Tuesday, May 9, 2017

NEC yapiga hatua elimu kwa njia ya Redio

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Kailima Ramadhani
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetoa wito kwa wananchi walioko kwenye halmashauri mbalimbali nchini, kuitumia vyema fursa ya utoaji wa elimu ya mpiga kura kupitia redio kwenye halmashauri zao ili kuondoa manung’uniko kwenye chaguzi.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume hiyo Kailima Ramadhani wakati akizungumzia mpango wa kutoa elimu ya mpiga kura nchi nzima ulioanza kutekelezwa jana katika mikoa kumi nchini.

Amesema kupitia mpango huo wananchi wanaosikiliza redio za kijamii kwenye halmashauri nchini, watapata fursa ya kujifunza elimu ya mpiga kura na kuelewa masuala yote muhimu yanayohusu mfumo mzima wa kupiga kura.

Utekelezaji wa mpango huo umegawanyika katika makundi matatu ambapo kundi la kwanza limeanza kutoa elimu hiyo elimu hiyo kwenye mikoa ya Kagera,Mwanza, Kilimanjaro, Morogoro, Mbeya na Dodoma.

Mikoa mingine itakayojumuishwa kwenye kundi hilo ni Ruvuma, Mara, Pwani na Mtwara ambapo elimu hiyo itatolewa hadi Mei 20 mwaka huu.

Kundi la pili linatarajiwa kutoa elimu hiyo kuanzia Mei 24 hadi Juni 7 mwaka huu katika mikoa ya Geita, Tanga, Singida, Shinyanga, Lindi, Arusha, Tabora, Kigoma, Iringa, Manyara, Rukwa, Katavi, Songwe, Njombe na Simiyu.


0 Comments:

Post a Comment