Ukweli na Kuheshimiana ni kiini ujenzi wa jamii zetu

Ulimwenguni kwa sasa kumejaa habari potofu na upotoshaji, ni muhimu kuhakikisha kwamba ukweli na kuheshimiana vinakuwa kiini kwa ujenzi wa jamii zetu.

Mapambano dhidi ya Habari za Uongo hayapaswi kukoma

Habari za uongo, habari za uongo zinazosambazwa kwa lengo la kumdhuru mtu au jambo fulani, huifanya jamii kuwa na sintofahamu. Zinaweza kutumika kwa madhumuni ya kiitikadi, kisiasa au hata uhalifu, kama vile ulaghai mtandaoni unaolenga kuiba data ya kibinafsi.

Utandawazi na Athari zake katika Uandishi wa Habari

Katika jamii yetu ya kisasa, ambapo habari ziko kila mahali na zinaweza kupatikana kwa kila mtu, mara nyingi ni ngumu kutofautisha kati ya vyanzo vya kuaminika na habari bandia.

Uandishi wa Habari nguzo msingi mkuu kwa ujenzi wa jamii inayojitambua

JAIZMELA blog ni miongoni mwa vyanzo vya habari, zilizochakatwa kwa kuzingatia miiko ya uandishi wa habari.

Mila na Desturi ni nguzo muhimu

Mila na desturi ni nguzo muhimu sana katika utamaduni wa jamii yoyote ile; mila ni sawa na sheria zisizoandikwa. Mila ni taratibu za maisha na mwenendo zinazofuatwa na jamii fulani katika utendaji kulingana na historia na utamaduni wao. Mila zinatambulisha maadili ya jamii husika, huelezea namna jamii inavyoendesha mambo yake.

Friday, March 29, 2019

Macademia: Mapinduzi ya kilimo Kilimanjaro


Mei 29, 1827 alizaliwa mtu aliyefahamika kwa jina la John Macadam katika kitongoji cha NorthBank jijini Glasgow nchini Scotland. Macadam alizaliwa katika familia ya mfanyabiashara na mmiliki wa kiwanda cha nguo na uchapishaji katika eneo la East Ayrshire huko Kilmarnock. 
Matunda ya Macademia yakiwa kwenye mti wake
Kwa mwonekane mtoto huyo kadri alivyokuwa akikua alionekana umbo lake halisi kuwa ni mrefu kwa kimo, nywele ndefu za rangi nyekundu, kidevu kikiwa kimesheheni ndevu na sauti nzito. Katika maisha yake yote alikuwa akihimiza umakini. 
Matunda za Macademia
Alisoma masomo ya kemia hadi anaondoka Glasgow alikuwa amechapisha makala mbalimbali kuhusu masuala ya Kemia. Licha ya kuzaliwa kwake kama ujuavyo kila kiumbe ni sharti kionje mauti akiwa na umri wa miaka 38 alifariki katika ardhi ya Australia.

Septemba 2, 1865 alifariki dunia akiwa amekaa miaka 10 katika ardhi hiyo. Macadam alikuwa msomi, mwanasiasa na mkemia hivyo alikuwa na ushawishi mkubwa ndani na nje ya Ulaya. 
Macadam alikuwa na rafiki yake raia wa Ujerumani Dkt. Ferdinand Mueller (1825-1896) ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Royal Botanic Gardens jijini Melbourne nchini Australia. 

Dkt. Mueller ndiye aliyegundua mmea wa Macademia ambao kwa lugha ya Kiswahili unafahamika kwa jina la Karanga Miti. Mwaka 1857 aligundua hivyo kwa heshima aliamua kuupa jina kwa heshima ya rafiki yake. 
Dkt. John Macadam kutokana na ushawishi wake kwenye taasisi yao nchini humo. Kwa ujumla wake mmea huu uligunduliwa na matajiri wa mashamba barani Ulaya ambao baadaye walikuja kusambaa duniani na kila walipoenda walifanikiwa kuupanda. 
Hivyo Kilimanjaro ni miongoni mwa maeneo ambayo yalikutwa na neema hiyo ya wahamiaji hawa kutokana walipofika walianza kumiliki maeneo makubwa kwa ajili ya ardhi na kuanza kulima kahawa ambapo waliendelea kupanda miti hiyo kama kivuli.
KWANINI MACADEMIA KILIMANJARO?
Zamani ilionekana kahawa ndio zao pekee lililo ghali ambalo linaweza kuleta faida kubwa lakini katika tafiti mbalimbali zinaonyesha makademia inaweza kubadili maisha ya wakulima zaidi ya ilivyo kahawa. 
Mimea ya Macademia katika Tudeley Estates LImited mkoani Kilimanjaro
Wawekezaji wazawa wameliona hilo na kuamua kuanza kubadilika taratibu ili kukabiliana na soko na maisha. Mwekezaji wa Tudeley Estates Limited Jensen Natai alisema, 

“Tumeanza majaribio ya kuona kama linaweza kuleta faida ikilinganishwa na kahawa lakini kwa maelezo ya awali ni zao ambalo lina protini kubwa kuliko hata ya korosho na karanga pia utunzaji wake ni mwepesi kuliko hata wa kahawa.” 
Macademia ni mmea ambao unaanza kuzaa baada ya miaka mitano kisha uvunaji wake utadumu kwa miaka hadi 30. Natai aliongeza kuwa Macademia katika majaribio yao wamepanda miti 1,000 ambayo ikishakomaa soko lake kubwa ni barani Ulaya. 
“Soko lake haliyumbi kama ilivyo kahawa pia urahisi wake ni kwamba linaweza kuchanganyikana na kahawa, linazuia upepo mkali,” alisema Natai. Pia Natai aliongeza kuwa nchi za Afrika Kusini na Zimbabwe ni zao muhimu na hutoa ajira sio chini ya 200. 
Kilimo cha Macademia kinatokana na changamoto katika sekta ya ufugaji. Mwekezaji huyo alisisitiza kuwa Macademia itavutia zaidi wenyeji baada ya kuanza kuvuna na kuuza.
Jensen Natai akizungumza na mwandishi wa habari nchini Tanzania Jabir Johnson.
 Story & Photo by: Jabir Johnson & Kija Elias

Wednesday, March 27, 2019

DAHIR JAMA YUSUF: Mfugaji wa Ngamia anayeibadilisha Jamii ya Ki-Maasai

BIBLIA inasema kwamba ngamia walikuwa kati ya wanyama wa kufugwa ambao Farao alimpa Ibrahimu. 
Mzee Dahir Jama Yusuf akiwa na mtoto wake Ahmed kwenye zizi la Ngamia Machi 20, 2019.
Wasomi wamebishana kuhusu usahihi wa kihistoria wa habari hiyo kuhusu ngamia kwa sababu wengi wao wanaamini kwamba wanyama hao walianza tu kufugwa katika sehemu nyingi karibu mwaka wa 1200 K.K., miaka mingi baada ya siku za Ibrahimu.
Kwa hiyo, inaweza kuonekana kwamba maandiko yoyote ya Biblia yaliyotaja ngamia si sahihi kwa sababu ngamia hawakutumiwa hivyo katika vipindi vinavyotajwa katika masimulizi hayo ya Biblia. 
Hata hivyo, wasomi wengine wanadai kwamba ingawa ngamia walianza kufugwa kwa wingi karibu mwisho wa miaka elfu mbili ya kwanza K.K., hilo halimaanishi kwamba ngamia hawakutumiwa kabla ya hapo. Katika kitabu cha Mwanzo 12:16 Biblia inaandika, “Farao alimtendea Abramu vema kwa sababu ya Sarai, naye akapata kondoo, ng’ombe, punda madume na majike, watumishi wa kiume na wa kike, na ngamia.” 
Katika Tarjuma ya Quran Tukufu kwa Kiswahili Surat Hajj aya ya 27 inasomeka hivi, “Na watangazie watu Hija; watakujia kwa miguu na juu ya kila ngamia aliye konda, wakija kutoka katika kila njia ya mbali.” 
Huo ni uthibitisho kuhusu Ngamia kwenye vitabu vya dini ya Kikristo na Uislamu. Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na wikipedia zinasema, Ngamia wamefugwa na binadamu tangu miaka 5,000–6,000 iliyopita. 
Leo hii mifugo hao ni takriban milioni 19 na idadi kubwa, yaani milioni 14, wako Afrika, milioni 7 pekee nchini Somalia na milioni 3.3 nchini Sudan. 
Katika miaka ya nyuma Wamasai wa Kenya na pia Tanzania wameanza kufuga ngamia baada ya kuona ya kwamba ng'ombe wao walikufa wakati wa ukame lakini ngamia waliendelea kuishi na kutoa maziwa. 
Katika makala haya tutaangazia Jamii ya Ki-Maasai katika maeneo ya Hai na Simanjiro nchini Tanzania  ilivyovutiwa na ufugaji wa ngamia.
Mzee Dahir akiwa mbele ya ngamia wake anayefahamika kwa jina la Soran.
DAHIR JAMA YUSUF NI NANI?
Huyu ni mtanzania mwenye asili ya Kisomali aliyezaliwa mwaka 1932. Dahir Jama Yusuf alizaliwa katika kijiji cha Bomang’ombe, Hai mkoani Kilimanjaro. 

Baada ya miaka mingi ya kuishi katika ardhi ya Bomang’ombe alifanikiwa kuoa mke aliyemzalia watoto 11. Mkewe alifariki miaka mitatu iliyopita akiwa na umri wa miaka 60. Katika watoto aliowazaa wa kiume wapo sita na wa kike watano. 

Kifungua mimba ni mtoto wa kike aliyemzaa mwaka 1969. Aidha mziwanda ni watoto mapacha aliowazaa mwaka 1985, wote wa kiume. Kwa sasa Mzee Dahir anaishi katika kijiji cha Mtakuja kilichopo mpakani mwa Hai na Simanjiro katika kata ya KIA wilayani Hai.

Kijiji hicho kipo umbali wa takribani kilometa 40 kutoka mji mdogo wa Bomang’ombe kwenye barabara ya Arusha-Moshi.
Mzee Dahir Jama Yusuf akikamua maziwa na Meneja wa ngamia hao Farul. 
KILICHOMSABABISHA DAHIR KUFUGA NGAMIA
Mzee huyo wa miaka 87 alikuwa mfugaji wa ng’ombe, mbuzi na kondoo kwa muda mrefu huku akiwa na kundi kubwa la wanyama hao zaidi ya 100 hali iliyomfanya ahame katika ilivyo jadi ya wafugaji kwa ajili ya kutafuta malisho. 

Lakini baadaye anasema, “ Nilijifikiria moyoni namna ninavyopata tabu ya kuwalisha, nikabadili mawazo na kuanza kufuga ngamia.” 

Pia mzee Dahir anaongeza kuwa ufugaji wa ngamia ni rafiki wa mazingira kutokana na kwamba wanyama hao hawali mimea ya kupandwa isipokuwa ya asili tu ikiwamo miti ya minyaa. 

“Hawaleti mmomonyoko wa mazingira kama unavyoona katika zizi hakuna mmomonyoko wa udongo.” Dahir anasema hiyo inatokana na kwamba ngamia hawana kwato hivyo hawachimbi ardhi kama wanyama wengine wenye kwato.
Kijana wa miaka 10 wa Jamii ya Ki-Maasai akiwa machungoni na ngamia wa Mzee Dahir Jama Yusufu kama alivyokutwa na mwandishi wa makala haya hivi karibuni alipomtembelea mfugaji huyo mtanzania mwenye asili ya Kisomali. 
ILIKUWAJE ALIPOINGIA KATIKA JAMII YA WAMAASAI?
Dahir alianza kufuga ngamia saba aliowachukua nchini Kenya kwa kiasi cha Dola za Kimarekani 3,500 wakati huo, ambayo kwa mmoja mmoja ilikuwa ni kiasi cha dola za Kimarekani 500. Pamoja na gharama nyingine ilifika dola za kimarekani 5,000. 

Aidha Mzee Dahir anasema wakati anawachukua kutoka Kenya aliwasafiri kwa mguu kwa takribani majuma mawili. Lakini sasa ana ngamia 80 na wote akiwa amewapa majina. Kinachostaajabisha kwa wanyama hao kila mmoja ikiitwa kwa jina lake inaelewa na kuitikia wito wa sauti ile. 

Miongoni mwa majina ya ngamia wake ni Shar, Soran Sikhagh, Hira na Kuze. Miaka hiyo ya mwishoni mwa karne ya 20 wakati akiingia katika kijiji cha Mtakuja alikutana na mtu mmoja anaitwa Emmanuel Simeli wa jamii ya Ki-Maasai. Simeli ambaye sasa ana umri wa miaka 54 anasema, 

“Wakati Mzee Dahir anaingia kijijini hapa, mimi nilikuwa mwenyekiti wa kitongoji; alinipa taarifa za kuhamia mahali hapa na tumeendelea kushirikiana hadi leo.”  
Dahir Jama Yusuf akisalimiana na Emmanuel Simeli ambaye alikuwa mtu wa kwanza kumpokea Dahir kijiji hapo.
USHUHUDA WA WAMAASAI KUHUSU NGAMIA
Simeli anasema, “Watu wa jamii yangu walipokuwa wanaona wanyama hao walikuwa wanakimbia, lakini baadaye tuliendelea kuelemishwa kuhusu ngamia na sasa wamewazoea na wengine wameanza kufuga.” 

Hata hivyo Simeli anasema miaka miwili ijayo ataanza kufuga mara baada ya kuona faida zake kwani hawana athari yoyote kwa mifugo mingine, na kwamba ni wanyama wapole. Farul ni kijana mwenye umri wa miaka 29 ambaye aliachana na kuchunga mifugo ya jamii ya Ki-Maasai na kuanza kuchunga ngamia wa mzee Dahir anasema, 

“Nilianza kuchunga ngamia nikiwa na miaka 10 hadi sasa nimekuwa meneja wa mifugo ya mzee huyu kwa muda wote nimejifunza namna ya kufuga ngamia.” Kijana huyo alianza kufanya kazi na Dahir wakati huo akiwa na ngamia 20. 

Farul ambaye alipewa ngamia mmoja na Mzee Dahir ambaye baadaye alimzalia ngamia wengine watano. Aidha kijana huyo mwenye watoto wawili nafurahi kufuga ngamia kuliko ng’ombe na mbuzi kutokana namna wanavyoweza kuvumilia mazingira na gharama ya kuwatunza ni ndogo huku faida zake zikiwa lukuki. 

“Imesaidia sana familia yangu kujenga, kusomesha vilevile suala la kuhamahama kumeondoka kabisa, hata Wamasai wenzangu wameanza kuelewa na kufurahia wanyama hawa,” anaongeza Farul.
Kijana Farul aliyeanza kufanya kazi kwa Mzee Dahir Jama Yusuf tangu akiwa na miaka 10 akizungumza na mwandishi wa makala haya.
MAJIRANI WANAMCHUKULIAJE DAHIR?
Jamii ya Ki-Maasai inamwona Mzee Dahir kama mtu ambaye ana mawazo chanya kuhusu maisha yao. “Dahir ni baba yetu nje ya kutusaidia kujua wanyama hawa lakini amekuwa msaada wa masuala mengi ya kijamii,” anasema Simeli. 

Kwa upande wake Dickson Jackson ambaye ni Mwalimu katika Shule ya Msingi Kibaoni iliyopo upande wa Simanjiro anasema, “Mimi ni mwenyeji wa Musoma, Mara nilikuja mwaka 2014 katika kazi ya ualimu; ilikuwa mara ya kwanza kuwaona ngamia uso kwa uso aisee nilishtuka nilianza kukimbia baada ya kuwaona lakini baadaye niliwazoea.” 

Aidha Dickson (32) anaongeza kuwa wamekuwa wakienda na wanafunzi ambao wengi ni wa jamii ya Ki-Maasai kujifunza namna ya kuwafuga wanyama hao.
Mwalimu Dickson Jackson wa Shule ya Msingi Kibaoni, Simanjiro katika mahojiano na mwandishi wa makala haya.
Watoto wa Ngamia wa Mzee Dahir Jama Yusuf wakipelekwa malishoni
Mwandishi wa makala haya Jabir Johnson katika mojawapo ya zizi la ngamia wa Mzee Dahir Jama Yusuf.
Dahir Jama Yusuf akiwa majirani zake walikwenda kumtembelea Machi 20, 2019.
Makala haya na: Jabir Johnson; 
Picha na: Kija Elias

Tuesday, March 26, 2019

Namna ‘Farming Solution App’ inavyofanya kazi

Kama ni mkulima wa zao la kahawa sasa Solidaridad imekufikia hadi mlango kupitia program yake ya ‘Farming Solution App’ ambayo utapata taarifa na kutuma taarifa zako kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu zao la kahawa lakini kwa uchache unajua Farming Solution App inavyofanya kazi? Fuatilia hapa.










Solidaridad yawafikia wakulima wa zao la Kahawa Kilimanjaro



Kasi ya mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia yamewafikiwa wakulima wa kahawa mkoani Kilimanjaro kwa kuunganishwa na matumizi ya mtandao na simu kwa upataji na utoaji wa taarifa mbalimbali kuhusu zao hilo kupitia ‘Farming Solution App’. 

Akizungumza katika semina hiyo ya siku moja mjini Moshi na watalaamu na maafisa ugani Meneja Mradi wa Solidaridad Mary Mkonyi alisema “Kama sekta tumepata changamoto kubwa za taarifa sahihi za uzalishaji, taarifa sahihi za biashara, taarifa sahihi za masoko katika ngazi ya taifa, kama sekta kiongozi tukasema tunataka sasa taarifa sahihi za mkulima, biashara ya kahawa ambapo itasaidia sisi kama wadau wajue ni kwa kiasi gani wanaweza kuwekeza nchini.”

Pia Mkonyi aliongeza kuwa baada ya mradi huo kufanya vizuri katika bara la Amerika Kusini wameona sasa ni zamu ya wakulima wa kahawa mkoani Kilimanjaro. “Bado tunashughulika na wakulima 10,000 lakini program hii itakapokuwa tayari tutachukua wakulima 1,000 ili kuona namna unavyofanya kazi na changamoto zake kisha nchi nzima,” aliongeza Mkonyi.
 
Meneja Mradi wa Solidaridad Mary Mkonyi akiwa kwenye mahojiano na Jaizmelanews


Aidha Afisa Mradi wa Solidaridad Jumanne Magese alisema, “Tumeileta program hii kwa wadau ili waweze kuiona na kutoa mapendekezo sisi kama Solidaridad tumetambua kuwa kuna changamoto katika kufikia wakulima kupitia wataalamu wa ugani hivyo tumeamua kuleta suluhisho la kilimo kupitia Farming Solution,” alisema Magese.

Aidha Magese alisema program hiyo inaweza kufanya kazi kwenye mazingira yasiyo na intaneti kisha baadaye mkulima akamalizia kwa kutumia intaneti.

“Utafiti wa mwaka 2018 wa  ‘The Mobile Economy, GSM Association’ ulionyesha kwa mwaka 2017 watu wanaotumia mtandao ni asilimia 21, aidha utafiti huo ulionyesha hadi ifikapo mwaka 2025 idadi ya watu wanaotumia mtandao litafikia asilimia 40. Pia utafiti huo ulionyesha kuwa mwaka 2017 asilimia 44 ya watu walikuwa wanatumia simu na kwamba ifikapo mwaka 2025 itafikia asilimia 52,” aliongeza Magese.

“Inamsaidia mkulima kujifanyia tathmini  yeye mwenyewe na kujipatia mpangokazi wa shamba lake  hivyo michango yao itaweza kusaidia nini iweze kuboreshwanini kiweze kuondolewa na nini kiweze kuwekwa, imegusa kila upande,” alisema afisa huyo. 
Afisa Mradi wa Solidaridad Erick Mlimba akitoa maelekezo kuhusu application kwa maafisa ugani na wataalamu wa zao la kahawa.
Afisa Maendeleo Bodi ya Kahawa Tanzania Kanda ya  Kaskazini Godfrey France alisema, “Ni program ambayo ni nzuri, vijana wengi wanakaa katika masuala ya kiteknolojia na itakuwa inawahamasisha kukipenda kilimo, Haitamlazimisha masaa yote kuwa shambani  anaweza akawa anaishi mjini na ikampa notification na akaelekeza mtu aliyepo shambani na akafanya kile alichokuwa akikifiri.”
Gazeti la Tanzanite ukurasa wa 8, Machi 27, 2019.


Story by: Kija Elias, Jabir Johnson

Monday, March 25, 2019

Watakiwa kupanda miti kwenye makaburi


Miti katika makaburi
Jamii imetakiwa kuacha tabia ya kujengea makaburi pindi wapendwa wao wanapofariki na badala yake wapande miti ya matunda kama vile maparachichi juu ya kaburi hilo.

Ushauri huo umetolewa na Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na utunzaji wa mazingira na upandaji wa miti LEPAJE, Leonard Massawe, wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Moshi mkoani humo.

Massawe ambaye pia ni mwanaharakati wa mazingira Mkoani Kilimanjaro, ameanza kampeini ya upandaji wa miti ya matunda juu ya makaburi, lengo likiwa ni kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Alisema ameanzisha kampeni hiyo ya uoteshaji wa miti ya matunda juu makaburi ikiwa ni kukabiliana na uharibifu wa mazingira nchini kwa kubadili wafu kuwa mti wa matunda.

“Ninaishauri jamii kuanza kubadilisha mitazamo yao kuwa mpendwa wao anapofariki wanaanza maandalizi ya kumjengea kaburi, wanachotakiwa kwa sasa ni kujenga  mazoea ya kuoteshe miti ya maparachichi, machungwa na mipapai,”alisema.

Alifafanua kuwa uoteshaji wa miti ya matunda kwenye makaburi itasaidia kuyatunza mazingira na kuongeza kipato na lishe kwa familia.

Hata hivvyo Massawe, alisema kwamba shirika hilo limeanza kampeini ya upandaji miti ya miparachichi juu ya kaburi la Mama yake Mkangera Koyanga aliyezaliwa mwaka 1910 na kufariki dunia 2001, ikiwa ni kuihamasisha jamii kuacha kujengea makabuli na badala yake wapande miti ya matunda juu ya makaburi hayo.

Vilevile alisema LEPAJE amewataka watanzania kujenga mazoea ya kutunza mazingira ikiwemo kila mwananchi kupanda miti mahali anapoishi ili kusaidia kuweka mazingira katika mpangilio mzuri.

Alisema endapo mwananchi atajenga tabia hiyo itawezesha kulinda uoto wa asili ambao kwa sasa umeonekana kuharibiwa kwa kiasi kikubwa.

“Kwa mwaka jana LEPAJE tulipanda miti 10,000 wilayani Mwanga, na kwamba tumefanikiwa kuendesha zoezi hilo la uhamasishaji wa upandaji miti kila mwaka kwa njia mbalimbali,”alisema Massawe.

Story by: Kija Elias