Thursday, February 25, 2021

AFCON U-20: Cameroon vs Ghana jijini Nouakchott, nani atapita?

 

Kikosi cha Cameroon U-20 mwaka 2021

Michuano ya Afrika kwa timu za vijana chini ya umri wa miaka 20 inaendelea leo katika hatua ya robo fainali ambapo itashuhudiwa timu yenye mashabiki wengi ya Cameroon ikiikabili Ghana katika mzunguko wa kwanza wa hatua hiyo jijini Nouakchott. 

Mchezo huo utachezwa katika dimba la Olimpiki nchini humo ambako michuano ya mwaka huu inafanyika. Ghana inazama katika mchezo huo ikiwa na matumaini ya kusonga mbele kulitafuta taji la nne na la kwanza tangu mwaka 2009. 

Kwa upande wao Cameroon watakuwa wakicheza fainali zao za 10 wakitaka kutimiza ndoto ya kulipata taji la pili na la kwanza kwa miaka 26. Kocha wa Ghana Abdul Karim Zito amesema siku zote mechi baina yao huwa ngumu kwa kila upande. 

Kocha huyo ameongeza kuwa itakuwa mechi ya kuvutia kwani miamba yote miwili inatamani ifuzu hatua hiyo. Aidha kocha wa Cameroon Ousmanou Christophe amekaririwa akisema Ghana ni taifa kubwa katika soka, na kwamba kila mmoja anafahamu kuwa mechi hiyo itakuwa ngumu lakini wachezaji wake wamejiandaa vizuri. 

Katika mchezo huo  kiungo wa Black Satelaite Abdul Fatawu Issahaku atakuwa mhimili mkubwa kutokana na uwezo wake wa kusambaza mipira yenye macho kwa wamaliziaji. 

Cameroon wanajivunia kuwa na kiungo kama huyo Fidel Bryce Ambina na mshambuliaji wao Sunday Jang Junior aliyeonyesha mchezo mzuri dhidi ya Uganda na Mauritania.

Wachezaji wa Ghana U-20 katika michuano ya AFCON 2021 jijini Nouakchott

 

0 Comments:

Post a Comment