Tuesday, September 27, 2016
Jela miezi 9 kwa wizi wa simu
ILALA, DAR ES SALAAM
MAHAKAMA ya Mwanzo ya
Ilala jijini Dar es Salaam imemhukumu Norman Norvat ‘Nyoka B’(25) kwenda jela
miezi tisa kwa kosa la wizi wa simu yenye thamani ya Sh. 180,000.
Ilidaiwa mahakamani
hapo na Karani Blanka Shayo kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Agosti 3 mwaka
huu saa 9 usiku katika Mtaa wa Likoma, Kariakoo.
Aidha Shayo alidai
siku ya tukio mlalamikaji Pius Alphonce ambaye ni rafiki wa mshtakiwa akiwa na
wenzake watatu walilala uani huku simu yake aina OGM ikiwa karibu na mto.
Shayo aliongeza
shahidi namba mbili ndiye aliyemuona mshtakiwa akiingia katika nyumba ya
mlalamikaji na kutokomea na simu hiyo.
Hakimu Matrona Luanda
alisema mahakama kwa pamoja imemtia hatiani ambapo mshtakiwa amehukumiwa adhabu
kali ya miezi tisa gerezani baada ya kukiuka sheria za nchi na akimaliza alipe
thamani ya simu aliyoiba.
Kizimbani kwa kukutwa na noti bandia
NA MWANDISHI WETU
Specimen ya Sh. 10,000 ya Tanzania |
MKAZI wa Kariakoo
jijini Dar es Salaam Mashaka Salum (52) amepandishwa katika Mahakama ya Wilaya
ya Ilala kwa kosa la kukutwa na noti bandia za Sh. 10,000 kinyume na sheria za
nchi.
Mwendesha Mashtaka wa
Serikali Ashura Mnzava, mbele ya Hakimu Mkazi Wilberforce Luhwago alidai kuwa Agosti
27 mwaka huu saa 3:10 usiku mshtakiwa alikutwa na noti hizo Buguruni Corner
Bar, Buguruni Kisiwani kinyume na Kifungu cha Sheria Na. 348 sura ya 16
kilicorekebishwa mwaka 2002 cha Kanuni ya Adhabu.
Ilidaiwa mahakamani
hapo noti hizo zenye Na. BT 8486897 kama zingekuwa ni fedha halali zingekuwa na
tahamani ya Sh. 90,000.
Hakimu alisema
mshtakiwa anaweza kupata dhamana endapo atapata wadhamini wawili kila mmoja awe
na Sh. 40,000 na miongoni mwao mmojawapo awe mwajiriwa.
Kesi itatajwa tena
Okotoba 10 mwaka huu.
Sunday, September 25, 2016
Kortini kwa uhujumu uchumi
NA MWANDISHI WETU
Watendaji wawili wa Kata ya Saranga jijini Dar es Salaam
wamepandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni kujibu mashtaka matano
ya uhujumu uchumi.
Wakisomewa na Mwendesha Mashtaka Vera Ndeoya mbele ya
Hakimu Mkazi Isihaka Kuppa ilidaiwa Missana Ernest (41) Afisa Mtendaji wa Kata
ya Saranga na Athumani Mtono (34) Mtendaji wa Mtaa wa Kimara B walitenda makosa
hayo Oktoba 27, 2012 na Novemba 20, 2013 kinyume cha sheria za nchi.
Aidha ilidaiwa mahakamani hapo kuwa kwa pamoja washtakiwa
waliitia serikali hasara ya Sh. Milioni 8 baada ya kutumia mamlaka yao vibaya
kuchota kiasi hicho cha fedha katika akaunti ya Kamati ya Maendeleo Kata ya
Saranga kutoka Benki ya Maendeleo ya Jamii (DCB) kwa manufaa yasiyostahili.
Pia mwendesha mashtaka alidai washtakiwa walitenda makosa
hayo kwa makusudi kutokana na kuwa waliaminiwa na serikali kuwa watia saini wa
akaunti ya kata husika hivyo kujipatia kwa njia za udanganyifu fedha hizo mali
za Baraza la Manispaa ya Kinondoni.
Katika kesi hiyo washtakiwa wanaotetewa na Wakili Msomi
Benjamin Kalume walikana mashtaka yote matano ya uhujumu uchumi.
Hakimu aliwataka kutimiza masharti ya dhamana kwa kuwa na
wadhamini wawili wanaotambulika na serikali na dhamana ya Sh. Milioni moja kila
mmoja.
Kesi hiyo itatajwa tena Oktoba 12 mwaka huu.
Thursday, September 22, 2016
Jela miaka 4 kwa wizi wa basi la Kanisa
ILALA, DAR ES
SALAAM
MAHAKAMA ya Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam imemhukumu
kifungo cha miaka minne jela mkazi wa Ilala Panga Yusuf Mbarouk (42) kwa wizi
wa basi la kanisa la Anglikana.
Mbele ya Hakimu Mkazi Adelf Sanchore, Mwendesha Mashtaka Eric
Shija alidai mnamo Oktoba 17, 2014 mshtakiwa akiwa na wenzake watatu waliiba
gari aina ya Toyota Coaster lenye usajili wa T.379 BBB yenye thamani ya Sh.
Milioni 30 mali ya Kanisa la Anglikana, Ilala.
Awali upande wa mashtaka uliteta mashahidi saba akiwamo
Padre Thomas Ernest pamoja na
vithibitisho leseni ya gari hilo lenye Chassis Na.1HZB 400003527 na Engine Na.
1HZ0266297, Model Na. HZB40.
Aidha ilidaiwa mahakamani hapo kuwa mshtakiwa ambaye alikuwa
mwajiri wa Kampuni la S & M Security Services akiwa na Bahati Mdoe (32),
Benard Karoli ‘Master’ (47) na Shaban Msanda (34) walitenda uhalifu huo kinyume
na Kifungu cha Sheria Na. 258 na 265 sura ya 16 kilichorekebishwa mwaka 2002
cha kanuni ya adhabu.
Hakimu alisema mahakama imejiridhisha na ushahidi uliotolewa
na upande wa mashtaka kuwa mshtakiwa namba moja alitenda kosa hivyo washtakiwa
wengine waliachiwa huru.
Monday, September 19, 2016
Fundi umeme kizimbani kwa wizi
NA MWANDISHI WETU
FUNDI umeme mkazi wa Kibaha mkoani Pwani Elihood Ruhomvya (37) amepandishwa
kortini katika mahakama ya wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam baada ya
kukutwa na hatia ya kutenda makosa
mawili kinyume na kanuni za nchi.
Mwendesha Mashtaka Eric Shija mbele ya Hakimu Mkazi Wilberforce Luhwago
alidai mshtakiwa alitenda makosa mawili ya kugushi na kuiba kati ya Agosti na
Oktoba mwaka 2014 jijini hapa.
Katika kosa la kwanza ilidaiwa mahakamani hapo mshtakiwa aligushi oda
za manunuzi zipatazo 31 zenye namba tofauti kwa kutumia saini ya Ashiq Abasi Versi
kinyume na Kifungu cha Sheria Na. 333, 335(a) na 337 CAP 168 R.E 2002
Aidha ilidaiwa mahakamani hapo mshtakiwa aliiba wire wenye kipenye cha
milimita 2.5 ukiwa kwenye mabunda 117 ukiwa na thamani ya Sh. Milioni 6.3,
circuit breaker 23pcs zenye thamani ya Sh. Milioni 2.3, AVs 11pcs zenye thamani
ya Sh. Milioni 1.1 na Led Lights 2pcs zenye thamani ya Sh. 29,000 jumla ya mali
yote ikiwa ni Sh. 9,654,000 mali ya Clippers Investiment.
Hakimu Mkazi Luhwago alisema masharti ya dhamana yapo wazi kwa
mshtakiwa ambaye alitakiwa awe na wadhamini wawili mmojawapo awe mwajiriwa wa
serikali na fedha taslimu Sh. 1,500,000.
Shauri hilo litatajwa tena Septemba 22 mwaka huu.
Kortini kwa kujeruhi
NA MWANDISHI WETU
MKAZI wa Tandika Rashid Bakari amepandishwa katika mahakama ya mwanzo
ya Ilala jijini Dar es Salaam kwa kosa la kujeruhi kwa kutumia kisu.
Akisomewa mashtaka na karani wa mahakama hiyo Kassim Mtanga mbele ya
Hakimu Asha Mpunga ilidaiwa mshtakiwa alimjeruhi Dua Hamad kwa kumchoma kisu
kwenye jicho la kulia kinyume na Kifungu cha Sheria Na. 228 sura ya 16 cha
kanuni ya adhabu.
Aidha ilidaiwa kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Septemba 16 mwaka huu majira ya 2:30 asubuhi maeneo
ya Sokoni Kariakoo jijini hapa.
Mshtakiwa alikana mashtaka hayo.
Hakimu Mpunga aliweka bayana masharti ya dhamana kwa mshtakiwa ambapo alitakiwa awe na wadhamini wawili na
kutakiwa kulipa kiasi cha Sh. 800,000.
Hata hivyo mshtakiwa alishindwa kutimiza masharti na kurudishwa rumande
hadi Oktoba 4 mwaka huu shauri hilo litakapotajwa tena.
Katika shauri jingine mkazi wa Ukonga Uwanja wa Ndege jijini hapa
Thomas Laida (18), alipandishwa kizimbani kwa kumchoma Deodatus Pais kwa
kutumia bisibisi kwenye bega la kushoto.
Ilidaiwa mahakamani hapo mshtakiwa alitenda kosa hilo Septemba 15 mwaka
huu saa 7:30 mwaka huu katika mtaa wa Aggrey, Kariakoo.
Hakimu Mpunga alisema mshtakiwa ataachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza
masharti kwa kuwa na wadhamini wawili na fedha taslimu Sh. Milioni moja.
Hata hivyo mshtakiwa alishindwa masharti hayo na kurudishwa rumande
hadi shauri hilo litakapotajwa tena Oktoba 4 mwaka huu.
Kortini kwa kumpiga ngumi jicho
NA MWANDISHI WETU
MFANYABIASHARA Twaha Iddi (25) mkazi wa Machimbo Lumo jijini Dar es
Salaam amefikishwa katika mahakama ya mwanzo ya Ilala kwa kosa la kumpiga
mwenzake ngumi ya jicho.
Akisomewa mashtaka na karani wa mahakama hiyo Kassim Mtanga mbele ya
Hakimu Asha Mpunga ilidaiwa mshtakiwa alimpiga ngumi ya jicho Harubu
Ngaona Septemba 15 mwaka huu saa 3
asubuhi katika mtaa wa Aggrey, Kariakoo.
Aidha ilidaiwa mshtakiwa alikiuka Kifungu cha Sheria Na. 241 sura ya 16 cha Kanuni ya Adhabu.
Mshtakiwa alikana kosa hilo na kurudishwa rumande baada ya kushindwa
kutimiza masharti ya dhamana hadi Oktoba 4 mwaka huu shauri hilo litakapotajwa
tena.
Friday, September 16, 2016
Kortini kwa wizi wa Sh. 450,000
NA MWANDISHI WETU
MKAZI wa Kurasini Bandari jijini Dar es Salaam Michael Mlowe (46) amepandishwa katika
mahakama ya Wilaya ya Ilala kwa makosa ya wizi ukiwamo wizi wa Sh. 450,000.
Mwendesha Mashtaka Florida Wenceslaus alidai mbele ya Hakimu Mkazi Catherine
Kiyoja kuwa mnamo Agosti 26 mwaka huu maeneo ya Morogoro Road katika duka la JD
Fashions mshtakiwa alitenda kosa hilo kinyume na Kifungu cha Sheria Na. 287A
sura ya 16 R.E 2002 kama ilivyofanyiwa marekebisho na sheria Na. 3 ya mwaka
2011.
Aidha mwendesha mashtaka alidai mshtakiwa aliiba DVR Decoder ya CCTV Camera
na fedha kiasi cha Sh. 450,000 mali ya Abid Khambalia.
Hakimu alisema mshtakiwa kabla
na baada kutenda kosa alimtishia kwa silaha ili kujipatia mali hizo.
Pia aliongeza kusema mshtakiwa hakutakiwa kupata dhamana yoyote kwa
makosa aliyoyatenda hivyo kurudishwa rumande.
Shauri hilo litatajwa tena Septemba 29 mwaka huu.
Umaarufu, Usanii usiharibu tasnia ya habari
NA JABIR JOHNSON
KATIKA siku za
hivi karibuni kwenye mitandao ya Kijamii, kumekuwa na ujumbe wa Mtangazaji
mmoja mahiri anayefahamika kwa jina la Fredy Bundala akiweka bayana mawazo yake
kuhusu fani ya Utangazaji na Uandishi wa habari kwa ujumla.
Sehemu ya maoni
yake aliandika, “Umesoma utangazaji kwenye chuo kikubwa chenye sifa na umepata
shahada au stashahada yako, lakini hadi leo, unazunguka na bahasha ya kaki
mkononi yenye vyeti vyako, kutafuta kazi lakini nazo zimeota mbawa!”
Aidha Bundala
anaongeza kuwa unaweza kuwa umesota miaka kadhaa ya kuwapo kwenye fani uliyosomea lakini kinachokuduwaza zaidi
ni pale unapoona wasio na elimu ya juu kama ya kwako waking’ara katika fani
uliyosomea.
Endelea…
Mtazamo huu
umeandika katika Gazeti la Tanzania Daima ISSN 0856 9762 Toleo Na. 4305 Ijumaa
Septemba 16, 2016 Uk.7