Sunday, October 23, 2022

Watumishi Hospitali Kibong'oto wapatiwa chanjo Homa ya Ini



Hospitali Maalum ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto  imeanza kuchukua hatua za kuwalinda Watumishi wake dhidi ya magonjwa ambukizi kwa kuwapatia chanjo ya Homa ya Ini na kuwapima magonjwa mengine ambayo yanaweza kuhatarisha maisha yao wakiwa kazini.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi mtendaji wa hospitali hiyo Dkt. Leonard Subi, wakati wa uzinduzi wa upimaji wa afya kwa watumishi wa hospitali hiyo uliofanyika hospitalini hapo.

Alisema ugonjwa huo umekuwa tishio katika siku za hivi karibuni ambapo amesema pamoja na tishio hilo jambo jema ni kuwa unatibika pale unapogundulika mapema.

“Mara nyingi tumekuwa wakitoa huduma za afya kwa watu wa nje ambapo  kwa mwaka 2021 takribani watu 13,000 tuliwafikia  katika maeneo mbalimbali ya nchini kwa kutumia gari letu maalumu kwa ajili ya kuwapima, kuwachunguza afya zao zikiwemo zile zinazotolewa kwa njia ya usafiri (mobile services),”alisema Dk.. Subi.

Alisema takribani asilimia 26 ya waliopimwa walikutwa na changamoto ya shinikizo la damu, asilimia tisa kisukari ikiwa ni sehemu tu ya matokeo ya huduma ya upimaji waliofanyiwa watu kipindi hicho.

Akizungumza kuhusu zoezi hilo la upimaji wa afya kwa wafanyakazi wa hospitali hiyo, Dk. Subi amesema limelenga kuhakikisha ya kuwa watumishi hao wako salama mahala pa kazi wakati wakiendelea kutoa huduma zao kwa watu wengine.

Aidha Dk. Subi alitoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanajenga tabia ya kupima afya zao kwa kushirikisha familia zao pamoja na wengine wote wanaoishi nao ili kuepuka kupata maradhi ambayo yaambukiza.

Kuhusu ugonjwa wa COVID-19, Dk. Subi amesema pamoja na juhudi kubwa zilizofanywa na zinazoendelea kufanywa na Serikali katika kukabiliana nao bado ugonjwa huo uko hivyo ni vyema watu wakaendelea kuchukua tahadhari kama inavyoelekezwa na wataalam wa afya.

Kwa upande wake Katibu wa Hospitali Maalum ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto  Rose Shawa, alisema zoezi hilo ni la hiyari na kutoa wito kwa watumishi wote kushiriki ili kujua hali zao za kiafya na pia kujenga mazingira ya uhakika wa afya zao pale wanapoendelea kuhudumia watu wengine.

Bi. Rose alisema zoezi hili sio la kwanza kufanyika hospitalini hapo kwani  mazoezi kama hayo yameshawahi kufanyika mwaka 2015  hadi mwaka 2022 kwa watumishi kuchunguza afya na kupatiwa chanjo ya homa ya ini.

Mratibu wa shughuli za afya ya Jamii hospitali ya Kibong’oto Dk. Alexander Mbuya, alisema zoezi la upimaji na chanjo ya homa ya ini ni suala muhimu sana kwa wafanyakazi wa hospitali ya Kiobong’oto.

Wakizungumza  kwa niaba ya  watumishi wenzao wa afya katika hospitali hiyo Afisa Mazingira Asharose Muttasingwa na Afisa Muuguzi Msaidizi  kitengo cha Afya ya Jamii Eulogy  Tukay walimpongeza Mkurugenzi wa hospitali hiyo kwa kuja na wazo la watumishi wenzake  kuona umuhimu wa kupima afya zao.

Zoezi la upimaji wa afya kwa Watumishi wa Hospitali Maalum ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto  lilianzihswa mwaka wa 2015 wakati huo kukiwa na watumishi 264 ambapo  256 kati yao walipima afya zao.





0 Comments:

Post a Comment