Saturday, August 13, 2022

Katibu Mkuu CCM Taifa aipongeza halmashauri ya Mwanga

Daniel Chongolo, Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa

Chama cha Mapinduzi (CCM), kimeipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga kwa kushika nafasi ya Nne na kufanikisha kuvuka lengo la ukusanyaji wa mapato na matumizi, utoaji wa mikopo ya asililimia 10%, ujibuji wa hoja za CAG, usimamizi wa matumizi ya fedha za marejesho na matumizi ya tovuti.

Katibu Mkuu wa (CCM), Taifa Daniel Chongolo, aliyasema hayo hivi karibuni  wilayani humo, wakati akizungumza na viongozi wa chama na serikali kwenye mkutano uliofanyika katika ukumbi wa ofisi za chama hicho wilayani humo.

Chongolo ameipongeza Halmashauri ya Mwanga chini ya Mkurugenzi  mtendaji Mwajuma Nasombe, kwa kuweka rekodi ambayo haijawahi kutokea na kuwa halmashauri  ya  Nne Kitaifa, baada ya tathmini ya jumla iliyofanywa na TAMISEMI ya kupimwa utendaji kazi wa Wakurugenzi kwa vigezo vitano  ikiwemo ya ukusanyaji wa mapato na matumizi, mikopo ya Wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

“Niipongeze halmashauri ya Mwanga chini ya Mkurugenzi mtendaji Mwajuma Nasombe, kwa ukusanyaji wa mapato ya ndani na matumizi ya halmashauri kwa kipindi cha robo ya nne ya Mwaka 2021/2022 na kuzielekeza fedha hizi kwenye miradi ya maendeleo,” alisema Chongolo.

 Alisema ili kufanikisha maswala ya maendeleo ni lazima viongozi wote waondoe ubinafsi na kwamba urafiki ndani ya kazi ndiyo msingi wa maendeleo.

Chongolo aliendelea kusema kuwa changamoto kubwa miongoni mwa watumishi wengi wa Serikali ni kukosa umoja miongoni mwao, huku wengine wakihangaika kuchunguza makosa ya mtu mmoja mmoja jambo ambalo alisema huchangia migogoro kazini.

 Aliongeza “Hali ya tulikotoka tunaijua, hapa tulipofikia hakuna mtu anaempongeza Mkurugenzi kwa kazi nzuri aliyoifanya  kila mmoja anakwenda kivyake, tujenge tabia ya kupongezana pindi mtu anapofanya kazi nzuri kama hii,” alisistiza Chongolo.

Aidha Chongolo alitoa wito kwa madiwani wa halmashauri hiyo kuonyesha njia kwa kupongeza juhudi zinazofanywa na mkurugenzi na timu yake na kwamba penye kasosro wasisite kukosoa.

“Ni vyema mtu akifanya vizuri mkampongeza na si hayo tu kama ikitokea amekosea jambo, msiache kumkosoa na kutoa ushauri maana hakuna aliekamilika kwa asilimia 100 wala hakuna Malaika hapa”, alisema na kuongeza kila mtu ana madhaifu yake.

 Alisisitiza,  “Rais Samia  kila mara anatoa maelekezo  kwa Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuhakikisha fedha zinazotolewa na Serikali zinahudumia wananchi kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizopo, hivyo ni majukumu yenu madiwani kusimamia watendaji wa halmashauri ili kuhakikisha agizo hilo linatekelezwa”.

Kauli ya Chongolo juu ya mafanikio ya halmashauri ya Mwanga, inakuja siku chache baada ya Waziri wa TAMISEMI Innocent Bashungwa kutangaza mafanikio yaliyopatikana baada ya halamashauri za wilaya, manispaa na majiji kuvuka malengo ya makusanyo nchini ambayo nayo yalivuka lengo. 

Kwa mujibu wa Waziri Bashungwa kipindi cha Julai mwaka jana  na Juni mwaka  huu, tathmini ya ufanisi wa utendaji wa halmashauri ni alama 80 kati ya 100, tathmini hii imezingatia ukusanyaji wa mapato na matumizi mapato ya ndani.

 

0 Comments:

Post a Comment