Ukweli na Kuheshimiana ni kiini ujenzi wa jamii zetu

Ulimwenguni kwa sasa kumejaa habari potofu na upotoshaji, ni muhimu kuhakikisha kwamba ukweli na kuheshimiana vinakuwa kiini kwa ujenzi wa jamii zetu.

Mapambano dhidi ya Habari za Uongo hayapaswi kukoma

Habari za uongo, habari za uongo zinazosambazwa kwa lengo la kumdhuru mtu au jambo fulani, huifanya jamii kuwa na sintofahamu. Zinaweza kutumika kwa madhumuni ya kiitikadi, kisiasa au hata uhalifu, kama vile ulaghai mtandaoni unaolenga kuiba data ya kibinafsi.

Utandawazi na Athari zake katika Uandishi wa Habari

Katika jamii yetu ya kisasa, ambapo habari ziko kila mahali na zinaweza kupatikana kwa kila mtu, mara nyingi ni ngumu kutofautisha kati ya vyanzo vya kuaminika na habari bandia.

Uandishi wa Habari nguzo msingi mkuu kwa ujenzi wa jamii inayojitambua

JAIZMELA blog ni miongoni mwa vyanzo vya habari, zilizochakatwa kwa kuzingatia miiko ya uandishi wa habari.

Mila na Desturi ni nguzo muhimu

Mila na desturi ni nguzo muhimu sana katika utamaduni wa jamii yoyote ile; mila ni sawa na sheria zisizoandikwa. Mila ni taratibu za maisha na mwenendo zinazofuatwa na jamii fulani katika utendaji kulingana na historia na utamaduni wao. Mila zinatambulisha maadili ya jamii husika, huelezea namna jamii inavyoendesha mambo yake.

Tuesday, January 31, 2017

Alfred Shauri aongoza kidato cha nne 2016

NA MWANDISHI WETU
Gazeti la Tanzania Daima Februari 1, 2016
MWANAFUNZI wa sekondari ya Feza Boys ya jijini Dar es Salaam Alfred Shauri ameongoza katika ufaulu wa mtihani wa kidato cha nne uliofanyika Novemba mwaka jana. 
Aidha Cynthia Mchechu wa shule ya sekondari ya St. Francis ya Mbeya ameongoza kwa ufaulu kwa wasichana nchini.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), Dkt. Charles Msonde amesema wanafunzi hao wanastahili pongezi kwa kufanya vizuri. 
Wanafunzi wengine waliofanya vizuri ni Erick Mamuya wa Marian Boys ya Pwani, Jigna Chavda wa St. Mary Goreti ya Kilimanjaro, Naomi Tundui wa Marian Girls ya Pwani, Victoria Chang’a wa St. Francis na Brian Johnson wa Marian Boys. 
Aidha Esther Mndeme wa St. Mary’s Mazinde Juu mkoani Tanga, Ally Koti wa ALCP Kilasara mkoani Kilimanjaro na Emmanuel Kajege wa Marian Boys wameingia katika kumi bora. 
Hata hivyo Dkt. Msonde amesema baraza lake mwanafunzi mmoja amefutiwa matokeo yake kwa kuandika matusi katika karatasi yake ya majibu hivyo kuungana na watahiniwa 126 waliofutiwa matokeo. 
Gazeti la Mtanzania Februari 1, 2016

NECTA yatangaza matokeo kidato cha nne 2016

NA MWANDISHI WETU

BARAZA la Mitihani Tanzania (NECTA) limetangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha nne na maarifa uliofanyika Novemba mwaka jana huku Dar es Salaam ikionekana kufanya vibaya kuliko mikoa mingine nchini. 
Aidha imebainika katika matokeo hayo ufaulu katika masomo ya Historia, Kiswahili, Hisabati, Fikizia, Book Keeping na Commerce umeendelea kushuka ukiwa chini ya asilimia 50. 
Akitangaza matokeo hayo leo Katibu Mtendaji wa NECTA Dkt. Charles Msonde amesema watahiniwa 277,283 sawa na asilimia 70.09 wamefaulu kati ya watahiniwa 408,372. 
Dkt. Msonde amesema kiwango cha ufaulu kimeongeza kwa asilimia 2.56 ukilinganisha na mwaka 2015 ambao ufaulu ulikuwa asilimia 67.06 
Pia shule ya Feza Boys ya Dar es Salaam imeongoza kwa ufaulu ikifuatiwa na St. Francis Girls ya Mbeya na nafasi ya tatu ikishikwa na Kaizirege Junior ya Kagera. 
Dkt. Msonde ameongeza kuwa shule sita kati ya kumi zilizofanya vibaya katika mtihani huo zinatoka Dar es Salaam ambazo ni Kitonga, Nyeburu, Mbopo, Mbondole, Somangira Day na Kidete. 
Mkoa wa Dar es Salaam haumo katika nafasi kumi za juu huku Njombe ikishika nafasi ya kwanza kwa ufaulu ikifuatiwa na Iringa na nafasi ya tatu ikishikwa na Kagera. 
Wakati huo huo NECTA imefuta matokeo ya watahiniwa 126 kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo udanganyifu. 
Dkt Msonde amesema wanafunzi 60 walikutwa na vibuti huku watahiniwa 52 wakionekana kufanana majibu.




Friday, January 27, 2017

Shahidi No. 4 ashindwa kufika kesi ya Scorpion

NA DIANA JOACHIM
Gazeti la Jamboleo Januari 27, 2017 kuhusu Salum Njwete 'Scorpion'

KESI inayomkabili Salum Njwete (34), maarufu Scorpion imeahirishwa tena katika mahakama ya wilaya ya Ilala baada ya shahidi namba nne kushindwa kufika mahakamani hapo.
Mwendesha Mashtaka Chesensi Gavyole mbele ya Hakimu Mkazi Flora Haule alidai mahakamani hapo kuwa shahidi namba nne ambaye ni daktari amepatwa na dharura itakayomweka nje kwa majuma matatu.
Hakimu aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 8 mwaka huu itakapojwa tena.
Awali imedaiwa kuwa Septemba 6 mwaka jana Scorpion mwenye miaka 34 akiwa Buguruni Shell alimchoma na kisu mlalamikaji Said Mrisho machoni, mabegani na tumboni kisha kumnyang’anya vitu vya thamani na fedha taslimu.
Hadi sasa mashahidi watatu wameshatoa ushahidi wao kuhusu tukio hilo.

Mfanyabiashara wa Madini kortini kwa kumjeruhi mkewe

NA MWANDISHI WETU



NA MWANDISHI WETU
Mfanya biashara maarufu wa madini  jijini Arusha, Venance  Moshi (30), amepandishwa kortini katika kesi inayomkabili ya kushambulia na kumjeruhi  mkewe kwa chupa usoni ,wakiwa wanasuluhishwa na baba mkwe, mgogoro wa ndoa yao.
Mwendesha Mashtaka Agnes Hyera mbele ya Hakimu Mkazi Devota Msofe alidai Machi 11 mwaka jana maeneo ya Moshono jijini hapo mshtakiwa alinyanyua bilauri na kumpiga kwenye jicho la kulia mlalamikaji Agnes Joseph.
Aidha mwendesha mashitaka alidai kitendo hicho kilimsababishia mlalamikaji atokwe na damu nyingi.
Mshtakiwa alikana mashtaka hayo ambapo Hakimu Hyera ameiahirisha hadi Februari 6 mwaka huu itakapotajwa tena.

Wednesday, January 25, 2017

Jela miaka 30 na vifungo vya maisha kwa kubaka na unyang'anyi

NA MWANDISHI WETU
WAKAZI watatu wa Kipunguni B, Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam wamehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela na kifungo cha maisha baada ya kukutwa na hatia ya kubaka kwa genge na unyang’anyi wa kutumia silaha.
Akisoma hukumu hiyo Hakimu Mkazi wa Mahakama Wilaya ya Ilala Juma Hassan kwa washtakiwa Jackson Simon, Kalambo Matiko na Marwa Mwita, amesema kwa pamoja waliwabaka mabinti wawili wenye miaka 14 na 15 walipovamia nyumba kwa nia ya kufanya uhalifu Julai 27, 2015 huko Kipunguni B.
Hakimu ameongeza kuwa ushahidi umethibitisha bila shaka yoyote kuwa siku ya tukio walimvamia baba wa mabinti hao ambaye alipiga kelele huku akiwaambia hana fedha yoyote na kuiba simu mbili, mabegi mawili na runinga moja.
Hata hivyo washtakiwa hao walimpiga kwa nondo baba wa mabinti hao huku wakiwa wamemfunga kamba na kumchoma kisu.
Aidha siku ya tukio washtakiwa walipomfunga baba huyo waliingia chumbani na kupekua huku wakisema haiwezekani dereva bodaboda awadanganye kiasi hicho, kuona hivyo walianza kuwabaka mabinti hao kwa zamu.

Hakimu akaongeza kuwa kutokana na washtakiwa kutokuwa na kumbukumbu ya makosa ya nyuma lakini kwa kitendo walichofanya wanastahili adhabu kali ili iwe fundisho kwa wote.

Umeme wakatika ghafla Dar

NA MWANDISHI WETU
TANESCO

Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO), limesema maeneo yote yaliyounganishwa kwenye mfumo wa taifa wa kusambaza umeme asubuhi ya leo yaliathirika na kukatika kwa ghafla kwa umeme kutokana na hitilafu katika mtambo wa kupooza na kusambaza umeme eneo la Ubungo jijini hapa Dar es Salaam.
Umeme ulikatika ghafla saa kumi na mbili na dakika 32 asubuhi hali ambayo iliibua sintofahamu kutokana na shughuli nyingi kuendeshwa kwa nishati hiyo.
Kituo hicho cha Ubungo ni kituo kinachotumiwa kudhibiti na kusambaza umeme mikoa yote ukiondoa mikoa ya Kagera na Kigoma inayopata umeme kutoka nchi jirani ya Uganda.
Kaimu Meneja uhusiano wa Tanesco, Leila Muhaji amesema wataalam wanaendelea kushughulikia tatizo hilo ambapo mtambo wa kilovolti 220 ulipata hitilafu
Aidha hitilafu hiyo imeathiri mitambo ya kusukuma maji katika ya DAWASCO, mitambo mitatu ya Ruvu Juu, Ruvu Chini na mtambo wa mtoni hivyo huduma ya maji kukosekana kwani mitambo hiyo hutegemea umeme kufanya kazi.

Kwa upande wake Kaimu Meneja uhusiano wa Shirika la Maji Safi na Maji Taka jijini Dar es Salaam Evalastin Liyaro amesema baadhi ya maeneo yanatarajiwa kukumbwa na uhaba wa maji ama kukosa huduma hiyo kwa muda usiojulikana.
CHANZO: BBC

Monday, January 23, 2017

Mwenyekiti wa Kitongoji Mapinga lawamani

NA MWANDISHI WETU
Mojawapo ya nyumba eneo la Kimele, Mapinga

WAKAZI wa kitongoji cha Kimele, kijiji cha Mapinga Wilayani Bagamoyo mkoani Pwani wamemtupia lawama mwenyekiti wa kitongoji hicho kuwa amekuwa akishirikiana na baadhi ya watu wenye nia mbaya katika mgogoro wa ardhi wa eneo la Kwa Ndevu.
Aidha walisema hadi sasa kuna watu wamejitokeza kutaka kuwahamisha wakazi wa eneo hilo huku wakiwatumia Wamasai na baadhi ya Polisi kutoa vitisho.
Pia inasemekana mwenyekiti huyo ameuza viwanja viwili ndani ya eneo hilo ambalo wajanja hao walijipenyeza baada ya kuona watu wa eneo hilo wamekaa kimya.
Hawakusita kuwataja watu wanaowasumbua katika eneo hilo ambao wanasadikika kutumia mgongo wa mwenyekiti huyo kuwa ni Msakuzi Hamisi, Maganga Abdallah Maganga, Victor Lawrence na Ramadhani Abdallah Chando.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakazi hao walisema wamekuwa wakimiliki eneo hilo tangu kuzaliwa kwao na walipotaka kuanza kujenga ndipo wenye nia mbaya wakaibuka na kuwataka wahame walipogoma walichomewa vitu vyao.
Mkazi wa kitongoji hicho aliyejitambulisha kwa jina la Mama Omary aliongeza kuwa yeye ni muhanga wa mgogoro huo ambapo alimfuata mwenyekiti huyo baada ya kuvunjiwa tofali zake lakini alikimbia.
Nyumba ya mmojawapo wa wakazi wa eneo la Kimele, Kwa Ndevu

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kitongoji hicho Pazi Jaha alisema amekuwa akitekeleza wajibu wake kuwatumikia wananchi lakini kuna watu ambao hawana nia njema naye ambao wameamua kuwarubuni wakazi hao na kuwalisha maneno.
Pia Pazi aligoma kutoa ufafanuzi kuwa anawatumia polisi kufanya vurugu katika eneo hilo huku akiapa kuwa Mungu ataingilia kati suala hilo na wanaomsingizia wataumbuka.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani hakupatikana kuzungumza suala hilo kutokana na kuhusishwa na matukio kadhaa ya eneo hilo lenye mzozo toka mwaka jana.

Mkoa wa Pwani ni miongoni mwa mikoa hapa nchini yenye migogoro mingi ya ardhi kutokana na wingi wa watu jijini Dar es Salaam ambao wamekuwa wakikimbilia mkoani humo kutafuta maeneo ya kujenga.

Wednesday, January 18, 2017

Watanzania na Mfuko wa Bima ya Afya

NA MWANDISHI WETU
Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dar es Salaam

WATANZANIA wametakiwa kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ili waweze kupata matibabu kwa unafuu kutokana na gharama kuwa juu hususani magonjwa ya moyo.
Akizungumza wakati wa kuiaga timu ya wataalamu kutoka Hospitali ya Apollo, Bangalore ya nchini India iliyotua katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI)  kwa ajili ya upasuaji wa moyo kwa wagonjwa sita Dk. Bashiri Nyangasa alisema wananchi wa kawaida hawawezi kuzimudu gharama za matitabu hayo.
Dk. Nyangasa alisema watalaamu hao wameisaidia serikali kuokoa kiasi cha zaidi ya shilingi Milioni 174 kwa wagonjwa hao endapo wangesafirishwa kwenda nje ya nchi kwa matibabu.
Aidha alisema upasuaji huo wa kuvuna mishipa ya damu mguuni na kuipandikiza katika mishipa ya moyo iliyokuwa imeziba kwa wanaume wanne na wanawake wawili umefanyika bila kutumia mashine ya mapafu na moyo.
JKCI
Kwa upande wake Dk. Sathyaki Nambala aliyeiongoza timu hiyo kuanzia Januari 12 hadi Januari 16 mwaka huu amesema watoto wenye umri kati ya 10 na 18 ni waathirika wakubwa wa magonjwa ya moyo na kuongeza taaasisi hiyo imejitahidi kuongeza vifaa na kwamba utalaamu waliouacha utaweza kuokoa kiasi kikubwa cha fedha siku za usoni.

Dk. Bashir Nyangasa akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kwenye Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete.
Hata hivyo ujio mwingine wa timu ya watalaamu kutoka kambi ya Madaktari Afrika inatarajia kutua nchini Januari 23 na kufanya upasuaji wa bila kufungua kifua kwa wagonjwa 15 huku Februari 4 ujio wa madaktari bingwa kutoka Saudia Arabia utawasili na kufanya upasuaji wa aina hiyo kwa wagonjwa 55 wenye miaka 12 na kuendelea.

Monday, January 16, 2017

Wagomea Shilingi 3,000 ya taka

NA MWANDISHI WETU
Wakazi wa Relini, Mtoni wakifuatilia hotuba ya diwani Mwakyembe.
WAKAZI wa Kata ya Mtoni Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam wameigomea halmashauri ya wilaya hiyo kutozwa shilingi 3,000 ya taka kwa kila kaya kwa mwezi ambayo wameanza kuitoza na badala yake watumie utaratibu wa zamani.
Hayo yamejiri huku maeneo ya Temeke na Mwembeyanga yaliyokuwa yakitumika kumwaga taka yamebinafsishwa hivyo taka zimeanza kupelekwa kwenye dampo kuu la Pugu.
Mwananchi akizungumza katika mgomo huo
Aidha wakazi hao wameitaka halmashauri hiyo kushusha tozo ya bei hadi shilingi elfu moja kutokana na hali ngumu ya maisha kwa sasa inayowanyemelea huku wakiwa hawana kazi za kudumu.
Wakizungumza katika mkutano wa dharura ambao umefanyika mwishoni mwa wiki lililopita katika mtaa wa Relini, Mtoni-Mtongani walisema halmashauri haikuwashirikisha katika mchakato kuhusu tozo hiyo.
“Lilipokuja tuliona kabisa serikali haitaki ushirikiano na wananchi wake kwani kumleta mkandarasi huyo ambaye anasemekana ni kutoka Kinondoni wakati sisi ni wa Temeke tuliona wazi lilishapangwa kunufaisha wachache,” walisema wakazi hao.
Diwani Bernard Mwakyembe akizungumza
“Mapendekezo ya wengi ni shilingi elfu moja kwa mwezi kwa kila nyumba, shilingi elfu tatu hatulipi na hakuna wa kutufanya lolote…hawakutushirikisha,” waliongeza kusema wakazi hao
Pia wamesema mpaka sasa mkandarasi aliyewekwa na halmashauri ni hatua za kunufaisha wachache huku vijana wao wakikosa ajira kupitia mfumo walioutengeneza tangu awali wa ukusanyaji wa taka kwa bei nafuu.
“Tulijiwekea utaratibu mzuri wa vikundi vya vijana wa hapa Mtoni ambao kila kaya ilikuwa ikichangia kiasi kidogo tu cha fedha, kutuletea mkandarasi wakati sisi hatujashindwa tunaona ni kutuvuruga,” walisema wakazi hao.
Hata hivyo wengine wamehoji magari ya halmashauri yaliyokuwa yakitumika kuzoa taka wameyapeleka wapi huku wakitaka njia ya wakandarasi wakubwa isipewe nafasi kutokana na hali za maisha za wakazi wa kata hiyo.
Kwa upande wake Diwani wa kata hiyo Bernard Mwakyembe alisema maoni ya wananchi atayapeleka kwa mkandarasi na endapo hatayakubali basi atakuwa ameshindwa kuzoa taka katika kata hiyo na hivyo utaratibu wa zamani unaweza kutumika kuifanya kata hiyo kuwa safi muda wote.