Chama cha mchezo wa ngumi, Kanda ya Kaskazini (KBA),umepania
kuurejesha mchezo huo baada ya kipindi kirefu kupotea kutokana na
vijana wengi kutokujitokeza kushiriki pambano hilo.
Katibu wa mchezo wa Ngumi mkoa wa Arusha na Mjumbe wa Taifa wa
maandalizi Ngumi Frank Francis, amesema hayo jana wakati wa uzinduzi wa mchezo
wa ngumi uliofanyika katika uwanja wa shule ya msingi Mawenzi mjini
Moshi mkoani Kilimanjaro
Amesema kutokana changamoto mbalimbali za kiutendaji kutoka kwa
baadhi ya viongozi wa mchezo huo, zilipelekea kupoteza ya sifa yake Kitaifa na
Kimataifa na kudidimiza maendeleo yake hapa nchini.
Francia ametumia fursa hiyo ya kuwataka vijana kujitokeza kwa
wingi kushiriki mchezo huo wa ngumi ambapo kwa sasa chama hicho kimeamua
kurejesha heshima ya mikoa hiyo ya Kanda ya Kaskazini.
“Ngumi ni miongoni mwa michezo ambayo imeitangaza na kuipa
heshima nchi yetu ya Tanzania duniani, kutokana na mabondia wake kuonyesha
uwezo mkubwa na kushinda katika mapambano mbalimbali ya Kimataifa,”amesema.
Amesema mchezo wa ngumi Kanda ya Kaskazini kwa kipindi kirefu
ulipotea baada ya vijana wengi kutojitokeza kushiriki pambano hilo na hivyo
wameamua kufufua na kuinua mchezo wa ngumi katika Kanda ya Kaskazini ili vijana
wengi waweze kushiriki mchezo huo.
Aidha ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa wadau wa mchezo wa
ngumi kuwasaidia vijana walioonesha nia ya kucheza mchezo huo kupata
viwanja vya kufanyia mazoezi ya ngumi sanjari na kuwapatia vifaa vya mchezo
huo.
Naye Bondia mstaafu mkoa wa Kilimanjaro Emmanuel Mushi amesema
wameandaa pambano hilo la ngumi kimkoa ili kukuza vipaji vilivyopo ili
kuwasaidia vijana waweze kupata ajira
Awali akisoma risala kwa mgeni rasmi Katibu wa Chama cha Ngumi
Mkoa wa Kilimanjaro (KBA), Malonga Kitika amesema ukosefu wa viwanja vya mchezo
wa ngumi pamoja na upungufu wa vifaa vya mchezo huo, umekuwa chanzo kikubwa cha
vijana wengi kurudi nyuma kushiriki mchezo wa ngumi na kutoa wito kwa taasisi
za umma na binafsi kuwapatia maeneo yao ili waweze kufanyia mazoezi ya mchezo
huo.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Bomang’ombe Wilaya ya Hai Evod
Njau, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika ufunguzi huo, amewashauri madiwani
kuhakikisha kila kata wanayoiongoza kuhamasisha vijana chini ya umri mdogo
kuanza kushiriki mchezo wa ngumi ili taifa liweze kupata wachezaji bora ambao
wataweza kushindana na kuweza kuleta medani za mchezo huo.
Mchezo wa ngumi
ni miongoni mwa michezo inayofahamika na kupendwa na watu wengi duniani, kama
ilivyo kwa michezo mingine kama vile mpira wa miguu, mchezo huu umekuwa ni
chanzo cha ajira na hivyo kujipatia umaarufu mkubwa ambapo vijana wengi
wanajiunga kwa lengo la kujipatia kipato.
Mchezo wa ngumi
nchini Tanzania ulianza kufahamika katika miaka ya 1950 ambapo miaka ya 1970
mabondia wake walianza kufahamika katika mashindando mbalimbali ya Kimataifa.
Medali ya kwanza
ya Kimataifa ililetwa na Titus Simba mwaka 1974 katika michezo ya Jumuiya ya
Madola iliyofanyika nchini Uingereza na mwaka 1998 bondia mwingine Michael
Yombayomba aliiletea Tanzania medali nyingine katika mashindano hayo ya Jumuiya
ya Madola yaliyofanyika nchini Malaysia.
0 Comments:
Post a Comment