mwanza ambapo mpaka sasa idadi ya watu waliokufa inatajwa kufikia 224 ambapo leo Waziri Mkuu ameongoza mazishi ya kitaifa katika makaburi ya pamoja yaliyopo eneo la Bwisya mkoani humo jirani na ajali ilipotokea.


Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini aliandika, 

" Kwamba mpaka dakika hii hakuna aliyewasilisha barua ya kujiuzulu, Rais hajawajibisha mtu, badala yake Waziri Mkuu anawapongeza kina Mongella na Kamwele kwa kazi kubwa waliofanya. Kazi ya kuacha KUOKOA na kufanya uopoaji, Waziri Mkuu tunakuheshimu sana lakini kwenye hili si sawa."


Kivuko cha MV. Nyerere kilinunuliwa na kuanza kutoa huduma mwaka 2004. Kilifungwa injini mbili mpya zenye thamani ya shilingi milioni 19 tarehe 1 Julai 2018. Kivuko cha MV. Nyerere kina uwezo wa kubeba tani 25 sawa na abiria 100 na magari 3 kwa wakati mmoja.
Zitto Kabwe

Lacazette, Aubameyang wamkuna Unai Emery

Arsenal 2-0 Everton, Sept. 23, 2018 katika dimba la Emirates

Mabao mawili ya Mfaransa Alexander Lacazette na raia wa Gabon Pierre Emerick Aubameyang dhidi ya Everton yamemfanya kocha Unai Emery kuwa na wiki njema baada ya ushindi katika Ligi ya Europa juma lililopita. 

Ushindi huo katika dimba la Emirates unaifanya Arsenal kuwa katika nafasi nzuri ya kufukuzia ubingwa wa EPL. Lacazette na Aubameyang waliipa ushindi  Arsenal ndani ya dakika tatu katika dakika ya 56 na 59 ya mchezo.

Chelsea yashindwa mbele ya West Ham

 
Olivier Giroud akijishika kichwa akiwa haamini kilichotokea

Sare ya bila kufungana baina ya Chelsea na West Ham katika mchezo wa Ligi Kuu ya England yameifanya miamba hiyo kupunguzwa kasi ya kuwania taji hilo. 


Andriy Yarmolenko alikosa nafasi muhimu katika mchezo huo baada ya mpira wa kichwa kutoka nje kidogo ya lango. Chelsea inashindwa kupata pointi tatu kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa msimu huu. 

Hivyo juma lijalo dhidi ya Liverpool katika dimba la Stamford Bridge utaifanya The Blues kuwa kwenye wakati mgumu.
Giroud akika katikati ya wachezaji wa West Ham


Eden Hazard akiwa amezongwa na wachezaji wa West Ham

Andriy Yamolenko alipata nafasi nyingine na kushindwa kuitumia katika mchezo huo


Wednesday, September 19, 2018

Chadema yatangaza kutoshiriki chaguzi za marudio

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Freeman Mbowe

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema hakitashiriki uchaguzi wa marudio katika Jimbo la Liwale na kata 37 kwa kile wanachodai hujuma zinazofanyika wakati wa chaguzi hizo.
Akitangaza mbele ya vyombo vya habari Mwenyekiti wa Chama hicho Freeman Mbowe alisema kumekuwa na hujuma ya namna ya kuwapata wagombea hadi siku ya kutangaza mshindi na kusisitiza hujuma hizo zinafanywa na Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa mgongo wa serikali.


Aidha Mbowe alibainisha kuwa kwa sasa wataelekeza nguvu katika ujenzi wa chama kwa njia ambazo hakutaka kuziweka bayana. 


Pia Mbowe aliongeza kuwa watafungua mashtaka katika mahakama mbalimbali na kuongeza kuwa uamuzi ambao wameufanya wameuchukua kwa umakini mkubwa.

Mahakama Afrika Kusini yahalalisha matumizi ya bangi maeneo ya faragha


Mahakama ya Kikatiba nchini Afrika kusini imehalalisha utumiaji wa bangi kwa watu wazima katika maeneo faragha.

Mahakama hiyo imefikia uamuzi huo kwa kauli moja, kuruhusu watu wazima kutumia bangi wakiwa majumbani na kukuza kiasi kinachoweza kutosheleza mahitaji binafsi. Wanaharakati wanaounga mkono utumiaji wa bangi wamesheherekea uamuzi huo wa kihistoria wakisema ''sasa tuko huru''.

Akitoa hukumu hiyo Naibu jaji Mkuu, wa Afrika Kusini, Raymond Zondo, amesema sheria inayopiga marufuku watu wazima kutumia bangi ilikuwa kinyume cha katiba.

Dkt. Misanya Bingi kuzikwa leo

Dkt. Misanya Bingi enzi za uhai wake
Mwili wa aliyekuwa mtangazaji mahiri nchini na Mhadhiri wa Shule ya Habari na Mawasiliano ya Umma (SJMC) iliyo chini ya Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Dkt Misanya Bingi (47) umeagwa Sept. 18 mwaka huu katika Kanisa Katoliki la Makongo Juu liliopo Dar es Salaam na kusafirishwa kuelekea Miuji jijini Dodoma kwa ajili ya mazishi hii leo.

Dkt. Bingi alifariki dunia siku Jumapili katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na wakati wa uhai wake alifanya kazi kwenye kituo cha Radio One ambapo alitangaza vipindi mbalimbali kikiwemo kipindi cha Chemsha Bongo siku za Jumanne na Ijuma saa tatu usiku.


Hadi mauti yanamkuta alikuwa akifundisha SJMC, tawi la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alianza tasnia ya utangazaji mwaka 1996. 

Jeneza la mwili wa marehemu Dkt. Misanya Bingi ukitoka kanisani kabla ya kusafirishwa.

Viongozi wa Korea Kusini na Kaskazini wakutana Pyongyang

Moon Jae-in na Kim Jong Un
Viongozi wa Korea mbili, kusini na kaskazini wameanza mkutano wao wa kilele mjini Pyongyang kujadili juu ya kuondoa silaha za nyuklia katika rasi ya Korea pamoja na masuala mengine.

Ofisi ya rais wa Korea Kusini imesema maafisa wawili waandamizi kutoka nchi zote mbili za Korea Kaskazini na Korea Kusini watashiriki pia mkutano huo wa kilele.

Andre Borcelli ni nani?

Andre Bocelli
Nyota huyu wa muziki kutoka nchini Italia alizaliwa Septemba 22, 1958 lakini alipokuwa na miaka 12 alipoteza kabisa uwezo wa kuona kwa maana nyepesi alikuwa kipofu hadi sasa akiwa na miaka 60. Alipata upofu akiwa katika mchezo wa mpira wa miguu (soka). 

Mwimbaji wa muziki nchini Marekani Celine Dion aliwahi kusema " Kama Mungu angekuwa na sauti ya uimbaji, angeimba kama Andrea Borcelli. " Pia prodyuza David Foster aliwahi kusema kuhusu Borcelli kuwa ni mwimbaji mwenye sauti nzuri kuliko wote duniani. Hadi sasa amerekodi albamu 15 za muziki  na kuuza zaidi ya kopi zaidi ya milioni 80. 

Mwaka 1998 Bocelli alitajwa katika Jarida la People kuwa miongoni mwa watu 50 bora wanaovutia duniani. Mwaka 1999 alishiriki katika tuzo za Grammy. Katika medani hiyo ya muziki akiwa na miaka 33 alikuwa bado anapiga kinanda (piano) katika maeneo ya baa. Bocelli alizaliwa kwa wazazi Alessandro na Edi; 

Wakati akiwa  tumboni mwa mama yake, ilielezwa kuwa daktari alimtaka mamaye kutoa mimba hiyo kwani ingemletea matatizo lakini alipuuzia hatimaye alimzaa Andrea. Katika makuzi yake akiwa na familia yake alikuwa akiuza vifaa vya shambani na kutengeneza mvinyo katika kijiji kidogo cha La Sterza, Tuscany takribani kilometa 40 kusini mwa mji wa Pisa. Baba yake alifariki mwaka 2000.

Supersub Roberto Firmino aipa mwanzo mzuri Liverpool yaizabua PSG 3-2

Neymar Jr. akimliki mpira mbele ya Mohamed Salah katika mchezo wa Kundi C wa ligi ya mabaingwa barani Ulaya usiku wa Septemba 18, 2018 Anfield

Roberto Firmino akiingia kuchukua nafasi ya Daniel Sturridge
Hakika ulikuwa ni usiku mzuri kwa Liverpool katika dimba la Anfield pale walipoizabua miamba ya Ufaransa Paris Saint Germain kwa mabao 3-2 katika mchezo wa kwanza wa kundi C wa Ligi ya Mabingwa barani Ulaya. 

Pongezi kwa mshambuliaji wa Brazil akitokea benchi Roberto Firmino alipoingia kuchukua nafasi ya Daniel Sturridge na kutupia bao la ushindi katika kikosi cha Jurgen Klopp. Sturridge alianza kufungua ukurasa kwa bao la kichwa katika dakika ya 30 kabla ya James Milner hajaipa uongozi Liverpool kwa mkwaju wa penati baada ya Georginio Wijnaldum kuangushwa katika eneo la hatari. 

Mfaransa Thomas Meunier aliirudisha PSG na baadaye Kylian Mbappe aliisawazishia PSG katika dakika ya 82 kabla ya Firmino kuharibu mahesabu ya matajiri hao wa Paris katika dakika ya 90. Neymar Jr na Edinson Cavani hawakuwa na ujanja mbele ya vijana wa Klopp huku Klopp mwenyewe akikutana na Thomas Tuchel waliyewahi kufanya naye kazi walipokuwa Borussia Dortmund na kuipa mafanikio makubwa katika historia ya klabu hiyo ya Bundesliga.

Maadhimisho ya Siku ya Tembo Sept. 22 Ruvuma


Shirika  la kimataifa la uhifadhi wa mazingira(WWF), kwa kushirikiana na Mamlaka ya usimamizi wa wanyamapori (TAWA) wameandaa maadhimisho ya Siku ya Tembo kitaifa, yanayotarajiwa kufanyika Madaba mkoani Ruvuma 22 Sept, 2018. 

Maadhimisho hayo yametanguliwa na Uelimishaji ambao unafanywa na WWF kwa kushirikiana na idara mbalimbali za serikali kwa kutumia njia tofauti ikiwemo maonesho ya shughuli za uhifadhi wa maliasili/wanyapori. 

Afisa Miradi wa WWF uwanda wa Ruvuma Richard Katondo alisema dhima hasa ya maadhimisho ni umuhimu wa kila kijiji kuwa na mpango bora wa matumizi ya ardhi ambao una ainisha maeneo ya kilimo, ufugaji, uhifadhi pamoja na mipaka ya kijiji huku ukishirikisha wananchi katika kila hatua ili kuondoa migogoro.

Tuesday, September 18, 2018

Rais wa Korea Kusini akutana na Kim Jong Un

Moon Jae-in na Kim Jong Un

Rais wa Korea Kusini Moon Jae-in amewasili leo Korea Kaskazini kwa ajili ya mkutano wake wa tatu wa kilele na ambao huenda ukawa mgumu zaidi na kiongozi Kim Jong Un ambapo anatumai kuyakwamua mazungumzo ya Marekani ya kuishinikiza Korea Kaskazini kuwachana na silaha za nyuklia. 

Ziara ya Moon pia inalenga kuziongeza nguvu juhudi zake za kuyatanua na kuboresha mahusiano kati ya Korea hizo mbili. Kim alimkaribisha Moon katika uwanja wa ndege wa Pyongyang kabla ya viongozi hao kukumbatiana na kushangiliwa na umati wa watu na kukagua guaride la heshima. 

Moon anatarajiwa kufanya mazungumzo na Kim hii leo na kesho kabla ya kurejea mjini Seoul Alhamisi. Kiongozi huyo wa Korea Kusini ameandamana na ujumbe mzito wa kibiashara wakiwemo wakuu wa makampuni makubwa.