Sunday, October 9, 2022

Vijana washauriwa kujitolea kuwatunza wazee

Kaimu Meneja wa Posta Tanzania Mkoa wa Kilimanjaro Veronica Magoto (kulia) akimkabidi mhudumu wa afya kituo cha kulelea wazee Njoro Bi. Maria Hatari Massawe

Vijana wameshauriwa  kujitolea na kuwatunza wazee katika maeneo yao ili kupata ushauri na busara za wazee hao kwa maendeleo yao na taifa.

Kaimu meneja wa Posta Mkoa wa Kilimanjaro Veronica Magoto ameyasema hayo jana wakati wakikabidhi misaada mbalimbali ya kijamii kwenye kituo cha kulelea wazee wasiojiweza kilichoko Njoro Manispaa ya Moshi mkoa wa Kilimanjaro, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Posta Duniani.

Magoto alisema kuwa jukumu la kuwatunza na kuwalea wazee sio la Serikali pekee bali jamii pia ina nafasi yake katika kuwatunza wazee hasa Vijana huku akisema kuwa Serikali imejitaidi sana kuweka mazingira mazuri kwa wazee kwa kuwapatia huduma za afya na kuwatunza wazee wote ambao hawana ndugu wa kuwatunza katika makambi mbalimbali ya wazee nchini.

Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa kituo cha wazee Derick Lugina,  Mhudumu wa afya Maria Hatari Massawe, amelishukuru Shirika la Posta Kilimanjaro kwa misaada hiyo ambapo amesema ni msaada mkubwa huku akiziiomba na taasisi nyingine kuwa na moyo wa kutoa kwa watu wenye uhitaji kama ambavyo wamefanya Posta.

“Kambi yetu ina wazee 17 hadi sasa wanaolelewa katika kituo hiki, hivyo Shirika la Posta Kilimanjaro mmefanya jambo kubwa sana ambalo limegusa maisha ya watu wengi ambao hawana msaada na hili linasisitizwa hadi kwenye vitabu vya dini,”alisema.

Awali akisoma risala ya maadhimisho ya siku ya Posta Duniani Afisa Masoko  wa Shirika la Posta Tanzania Mkoa wa Kilimanjaro Mwanamkuu Mussa, amesema  wametoa misaada hiyo kwenye kituo cha kulele a wazee wasiojiweza cha Njoro kilichoko Manispaa ya moshi ikiwa ni sehemu ya shughuli za kijamii kuadhimisha siku ya posta duniani.

“Misaada tuliyookabidhiwa kwa wazee wasiojiweza wanaoishi kwenye kambi ya wazee ya Njoro iliyoko Manispaa ya Moshi inayomilikiwa na Serikali kuu  ni mchele, sukari, sabuni za kufulia, kuogea na kudekia pamoja na pampers kwa ajili ya kuwasitiri wazee,”alisema Mwanamkuu.

Wakizungumza kwa niaba ya wazee wenzao wanaolelewa katika kituo hicho James Joseph na Katarina Batazari wameushukuru uongozi wa Shirika la Posta  kwa moyo wao wa kuwajali wazee na kuweza kuja kuwaona.

“Naomba utufikishie shukurani zetu kwa Meneja wa Posta mkoa wa Kilimanjaro kwa kutujali wazee hasa kwa kutatua changamoto zetu zinazotukabili, kwani tupo wazee ambao tumetelekezwa na watoto wentu…lakini kumbe tuna watoto wanaoweza kuja na kututembea na kutupatia zawadi kama hizi,” alisema mzee Joseph.



Bi. Katarina Batazari akipokea msaada wa sabuni ya maji kutoka kwa mfanyakazi wa Shirika la Posta Tanzania mkoa wa Kilimanjaro

Emmanuel Assey (kulia) akimkabidhi mhudumu wa afya kituo cha kulelea wazee Njoro Bi. Maria Hatari Massawe, mfuko wa sukari, ikiwa ni siku ya maadhimisho ya siku ya Posta Duniani.


0 Comments:

Post a Comment