ILALA, DAR ES SALAAM
MKAZI wa Unguja Migombani Said Rashid Said (26) amehukumiwa kwenda jela
miaka mitatu na mahakama ya Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam baada ya kukutwa na
hatia ya wizi wa gari mali ya Mohamed
Ibrahim Ismail.
Mwendesha mashtaka mahakamani hapo Florida Wenceslaus alidai mshtakiwa
alitenda kosa hilo kati ya Aprili 7 na 19 mwaka 2012 alikula njama na
udanganyifu ili kujipatia gari aina ya Suzuki Escudo lenye usajili wa T 708 BZS
lililokuwa likisafiriwa kutoka Zanzibar kwenda Kilimanjaro kupitia Dar es
Salaam.
Wenceslaus alidai gari hilo awali lilikuwa Zanzibar chini ya mmiliki wa
kwanza Maliki Said Ramadhani likiwa na usajili wa Z 326 DQ na kuuzwa kwa
Mohamed kwa Sh. Milioni 14.
Wakili wa mshitakiwa Ludovick Nickson aliiomba mahakama kumpunguzia
kifungo mshtakiwa kutokana na kukabiliwa na majukumu ya kifamilia kwani ana
mke, watoto na wazazi wanaomtegemea na kusisitiza ingefaa apewe kifungo cha
nje.
Awali Mwendesha Mashtaka aliiomba mahakama impe adhabu kali mshtakiwa
kwani alidhamiria kufanya kosa hilo na
kwamba amemtia hasara mlalamikaji kutokana
na kesi hiyo kuchukua muda mrefu.
Hakimu Mkazi Catherine Kiyoja alisema
mahakama imejiridhisha pasipo shaka kuhusu ushahidi wa watu watano uliotolewa
kuhusu mshtakiwa kwamba alikwenda
kinyume na Kifungu cha Sheria Na. 258, 265 cha Kanuni ya Adhabu CAP 16 R.E 2002.
Kiyoja aliongeza mshtakiwa anapaswa kutumikia jela miaka mitatu na gari
T 708 BZS litatakiwa kukabidhiwa kwa mlalamikaji.
0 Comments:
Post a Comment