Wednesday, January 25, 2017

Jela miaka 30 na vifungo vya maisha kwa kubaka na unyang'anyi

NA MWANDISHI WETU
WAKAZI watatu wa Kipunguni B, Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam wamehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela na kifungo cha maisha baada ya kukutwa na hatia ya kubaka kwa genge na unyang’anyi wa kutumia silaha.
Akisoma hukumu hiyo Hakimu Mkazi wa Mahakama Wilaya ya Ilala Juma Hassan kwa washtakiwa Jackson Simon, Kalambo Matiko na Marwa Mwita, amesema kwa pamoja waliwabaka mabinti wawili wenye miaka 14 na 15 walipovamia nyumba kwa nia ya kufanya uhalifu Julai 27, 2015 huko Kipunguni B.
Hakimu ameongeza kuwa ushahidi umethibitisha bila shaka yoyote kuwa siku ya tukio walimvamia baba wa mabinti hao ambaye alipiga kelele huku akiwaambia hana fedha yoyote na kuiba simu mbili, mabegi mawili na runinga moja.
Hata hivyo washtakiwa hao walimpiga kwa nondo baba wa mabinti hao huku wakiwa wamemfunga kamba na kumchoma kisu.
Aidha siku ya tukio washtakiwa walipomfunga baba huyo waliingia chumbani na kupekua huku wakisema haiwezekani dereva bodaboda awadanganye kiasi hicho, kuona hivyo walianza kuwabaka mabinti hao kwa zamu.

Hakimu akaongeza kuwa kutokana na washtakiwa kutokuwa na kumbukumbu ya makosa ya nyuma lakini kwa kitendo walichofanya wanastahili adhabu kali ili iwe fundisho kwa wote.

0 Comments:

Post a Comment