Monday, January 23, 2017

Mwenyekiti wa Kitongoji Mapinga lawamani

NA MWANDISHI WETU
Mojawapo ya nyumba eneo la Kimele, Mapinga

WAKAZI wa kitongoji cha Kimele, kijiji cha Mapinga Wilayani Bagamoyo mkoani Pwani wamemtupia lawama mwenyekiti wa kitongoji hicho kuwa amekuwa akishirikiana na baadhi ya watu wenye nia mbaya katika mgogoro wa ardhi wa eneo la Kwa Ndevu.
Aidha walisema hadi sasa kuna watu wamejitokeza kutaka kuwahamisha wakazi wa eneo hilo huku wakiwatumia Wamasai na baadhi ya Polisi kutoa vitisho.
Pia inasemekana mwenyekiti huyo ameuza viwanja viwili ndani ya eneo hilo ambalo wajanja hao walijipenyeza baada ya kuona watu wa eneo hilo wamekaa kimya.
Hawakusita kuwataja watu wanaowasumbua katika eneo hilo ambao wanasadikika kutumia mgongo wa mwenyekiti huyo kuwa ni Msakuzi Hamisi, Maganga Abdallah Maganga, Victor Lawrence na Ramadhani Abdallah Chando.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakazi hao walisema wamekuwa wakimiliki eneo hilo tangu kuzaliwa kwao na walipotaka kuanza kujenga ndipo wenye nia mbaya wakaibuka na kuwataka wahame walipogoma walichomewa vitu vyao.
Mkazi wa kitongoji hicho aliyejitambulisha kwa jina la Mama Omary aliongeza kuwa yeye ni muhanga wa mgogoro huo ambapo alimfuata mwenyekiti huyo baada ya kuvunjiwa tofali zake lakini alikimbia.
Nyumba ya mmojawapo wa wakazi wa eneo la Kimele, Kwa Ndevu

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kitongoji hicho Pazi Jaha alisema amekuwa akitekeleza wajibu wake kuwatumikia wananchi lakini kuna watu ambao hawana nia njema naye ambao wameamua kuwarubuni wakazi hao na kuwalisha maneno.
Pia Pazi aligoma kutoa ufafanuzi kuwa anawatumia polisi kufanya vurugu katika eneo hilo huku akiapa kuwa Mungu ataingilia kati suala hilo na wanaomsingizia wataumbuka.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani hakupatikana kuzungumza suala hilo kutokana na kuhusishwa na matukio kadhaa ya eneo hilo lenye mzozo toka mwaka jana.

Mkoa wa Pwani ni miongoni mwa mikoa hapa nchini yenye migogoro mingi ya ardhi kutokana na wingi wa watu jijini Dar es Salaam ambao wamekuwa wakikimbilia mkoani humo kutafuta maeneo ya kujenga.

0 Comments:

Post a Comment