Friday, February 26, 2021

MAKTABA YA JAIZMELA: Roberto Carlos aitwa timu ya taifa

Februari 26, 1992 nyota wa zamani wa soka wa Brazil Roberto Calos aliitwa kwa mara ya kwanza katika kikosi cha timu ya taifa hilo. Alizaliwa Aprili Mosi, 1973 mjini Sao Paulo.

Aliitwa katika kikosi hicho akiwa na umri wa miaka 19 ambako alidumu hadi mwaka Kombe la Dunia la mwaka 2006. Akiwa na Seleccao alihudumu katika mechi 125 na kutupia mabao 11. Alikuwa katika nafasi ya ulinzi upande wa kushoto.

Jina lake kamili ni Roberto Carlos da Silva Rocha. Alianza maisha yake ya soka kama mshambuliaji lakini baadaye alionekana mzuri zaidi kama beki wa kushoto. Carlos amekuwa akitajwa kuwa katika historia ya soka, ni beki namba moja wa kushoto ambaye akili yake inawaza kushambulia zaidi.

Katika soka alipewa jina la utani la “The Bullet Man” kutokana na kuwa na miguu yenye nguvu, iliyopiga mipira ya faulo kwa ustadi mkubwa, faulo zake zilipimwa kuwa zilikuwa na uwezo wa kwenda kilometa 169 kwa saa.

Gwiji huyu alijulikana kwa stamina, kasi ya kukimbia, uwezo wa kumimina mipira yenye macho kutokea pembeni, kurusha mipira mirefu, na paja lake lilikuwa na ukubwa wa inchi 24 sawa na  sentimita 61. Mwaka 1997, licha ya kuwa beki, Carlos alifanikiwa kuwa mchezaji bora namba mbili wa dunia. Huyu ni mmoja wa mabeki bora zaidi wa kushoto waliowahi kutokea ka­tika soka.

Alipata umaarufu mkubwa akiwa na kikosi cha Real Madrid. Akiwa na timu ya  Carlos alihudumu katika michuano mikubwa na mechi za kirafiki. Alihudumu katika Kombe la Dunia mnamo mwaka 1998, 2002 na 2006; pia katika Copa America mara nne, Kombe la Shirikisho la FIFA mnamo mwaka 1997 na Michuano ya Olimpiki mwaka 1996.

Akiwa na Real Madrid, alijulikana na kupewa sifa ya kwamba akiwa upande wa kushoto anaweza kucheza mwenyewe namba tatu na 11, kwa maana ya kukaba na kushambulia. Kocha wa zamani wa Real Madrid, Vicente del Bosque, aliwahi kusema: “Ana uwezo mkubwa wa kulinda na kushambulia mwenyewe eneo lote la kushoto.”

Carlos aliichezea Los Blancos kwa misimu 11 ya mafanikio; alishinda mataji manne ya La Liga, na matatu ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Mnamo Aprili 2013, alitajwa na Gazeti la Marca la nchini Hispania, kuwa mmoja wa wachezaji 11 bora wa kigeni katika klabu ya Real Madrid kwenye historia ya miamba hiyo.

 

0 Comments:

Post a Comment