NA MWANDISHI WETU
MKAZI wa Tandika Rashid Bakari amepandishwa katika mahakama ya mwanzo
ya Ilala jijini Dar es Salaam kwa kosa la kujeruhi kwa kutumia kisu.
Akisomewa mashtaka na karani wa mahakama hiyo Kassim Mtanga mbele ya
Hakimu Asha Mpunga ilidaiwa mshtakiwa alimjeruhi Dua Hamad kwa kumchoma kisu
kwenye jicho la kulia kinyume na Kifungu cha Sheria Na. 228 sura ya 16 cha
kanuni ya adhabu.
Aidha ilidaiwa kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Septemba 16 mwaka huu majira ya 2:30 asubuhi maeneo
ya Sokoni Kariakoo jijini hapa.
Mshtakiwa alikana mashtaka hayo.
Hakimu Mpunga aliweka bayana masharti ya dhamana kwa mshtakiwa ambapo alitakiwa awe na wadhamini wawili na
kutakiwa kulipa kiasi cha Sh. 800,000.
Hata hivyo mshtakiwa alishindwa kutimiza masharti na kurudishwa rumande
hadi Oktoba 4 mwaka huu shauri hilo litakapotajwa tena.
Katika shauri jingine mkazi wa Ukonga Uwanja wa Ndege jijini hapa
Thomas Laida (18), alipandishwa kizimbani kwa kumchoma Deodatus Pais kwa
kutumia bisibisi kwenye bega la kushoto.
Ilidaiwa mahakamani hapo mshtakiwa alitenda kosa hilo Septemba 15 mwaka
huu saa 7:30 mwaka huu katika mtaa wa Aggrey, Kariakoo.
Hakimu Mpunga alisema mshtakiwa ataachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza
masharti kwa kuwa na wadhamini wawili na fedha taslimu Sh. Milioni moja.
Hata hivyo mshtakiwa alishindwa masharti hayo na kurudishwa rumande
hadi shauri hilo litakapotajwa tena Oktoba 4 mwaka huu.
0 Comments:
Post a Comment