WAKAZI wa Kata ya
Mtoni Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam wameigomea halmashauri ya wilaya
hiyo kutozwa shilingi 3,000 ya taka kwa kila kaya kwa mwezi ambayo wameanza
kuitoza na badala yake watumie utaratibu wa zamani.
Hayo yamejiri huku maeneo
ya Temeke na Mwembeyanga yaliyokuwa yakitumika kumwaga taka yamebinafsishwa
hivyo taka zimeanza kupelekwa kwenye dampo kuu la Pugu.
Mwananchi akizungumza katika mgomo huo |
Wakizungumza katika
mkutano wa dharura ambao umefanyika mwishoni mwa wiki lililopita katika mtaa wa
Relini, Mtoni-Mtongani walisema halmashauri haikuwashirikisha katika mchakato
kuhusu tozo hiyo.
“Lilipokuja tuliona
kabisa serikali haitaki ushirikiano na wananchi wake kwani kumleta mkandarasi
huyo ambaye anasemekana ni kutoka Kinondoni wakati sisi ni wa Temeke tuliona
wazi lilishapangwa kunufaisha wachache,” walisema wakazi hao.
Diwani Bernard Mwakyembe akizungumza |
Pia wamesema mpaka
sasa mkandarasi aliyewekwa na halmashauri ni hatua za kunufaisha wachache huku
vijana wao wakikosa ajira kupitia mfumo walioutengeneza tangu awali wa
ukusanyaji wa taka kwa bei nafuu.
“Tulijiwekea utaratibu
mzuri wa vikundi vya vijana wa hapa Mtoni ambao kila kaya ilikuwa ikichangia
kiasi kidogo tu cha fedha, kutuletea mkandarasi wakati sisi hatujashindwa
tunaona ni kutuvuruga,” walisema wakazi hao.
Hata hivyo wengine
wamehoji magari ya halmashauri yaliyokuwa yakitumika kuzoa taka wameyapeleka
wapi huku wakitaka njia ya wakandarasi wakubwa isipewe nafasi kutokana na hali
za maisha za wakazi wa kata hiyo.
Kwa upande wake Diwani
wa kata hiyo Bernard Mwakyembe alisema maoni ya wananchi atayapeleka kwa
mkandarasi na endapo hatayakubali basi atakuwa ameshindwa kuzoa taka katika
kata hiyo na hivyo utaratibu wa zamani unaweza kutumika kuifanya kata hiyo kuwa
safi muda wote.
0 Comments:
Post a Comment