Ukweli na Kuheshimiana ni kiini ujenzi wa jamii zetu

Ulimwenguni kwa sasa kumejaa habari potofu na upotoshaji, ni muhimu kuhakikisha kwamba ukweli na kuheshimiana vinakuwa kiini kwa ujenzi wa jamii zetu.

Mapambano dhidi ya Habari za Uongo hayapaswi kukoma

Habari za uongo, habari za uongo zinazosambazwa kwa lengo la kumdhuru mtu au jambo fulani, huifanya jamii kuwa na sintofahamu. Zinaweza kutumika kwa madhumuni ya kiitikadi, kisiasa au hata uhalifu, kama vile ulaghai mtandaoni unaolenga kuiba data ya kibinafsi.

Utandawazi na Athari zake katika Uandishi wa Habari

Katika jamii yetu ya kisasa, ambapo habari ziko kila mahali na zinaweza kupatikana kwa kila mtu, mara nyingi ni ngumu kutofautisha kati ya vyanzo vya kuaminika na habari bandia.

Uandishi wa Habari nguzo msingi mkuu kwa ujenzi wa jamii inayojitambua

JAIZMELA blog ni miongoni mwa vyanzo vya habari, zilizochakatwa kwa kuzingatia miiko ya uandishi wa habari.

Mila na Desturi ni nguzo muhimu

Mila na desturi ni nguzo muhimu sana katika utamaduni wa jamii yoyote ile; mila ni sawa na sheria zisizoandikwa. Mila ni taratibu za maisha na mwenendo zinazofuatwa na jamii fulani katika utendaji kulingana na historia na utamaduni wao. Mila zinatambulisha maadili ya jamii husika, huelezea namna jamii inavyoendesha mambo yake.

Sunday, October 23, 2022

Watumishi Hospitali Kibong'oto wapatiwa chanjo Homa ya Ini



Hospitali Maalum ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto  imeanza kuchukua hatua za kuwalinda Watumishi wake dhidi ya magonjwa ambukizi kwa kuwapatia chanjo ya Homa ya Ini na kuwapima magonjwa mengine ambayo yanaweza kuhatarisha maisha yao wakiwa kazini.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi mtendaji wa hospitali hiyo Dkt. Leonard Subi, wakati wa uzinduzi wa upimaji wa afya kwa watumishi wa hospitali hiyo uliofanyika hospitalini hapo.

Alisema ugonjwa huo umekuwa tishio katika siku za hivi karibuni ambapo amesema pamoja na tishio hilo jambo jema ni kuwa unatibika pale unapogundulika mapema.

“Mara nyingi tumekuwa wakitoa huduma za afya kwa watu wa nje ambapo  kwa mwaka 2021 takribani watu 13,000 tuliwafikia  katika maeneo mbalimbali ya nchini kwa kutumia gari letu maalumu kwa ajili ya kuwapima, kuwachunguza afya zao zikiwemo zile zinazotolewa kwa njia ya usafiri (mobile services),”alisema Dk.. Subi.

Alisema takribani asilimia 26 ya waliopimwa walikutwa na changamoto ya shinikizo la damu, asilimia tisa kisukari ikiwa ni sehemu tu ya matokeo ya huduma ya upimaji waliofanyiwa watu kipindi hicho.

Akizungumza kuhusu zoezi hilo la upimaji wa afya kwa wafanyakazi wa hospitali hiyo, Dk. Subi amesema limelenga kuhakikisha ya kuwa watumishi hao wako salama mahala pa kazi wakati wakiendelea kutoa huduma zao kwa watu wengine.

Aidha Dk. Subi alitoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanajenga tabia ya kupima afya zao kwa kushirikisha familia zao pamoja na wengine wote wanaoishi nao ili kuepuka kupata maradhi ambayo yaambukiza.

Kuhusu ugonjwa wa COVID-19, Dk. Subi amesema pamoja na juhudi kubwa zilizofanywa na zinazoendelea kufanywa na Serikali katika kukabiliana nao bado ugonjwa huo uko hivyo ni vyema watu wakaendelea kuchukua tahadhari kama inavyoelekezwa na wataalam wa afya.

Kwa upande wake Katibu wa Hospitali Maalum ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto  Rose Shawa, alisema zoezi hilo ni la hiyari na kutoa wito kwa watumishi wote kushiriki ili kujua hali zao za kiafya na pia kujenga mazingira ya uhakika wa afya zao pale wanapoendelea kuhudumia watu wengine.

Bi. Rose alisema zoezi hili sio la kwanza kufanyika hospitalini hapo kwani  mazoezi kama hayo yameshawahi kufanyika mwaka 2015  hadi mwaka 2022 kwa watumishi kuchunguza afya na kupatiwa chanjo ya homa ya ini.

Mratibu wa shughuli za afya ya Jamii hospitali ya Kibong’oto Dk. Alexander Mbuya, alisema zoezi la upimaji na chanjo ya homa ya ini ni suala muhimu sana kwa wafanyakazi wa hospitali ya Kiobong’oto.

Wakizungumza  kwa niaba ya  watumishi wenzao wa afya katika hospitali hiyo Afisa Mazingira Asharose Muttasingwa na Afisa Muuguzi Msaidizi  kitengo cha Afya ya Jamii Eulogy  Tukay walimpongeza Mkurugenzi wa hospitali hiyo kwa kuja na wazo la watumishi wenzake  kuona umuhimu wa kupima afya zao.

Zoezi la upimaji wa afya kwa Watumishi wa Hospitali Maalum ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto  lilianzihswa mwaka wa 2015 wakati huo kukiwa na watumishi 264 ambapo  256 kati yao walipima afya zao.





Sunday, October 9, 2022

Vijana washauriwa kujitolea kuwatunza wazee

Kaimu Meneja wa Posta Tanzania Mkoa wa Kilimanjaro Veronica Magoto (kulia) akimkabidi mhudumu wa afya kituo cha kulelea wazee Njoro Bi. Maria Hatari Massawe

Vijana wameshauriwa  kujitolea na kuwatunza wazee katika maeneo yao ili kupata ushauri na busara za wazee hao kwa maendeleo yao na taifa.

Kaimu meneja wa Posta Mkoa wa Kilimanjaro Veronica Magoto ameyasema hayo jana wakati wakikabidhi misaada mbalimbali ya kijamii kwenye kituo cha kulelea wazee wasiojiweza kilichoko Njoro Manispaa ya Moshi mkoa wa Kilimanjaro, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Posta Duniani.

Magoto alisema kuwa jukumu la kuwatunza na kuwalea wazee sio la Serikali pekee bali jamii pia ina nafasi yake katika kuwatunza wazee hasa Vijana huku akisema kuwa Serikali imejitaidi sana kuweka mazingira mazuri kwa wazee kwa kuwapatia huduma za afya na kuwatunza wazee wote ambao hawana ndugu wa kuwatunza katika makambi mbalimbali ya wazee nchini.

Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa kituo cha wazee Derick Lugina,  Mhudumu wa afya Maria Hatari Massawe, amelishukuru Shirika la Posta Kilimanjaro kwa misaada hiyo ambapo amesema ni msaada mkubwa huku akiziiomba na taasisi nyingine kuwa na moyo wa kutoa kwa watu wenye uhitaji kama ambavyo wamefanya Posta.

“Kambi yetu ina wazee 17 hadi sasa wanaolelewa katika kituo hiki, hivyo Shirika la Posta Kilimanjaro mmefanya jambo kubwa sana ambalo limegusa maisha ya watu wengi ambao hawana msaada na hili linasisitizwa hadi kwenye vitabu vya dini,”alisema.

Awali akisoma risala ya maadhimisho ya siku ya Posta Duniani Afisa Masoko  wa Shirika la Posta Tanzania Mkoa wa Kilimanjaro Mwanamkuu Mussa, amesema  wametoa misaada hiyo kwenye kituo cha kulele a wazee wasiojiweza cha Njoro kilichoko Manispaa ya moshi ikiwa ni sehemu ya shughuli za kijamii kuadhimisha siku ya posta duniani.

“Misaada tuliyookabidhiwa kwa wazee wasiojiweza wanaoishi kwenye kambi ya wazee ya Njoro iliyoko Manispaa ya Moshi inayomilikiwa na Serikali kuu  ni mchele, sukari, sabuni za kufulia, kuogea na kudekia pamoja na pampers kwa ajili ya kuwasitiri wazee,”alisema Mwanamkuu.

Wakizungumza kwa niaba ya wazee wenzao wanaolelewa katika kituo hicho James Joseph na Katarina Batazari wameushukuru uongozi wa Shirika la Posta  kwa moyo wao wa kuwajali wazee na kuweza kuja kuwaona.

“Naomba utufikishie shukurani zetu kwa Meneja wa Posta mkoa wa Kilimanjaro kwa kutujali wazee hasa kwa kutatua changamoto zetu zinazotukabili, kwani tupo wazee ambao tumetelekezwa na watoto wentu…lakini kumbe tuna watoto wanaoweza kuja na kututembea na kutupatia zawadi kama hizi,” alisema mzee Joseph.



Bi. Katarina Batazari akipokea msaada wa sabuni ya maji kutoka kwa mfanyakazi wa Shirika la Posta Tanzania mkoa wa Kilimanjaro

Emmanuel Assey (kulia) akimkabidhi mhudumu wa afya kituo cha kulelea wazee Njoro Bi. Maria Hatari Massawe, mfuko wa sukari, ikiwa ni siku ya maadhimisho ya siku ya Posta Duniani.


Saturday, October 8, 2022

Chifu Marealle akabidhi madaraka, aonya matumizi ya fedha za UMT

Chifu Marealle (kushoto) akipokea zawadi ya kifimbo cha uchifu kutoka kwa Chifu Omary Mwariko 'Mhelamwana' walipokutana Marangu, Moshi mnamo mwezi Agosti 2022. (Picha: Maktaba)

Mwenyekiti wa Umoja wa Machifu Tanzania (UMT) anayemaliza muda wake Chifu Frank Marealle ameonya kuhusu matumizi ya fedha kwa mwenyekiti mpya atakayeongoza umoja huo.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi uenyekiti wa UMT aliodumu nao kwa takribani miaka 13, huko Marangu, Moshi mkoani Kilimanjaro; Chifu Marealle amesema matumizi ya fedha yamekuwa changamoto kubwa kwa taasisi nyingi nchini.

“Fedha zitumike kwa lengo lililokusudiwa la kuendeleza shughuli za umoja, msitumie fedha hovyo, fedha kidogo inayopatikana itumike kuendeleza umoja huo,” amesema Chifu Marealle

Aidha Chifu Marealle amesema suala la matumizi ya  fedha linapaswa kutiliwa mkazo ili kuepusha mgongano wa kimaslahi unaoweza kufanywa endapo hakutafnyika uchaguzi wa viongozi sahihi kuongoza UMT.

“Changamoto; wako baadhi ya wanachama walitaka kuuvuruga umoja huo lakini aliweza kusimama imara na kuweza kufanikiwa kuwaunganisha na kuwa wamoja,” ameongeza Chifu Marealle.

Chifu Marealle amesema kwa miaka yote alioongoza umoja huo amejifunza mambo mengi kutoka kwa machifu huku akisisitiza kuwa ameachia kiti hicho kwa hiari ili Kujenga tabia ya kuachiana madaraka.

“Watu tujenge umoja wa kukabidhi madaraka tusiwe ving'ang'anizi na huu utaratibu niliamua kuujenga ili pasitokee mtu yeyote kutaka kuvuruga,” amesisitiza.

Katika miaka 13 yake ya uongozi ameweza kuwaunganisha, mshikamano, amehamasisha kila chifu kuweza kusimamia maadili, elimu afya kusimamia Mila na desturi na mazingira.

Chifu Marealle akisoma hotuba yake wakati wa kukabidhi madaraka kwa hiari  mnamo Oktoba 8, 2022 





Tuesday, September 13, 2022

JAMES MMANDA: Milioni 70 zilivyofuta ndoto zake baada ya kukatwa miguu-1

Hiki ni kisa cha kweli kilichomkuta kijana James mkazi wa mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro…Nani alimsaliti kijana huyu mwenye umri wa miaka 37 afike hapo alipofikia? ANKO TUNUNU anaanza katika sehemu ya kwanza ya makala haya…

 

Tulipokuwa shuleni tulikuwa tukifundishwa methali, vitendawili, misemo na mambo kadha wa kadha. Katika kipengele cha methali miongoni mwao ilikuwa ni “Hujafa, Hujaumbika”.

Maana yake halishi ni kwamba mwili wa binadamu unaweza kubadilika kimaumbile wakati wowote angali akiwa hai.

Hivyo basi haifai kwa sababu yoyote ile kumcheka, kumdhihaki au kumkejeli mtu ambaye ana ulemavu wa kiungo mwilini mwake.

Aliyekufa ndio amekamilika, safari yake imefika mwisho. Mfuatiliji wa makala haya utakubaliana name na methali hii kwa asilimia mia moja, utapofuatilia kisa hiki cha kweli kilichompata kijana anayefahamika kwa jina la James Severin Mushi (37) mkazi wa Moshi katika mkoa wa Kilimanjaro.

Watu wengi hupewa sifa na heshima wanazostahili wakishakufa.

Wakati wa uhai wao watu huwachukulia "poa", hawautambui au kuuthamini mchango wao mpaka wakishakufa na pengo lao kuonekana.

Watu wachache sana katika historia walifanikiwa "kuumbika" angali wakiwa hai.

Kwa haraka watu wanaokuja kichwani ni kama Nelson Mandela, Michael Jackson, Steven Hawkings, Muhammad Ali na wengineo.

Wapo pia wenye bahati zaidi ambao wanapewa tuzo za heshima sana au kupendwa na mamilioni ya watu angali wakiwa hai kama Barak Obama, Pele, Beyonce na kadhalika.

Kisa hiki cha kweli cha kijana James kinaanzia katika kivuko cha waenda kwa miguu cha Karanga-Magereza mjini Moshi mnamo Aprili 2003 majira ya saa 11 jioni wakati akitoka shule.

Wakati huo alikuwa akisomea katika shule ya Ufundi ya Moshi  masuala ya ufundi bomba (Plumbing).

James anasema, “Nakumbuka ilikuwa siku ya Ijumaa mida ya saa 11 jioni katika kivuko cha waenda kwa miguu eneo la Karanga nikiwa na baiskeli basi lilinigonga.”

Muathirika huyo ambaye kwa sasa hana miguu yake ya asili, alijikuta akiwa katika Hospitali ya KCMC iliyopo mjini Moshi akiwa kwenye vitanda vya hospitali hiyo huku maumivu makali yakiendelea katika mwili wake.

James anasema machozi yalizidi kutoka baada ya kugundua kuwa maumivu makali sio pekee yamesababishwa na ajali kama ajali bali ni baada ya taa ya mwili (macho) kuangaza katika mwili wake na kujikuta hana miguu yote miwili.

“Baada ya kupelekwa hospitalini na kufika huko miguu ilikuwa haina uwezo tena wa kutibika isipokuwa kukatwa…machozi yalinitoka sikujua la kufanya,” anasimulia James.

ITAENDELEA…

 

Uhuru Kenyatta akabidhi madaraka kwa Ruto, sherehe zafana Kasarani

 

Rais wa nne wa Kenya Uhuru Kenyatta amekabidhi madaraka kwa amani kwa Rais wa Tano wa taifa hilo William Ruto katika tukio lililofanyika katika Uwanja wa Moi-Kasarani jijini Nairobi.

Rais Ruto ameapa kuitumikia Jamhuri ya Kenya kwa moyo mkunjufu na uaminifu mkubwa pasipo kuwa na upendeleo wala ushawishi ili kulijenga taifa hilo.

Sambamba na hilo Makamu wa Rais Gachagua naye amekula kiapo cha utii cha kulitumikia taifa la Kenya.

Marais 20 wa barani Afrika wamehudhuria sherehe hizo akiwamo Rais Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Mfalme Mswati III wa Eswatini.

Monday, August 29, 2022

Ngumi kufufuliwa upya Kilimanjaro

 

Chama cha mchezo wa ngumi, Kanda ya Kaskazini (KBA),umepania kuurejesha mchezo huo baada ya kipindi kirefu kupotea  kutokana na vijana wengi kutokujitokeza kushiriki pambano hilo.

Katibu wa mchezo wa Ngumi mkoa wa Arusha na Mjumbe wa Taifa wa maandalizi Ngumi Frank Francis, amesema hayo jana wakati wa uzinduzi wa mchezo wa ngumi  uliofanyika katika uwanja wa shule ya msingi Mawenzi mjini Moshi mkoani Kilimanjaro

Amesema kutokana changamoto mbalimbali za kiutendaji kutoka kwa baadhi ya viongozi wa mchezo huo, zilipelekea kupoteza ya sifa yake Kitaifa na Kimataifa na kudidimiza maendeleo yake hapa nchini.

Francia ametumia fursa hiyo ya kuwataka vijana kujitokeza kwa wingi kushiriki mchezo huo wa ngumi ambapo kwa sasa chama hicho kimeamua kurejesha heshima ya mikoa hiyo ya Kanda ya Kaskazini.

“Ngumi ni miongoni mwa michezo ambayo imeitangaza na kuipa heshima nchi yetu ya Tanzania duniani, kutokana na mabondia wake kuonyesha uwezo mkubwa na kushinda katika mapambano mbalimbali ya Kimataifa,”amesema.

Amesema mchezo wa ngumi Kanda ya Kaskazini kwa kipindi kirefu ulipotea baada ya vijana wengi kutojitokeza kushiriki pambano hilo na hivyo wameamua kufufua na kuinua mchezo wa ngumi katika Kanda ya Kaskazini ili vijana wengi waweze kushiriki mchezo huo.

Aidha ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa wadau wa mchezo wa ngumi kuwasaidia vijana walioonesha nia ya kucheza mchezo huo kupata viwanja vya kufanyia mazoezi ya ngumi sanjari na kuwapatia vifaa vya mchezo huo.

Naye Bondia mstaafu mkoa wa Kilimanjaro Emmanuel Mushi amesema wameandaa pambano hilo la ngumi kimkoa ili kukuza vipaji vilivyopo ili kuwasaidia vijana waweze kupata ajira

Awali akisoma risala kwa mgeni rasmi Katibu wa Chama cha Ngumi Mkoa wa Kilimanjaro (KBA), Malonga Kitika amesema ukosefu wa viwanja vya mchezo wa ngumi pamoja na upungufu wa vifaa vya mchezo huo, umekuwa chanzo kikubwa cha vijana wengi kurudi nyuma kushiriki mchezo wa ngumi na kutoa wito kwa taasisi za umma na binafsi kuwapatia maeneo yao ili waweze kufanyia mazoezi ya mchezo huo.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Bomang’ombe Wilaya ya Hai Evod Njau, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika ufunguzi huo, amewashauri madiwani kuhakikisha kila kata wanayoiongoza kuhamasisha vijana chini ya umri mdogo kuanza kushiriki mchezo wa ngumi ili taifa liweze kupata wachezaji bora ambao wataweza kushindana na kuweza kuleta medani za mchezo huo.

Mchezo wa ngumi ni miongoni mwa michezo inayofahamika na kupendwa na watu wengi duniani, kama ilivyo kwa michezo mingine kama vile mpira wa miguu, mchezo huu umekuwa ni chanzo cha ajira na hivyo kujipatia umaarufu mkubwa ambapo vijana wengi wanajiunga kwa lengo la kujipatia kipato.

Mchezo wa ngumi nchini Tanzania ulianza kufahamika katika miaka ya 1950 ambapo miaka ya 1970 mabondia wake walianza kufahamika katika mashindando mbalimbali ya Kimataifa.

Medali ya kwanza ya Kimataifa ililetwa na Titus Simba mwaka 1974 katika michezo ya Jumuiya ya Madola iliyofanyika nchini Uingereza na mwaka 1998 bondia mwingine Michael Yombayomba aliiletea Tanzania medali nyingine katika mashindano hayo ya Jumuiya ya Madola yaliyofanyika nchini Malaysia.








Tuesday, August 16, 2022

Uwekezaji wa bilioni 429.1 kuboresha Bandari ya Tanga waanza kuzaa matunda

 

Afisa Uhusiano wa Bandari ya Tanga Peter Milanzi akizungumza na waandishi wa habari mjini Moshi kuhusu maboresho yaliyofanyika tangu mwaka 2019 hadi sasa


Uwekezaji wa bilioni 429.1 kwa ajili ya uboreshaji wa bandari ya Tanga umeanza kuzaa matunda baada ya mkandarasi kukabidhi ujenzi wa wa gati wenye urefu wa mita 200 ambao utaruhusu bandari hiyo kongwe kuhudumia meli zisizozidi mita 200 gatini kwa wakati mmoja.

 

Hatua hiyo imekuja baada ya Mamlaka ya usimamizi wa Bandari Tanzania  (TPA) iliamua kutenga kiasi hicho cha fedha ili kutekeleza mradi mkubwa na wa kimkakati  katika bandari ya Tanga ambao unatekelezwa kwa awamu mbili. 

Nchi jirani za Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) zimeanza kutumia bandari ya Tanga kupitishia mizigo yake kutokana na maboresho ya bandari hiyo yanayoendelea ya upanuzi wa bandari hiyo, huku nchi nyingi zaidi zikitarajiwa kutumia bandari hiyo.

Rwanda imeanza kutumia bandari hiyo kupitishia malighafi inayotumika kutengenezea saruji huku nchi ya Burundi ikipitisha mzigo wa mafuta kupitia bandari hiyo. 

Mnamo mwanzoni mwa Agosti mwaka huu mkandarasi ambaye ni kampuni ya China Harbour Engineering (CHEC) Limited alikabidhi kipande cha urefu wa mita 200 hivyo kufanya uboreshaji wa bandari hiyo  kufikia asilimia 61.

 

Akizungumza na waandishi wa habari  mjini Moshi Afisa Uhusiano wa Bandari ya Tanga Peter Milanzi amesema mradi huo uliwekwa katika awamu mbili za utekelezaji ambapo awamu ya kwanza ilijikita katika uchimbaji wa kina cha maji kwenye mlango wa kuingilia meli  na shemu ya kugeuzia meli kutoka mita tatu hadi mita 13.

“Aidha licha ya uchimbaji huo, ununuzi wa mitambo ya bandari (operational equipment) kwa gharama ya shilingi 172.3 bilioni ulifanyika,” amesema.

 

Awamu ya pili ya utekelezaji wa mradi umegharimu shilingi 256.8 bilioni na utadumu kwa miezi 22 ulioanza Septemba 5, 2020 na unatarajiwa kumalizika Novemba 28, 2022.

 

“Awamu ya pili unahusisha ujenzi wa gati mbili zenye urefu wa mita 450 na kuongeza kuchimba kina cha maji kutoka mita tatu hadi 13 wakati wa maji kupwa

 

Bandari ya Tanga ni ya namna gani?

 

Bandari ya Tanga ni bandari kongwe iliyojengwa katika Pwani ya Afrika Mashariki na kuanza kufanya kazi mwaka 1891 wakati wa utawala wa Wajerumani katika ardhi ya Afrika Mashariki.

 

Bandari ya Tanga ni ya pili kwa ukubwa katika kuhudumia shehena baada ya bandari ya Dar es Salaam.  Bandari ya Tanga ina uwezo wa kuhudumia shehena ya jumla ya tani 750,000 kwa mwaka ikijumuisha mzigo mchanganyiko, shehena ya mafuta pamoja na shehena ya makasha kwa mwaka

 

Kwa mwaka wa fedha 2021/2022 imeweza kuvuka lengo kwa kuhudumia jumla ya Tabi 870,000, hata hivyo hayo ni matokeo ya awali mara baaada ya uwekezaji mkubwa wa uboreshaji wa bandari ya Tanga tangu mwaka 2019.

 

Tangu kujengwa kwake, bandari ya Tanga ilikuwa inahudumia shehena katika kina kirefu cha maji eneo la umbali wa mita 1700 kutoka gatini kwasababu ya changamoto ya kina kifupi cha maji eneo la gati ambapo kina cha maji kilikuwa mita tatu hali iliyofanya meli zishindwe kufika kwenye gati.

 

Mamlaka ya usimamizi wa Bandari Tanzania  (TPA) iliamua kutenga kiasi cha shilingi 429.1 bilioni ili kutekeleza mradi mkubwa na wa kimkakati  katika bandari ya Tanga ambao unatekelezwa kwa awamu mbili.  

 

TPA imejipanga vipi na bandari kavu ya Arumeru?

 

Kuhusu ujenzi wa Bandari kavu katika eneo la Malula wilayani Arumeru, ujumbe huo wa bandari ya Tanga umesema Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imetenga bajeti ya fedha ya kufanya upembuzi yakinifu katika mwaka huu wa fedha 2022/23.

 

Ujumbe wa kueleza uboreshaji uliofanyika katika bandari ya Tanga uliongozwa  na Afisa Uhusiano Peter Milanzi, Afisa Masoko Mkuu Rose Tandiko na Mhandisi wa Bandari hiyo,Hamis Kipalo.

 

Mikoa ya Arusha na Kilimanjaro imekuwa wanufaika na ziara hiyo ya taarifa ya maboresho ya bandari ya Tanga tangu mwaka 2019.

 

Afisa Masoko Mkuu wa Bandari ya Tanga Rose Tandiko akizungumza na waandishi wa habari kuhusu matunda yaliyoanza kupatikana baada ya uwekezaji wa shilingi 429.1 bilioni bandari hapo.

Mhandisi wa Bandari ya Tanga Hamisi Kapilo

Hecton Chuwa, mwandishi wa Daily News akiuliza swali kwa ujumbe wa TPA Bandari ya Tanga uliofika mjini Moshi kuzungumza na waandishi wa habari.


Bahati M. Nyakiraria, Mwenyekiti wa Kilimanjaro Press Club (MECKI) akizungumza na ujumbe wa Bandari ya Tanga 

William Ruto, Rais Mteule wa Kenya, amshinda Odinga kwa asilimia mbili


Rais mteule wa Kenya William Ruto ameshinda uchaguzi ambao ulikuwa na ushindani mkali katika historia ya Kenya.

William Ruto alimshinda mpinzani wake aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga ambaye alikuwa anawania urais kwa mara ya tano.

Ruto alishinda kwa asilimia 50.49 ya kura huku Odinga akiachwa kwa asilimia mbili tu.

 

Uchaguzi huo hata hivyo ulifanyika wakati ambapo taifa hilo lenye uchumi mkubwa Afrika mashariki linakabiliwa na gharama kubwa ya maisha na ukosefu wa ajira, masuala ambayo wagombea wote wakuu walikuwa wameahidi kuyaangazia. 

William Ruto, ni miongoni mwa wanasiasa wengi wakubwa nchini Kenya walioweka wazi nia zao za kuingia Ikulu ya Kenya, kupitia uchaguzi mkuu wa mwaka 2022, kurithi mikoba ya aliyekuwa 'swahiba wake', Uhuru Kenyatta.

 

Mwanasiasa huyu tajiri ambaye amekuwa na ndoto za kuwa Rais wa Kenya, amekuwa akikutana na vikwazo lukuki vya kisiasa, ikiwemo kuzuiwa kwa sababu ama kuzuiwa kwa makusudi kufanya shughuli kadhaa za kisiasa na binafsi kutokana na msukumo wa kisiasa. 

Ni miongoni mwa wanasiasa mashuhuri nchini humo, walioweka wazi nia zao za kuingia Ikulu ya Kenya, kupitia uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2022, kurithi mikoba ya 'swahiba wake', Uhuru Kenyatta.