.........Safari ya Paul Rusesabagina hadi mikononi mwa Kagame
Mwishoni mwa mwezi Agosti mwaka huu nchini Rwanda na ulimwengu kote kuliibuka taarifa za kustaajabisha zilizoihusu serikali ya Rwanda iliyo mikononi mwa Paul Kagame baada ya kukamatwa kwa mwanaharakati Paul Rusesabagina.
Rusesabagina ambaye alianza kuwa maarufu kutokana na uokoaji wake wa mamia ya wanyarwanda wakati wa mauaji ya kimbari mnamo mwaka 1994 kupitia kazi yake ya hotel alikamatwa na vyombo vya usalama vya kimataifa na kumkabidhi mikononi mwa serikali ya Rwanda.
Idara ya Upelelezi nchini Rwanda ilisema kupitia ujumbe wa Twitter kuwa Rusesabagina kuwa yupo mikononi mwa Rwanda kwa ushirikiano wa kimataifa bila kutaja taifa ambalo lilisaidia kukamatwa kwa Rusesabagina.
Waranti ya Kimataifa ilitolewa kwa ajili ya kukamatwa kwake na polisi ya Kigali. Hata hivyo mwanaye wa kiume Tresor Rusesabagina katika taarifa yake kwa vyombo vya habari aliweka bayana kuwa kabla ya kukamatwa kwake mama na dada yake walikuwa wakizungumza na baba yao wakati akiwa safarini huko Dubai.
“Huo ndio muda wa mwisho kabisa ambao aliongea nasi,” alisema Tresor na kuongeza kuwa hajui sababu za baba yake kwenda Dubai. Rusesabagina mwenye umri wa miaka 66 hadi sasa bado yupo mikononi mwa vyombo vya usalama vya Rwanda. Anatuhumiwa kwa makosa ya ugaidi akiwa kama mwanzilishi, kiongozi na mfadhili wa vurugu.
Katika makala haya tutamwangazia Rusesabagina tangu alipoliona jua hadi kukamatwa kwake.
Rusesabagina alizaliwa Juni 15, 1954 huko Murama, Kigali akiwa ni miongoni mwa watoto tisa waliozaliwa kwa baba Mhutu na mama Mtutsi. Wazazi wake walimpeleka kusoma shule iliyokuwepo huko Gitwe ambayo ilikuwa ikiongozwa na Kanisa la Wasabato. Akiwa na umri wa miaka 13 alikuwa amejifunza vizuri Kiingereza na Kifaransa kwa ufasaha. Alimuoa mwanadada aliyefahamika kwa jina la Esther Sembeba mnamo Septemba 8, 1967 na kuwa mkewe wa kwanza. Mwishoni mwa ujana wake Rusesabagina aliona ni vema akawa mtumishi wa kanisa. Yeye na mkewe waliamua kuondoka nchini Rwanda na kwenda zao nchini Cameroon ambako Rusesabagina alisoma katika seminari.
Mnamo mwaka 1978 Rusesabagina na mkewe walirudi nchini Rwanda na kuweka makazi yao Kigali. Wakiwa hapo alikutana na rafiki yake tangu wakiwa watoto Isaac Mulihano ambaye alimwalika Rusesabagina kuomba kazi katika hoteli moja iliyofahamika kwa jina la Hôtel des Mille Collines. Akiwa hapo alipata fursa ya kuwa kiongozi na miaka michache baadaye alipelekwa Uswisi na akiwa huko alihudhuria masomo zaidi ya hoteli pia jijini Brussels, Ubelgiji.
Kutokana na umbali kama ambavyo wahenga walivyosema ‘Fimbo ya Mbali haiui Nyoka’, penzi lake na Esther liliingia ruba ambapo walitalikiana mnamo mwaka 1981. Rusesabagina akajikuta akipata majukumu makubwa zaidi ya kulea watoto wake watatu ambao ni Diane, Lys na Roger.
Kama ujuavyo maisha ni safari ndefu isiyo na mwisho, mnamo mwaka 1987 alialikwa kwenye harusi moja ambako huko alikutana na mwanadada Tatiana, ambaye alikuwa na heshima zake na muuguzi wa Kitutsi huko Ruhengeri. Rusesabagina hakujivunga kuonyesha hisia zake za upendo. Alitumia kila njia kumpata Tatiana.
Taarifa kutoka nchini Rwanda zinasema Rusesabagina aliwahi kutoa rushwa kwa wamiliki wa hoteli vilevile kwa Wizara ya Afya ili ufanyike uhamisho wa kikazi wa Tatiana kutoka Ruhengeri hadi makao makuu jijini Kigali. Miaka miwili baadaye azma yake ilifanikiwa kwani alimwoa Tatiana ambaye aliwaasili watoto na baadaye akampata mtoto waliyempa jina la Tresor.
Mnamo mwaka 1992 Rusesabagina alipandishwa cheo na kuwa Meneja Mkuu Msaidizi wa Hotel ya Diplomates ambayo ina uhusiano naile ya Mille Collines.
RUSESABAGINA NA MAUAJI YA KIMBARI 1994
Wakati vurugu za Rwanda zilipoanza, Rusesabagina alikuwa masomoni jijini Nairobi nchini Kenya pia Uswisi na baadaye Ubelgiji. Serikali ya Wahutu iliyokuwa mikononi mwa Rais Juvenal Habyarimana ilijikuta ikipata shinikizo kali kutoka kwa vikosi vya kijeshi ya Watutsi. Mapanga yaliagizwa na kuingizwa jijini Kigali na kukabidhiwa kwa Interahamwe. Watutsi walianza kupinga madai ambayo yalitangazwa na kituo cha redio cha RTLM kuwa Watutsi wanapanga kuwaangamiza wahutu wote nchini humo.
Manmo Aprili 6, 1994 Rais Habyarimana akiwa kwenye ndege akitokea Tanzania alipoteza maisha baada ya ndege yake kutunguliwa wakati ilikuwa ikikaribia kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kigali. Katika ndege hiyo kulikuwa na Rais wa Burundi Cyprien Ntaryamira, Kiongozi wa Kijeshi wa Rwanda Chief of Staff Deogratias Nsabimana na Luteni Elie Sagatwa ambaye alikuwa Mkuu wa Idara ya Usalama ya Rais.
Tangu walipouawa kutofautiana kwa mitazamo miongoni mwa serikali na wananchi kulianzisha vuurugu hizo ambapo Aprili 7, 1994 aliuawa Waziri Mkuu Agathe Uwilingiyimana na Mlinzi wa Rais; pia walinzi 10 wa amani wa Umoja wa Mataifa raia wa Ubelgiji waliuawa. Interahamwe ikaanza kuwawinda Watutsi na kuanza kuwaua na ukawa mwanzo wa mauaji ya kimbari.
Japokuwa Rusesabagina alikuwa Mhutu mkewe Tatiana alikuwa Mtutsi hivyo watoto nao walikuwa na damu za pande zote mbili. Hivyo kutokana na kutokuwa na uwezo wa kutoroka kwenye ukanda huo wa vita na familia yake, Rusesabagina aliichukua familia yake hadi hotelini alikokuwa akifanya kazi kwa ajili ya usalama. Katika hoteli hiyo mameneja wengine walitoroka kuepuka kuuawa.
Rusesabagina akawapigiwa simu wamiliki wa hoteli ambao ni Sabena walimtumia barua kuwa atasalia hapo kama kaimu meneja mkuu wa Mille Collines. Hata wakati Wahutu walipotishia kuivamia hotel hivyo Rusesabagina alisimama kidete kuhakikisha watoto na mkewe wanawakua salama.
Alifanya mipango ya kuwatorosha kwenda nchi nyingine huku yeye akibaki kuisimamia hoteli hiyo na wakimbizi baadhi.
Rusesabagina alikaririwa mnamo Machi 1, 2005 akisema, “ Kila mmoja wetu alikuwa anajua kuwa tutakufa, hilo halikuwa na swali. Swali pekee lilikuwa ni kwa namna gani. Watatukata vipande vipande? Wakiwa na mapanga yao watakukata mkono wako wa kushoto. Kisha kutoroka na kuonekana tena masaa machache baadaye na kuukata mkono wako wa kulia. Kisha mguu wa kushoto n.k Watafanya hivyo hadi unakufa.”
Hata hivyo licha ya hofu yote hiyo Rusesabagina, mkewe na watoto na baadhi ya wakimbizi walifanikiwa kuingia nchini Tanzania na shukrani za pekee ziwaendee RPF iliyokuwa mikononi mwa Paul Kagame. Baada ya kuishi miaka miwili, Rusesabagina aliomba makazi nchini Ubelgiji kasha kuondoka na familia yake jijini Brussels. Wakiwa huko walipokea vitisho hali ambayo iliwafanya waombe kuishi Texas nchini Marekani licha ya kwamba wanaendelea kuisimamia nyumba yao huko Ubelgiji.
Rusesabagina alijizolea umaarufu mkubwa na kutunukiwa tuzo mbalimbali kutokana na filamu ya Hotel Rwanda ya mwaka 2004 ambayo alicheza kama Don Cheadle. Rusesabagina alikuwa na makazi huko Brussels, Ubelgiji na San Antonio, Texas nchini Marekani. Rusesabagina ana uraia wa Ubelgiji na Marekani. Rusesabagina alianzia taasisi ya kujitolea ya Hotel Rwanda Rusesabagina ili kupambana dhidi ya ukiukwaji wa haki za binadamu. Madai yote yanayomkabili dhidi ya serikali ya Paul Kagame ameyakataa.
Makala haya yametayarishwa na Jabir Johnson kwa msaada wa mitandao, vitabu na maktaba mbalimbali na kuchapishwa Septemba 2020 katika gazeti la LaJiji nchini Tanzania.
0 Comments:
Post a Comment