NA MWANDISHI WETU
Watendaji wawili wa Kata ya Saranga jijini Dar es Salaam
wamepandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni kujibu mashtaka matano
ya uhujumu uchumi.
Wakisomewa na Mwendesha Mashtaka Vera Ndeoya mbele ya
Hakimu Mkazi Isihaka Kuppa ilidaiwa Missana Ernest (41) Afisa Mtendaji wa Kata
ya Saranga na Athumani Mtono (34) Mtendaji wa Mtaa wa Kimara B walitenda makosa
hayo Oktoba 27, 2012 na Novemba 20, 2013 kinyume cha sheria za nchi.
Aidha ilidaiwa mahakamani hapo kuwa kwa pamoja washtakiwa
waliitia serikali hasara ya Sh. Milioni 8 baada ya kutumia mamlaka yao vibaya
kuchota kiasi hicho cha fedha katika akaunti ya Kamati ya Maendeleo Kata ya
Saranga kutoka Benki ya Maendeleo ya Jamii (DCB) kwa manufaa yasiyostahili.
Pia mwendesha mashtaka alidai washtakiwa walitenda makosa
hayo kwa makusudi kutokana na kuwa waliaminiwa na serikali kuwa watia saini wa
akaunti ya kata husika hivyo kujipatia kwa njia za udanganyifu fedha hizo mali
za Baraza la Manispaa ya Kinondoni.
Katika kesi hiyo washtakiwa wanaotetewa na Wakili Msomi
Benjamin Kalume walikana mashtaka yote matano ya uhujumu uchumi.
Hakimu aliwataka kutimiza masharti ya dhamana kwa kuwa na
wadhamini wawili wanaotambulika na serikali na dhamana ya Sh. Milioni moja kila
mmoja.
Kesi hiyo itatajwa tena Oktoba 12 mwaka huu.
0 Comments:
Post a Comment