Saturday, August 20, 2016

Abaka mwanafunzi darasa la pili Bagamoyo

BAGAMOYO, PWANI
Binti aliyebakwa na mtuhumiwa Umbuje
MWANAJESHI wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Ramadhani Kimweri ‘Umbuje’ anatuhumiwa kumbaka mtoto wa miaka tisa wa darasa la pili katika Shule ya Msingi Mtambani wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.

Uchunguzi umebaini mtuhumiwa alilitenda kosa hilo Julai 16 mwaka huu saa nane mchana nyumbani kwake mtaa wa Mingoi kata ya Mapinga wilayani hapa baada ya mtoto huyo kutumwa kuchukua ‘Ice Cream’ ndani.

Aidha baada ya mtuhumiwa kutenda kitendo hicho alimtishia mtoto huyo kwamba angemnyonga kama angetoa siri za kufanyiwa kitendo hicho cha kinyama.

Akizungumza mtoto huyo alisema, “Mimi hapa nilitoka shule baada ya kula chakula dada alinituma nichukue Ice Cream ndani ndipo alipokuja…alinichukua juu, akaniziba mdomo na kuniweka kwenye kochi akanibaka.”

Mtoto huyo aliongeza kuwa mtuhumiwa ambaye mtaani anajulikana kama Baba Mukhsin, 
“Hakuvua suruali, wala shati katoa tuu m****** wake, kisha nikavaa sketi yangu nikaondoka lakini damu kidogo ilinitoka,…nilikaa kama wiki hivi…aliyenigundua ni mwalimu wa afya na kutunza mazingira.”
Pia mtoto huyo alisisitiza licha ya mwalimu huyo kumgundua na kumtaka aseme kuhusu hali hiyo lakini hakusema akihofia vitisho vya mwanajeshi huyo na kwamba aliweka bayana baada ya askari polisi wa kike kumhoji.

Mwalimu aliyegundua hali ya binti huyo Kandida  Asenga alisema, “Tulimuona mtoto huyo akishindwa kabisa kukaa tukamuuliza akasema nina mchubuko, tukahisi ana tatizo jingine, ndipo tulipoamua kumchukua na kumpeleka katika Zahanati ya Mtambani ambako nesi akatupa majibu kwamba amebakwa…tukaenda polisi.”

Daktari wa Zahanati ya Mtambani wilayani hapa Baraka Mushi alithibitisha kumpokea mtoto huyo Julai 21 mwaka huu na kubaini kwamba alitendewa unyama huo.

Mama wa binti huyo aliyejitambulisha kwa jina la Zainabu Mtungwe (31) alisema, “Dada yake alinipigia simu, huyu mtoto nilimwacha na dada yake nilimkabidhi kwake kwani alikuwa anafanya kazi kwa mama Mukhsin kwa mazingira ya shule…kutokana na hali yangu haikuwa vizuri nikarudi Kusini (Mtwara), na nilitaka kumhamisha anifuate lakini wakanishauri nimwache hadi oktoba… nimekuja jana (Agosti 10 mwaka huu)….hayo uliyoyasikia ni hayohayo  …na upelelezi wa Polisi unaendelea.”

Mjomba wa binti huyo Hamis Abdallah Omari ‘Subiri’ mwenye miaka 55 aliyesafiri kutoka Mtwara hadi wilayani hapa alisema, “Natokea Chungutwa, Masasi mkoani Mtwara, kilichonileta ni taarifa ambayo dada yangu…kwamba binti yetu amebakwa na mwanajeshi Baba Mukhsin. Nilipofika nilienda kituo cha Polisi Mapinga lakini wakawa wananizungusha ikabidi niende kwa Mwalimu shuleni anakosoma nikapata kila kitu.”

Kwa upande wake Umbuje alisema, “Kwa sasa nafanya kazi kwenye Ofisi ya Makamu wa Rais…Jambo hilo sio la kweli hata Jeshi la Polisi liliniita jana (juzi),nami niliripoti… yaani halina ukweli wowote…hivi kweli mtu mzima na akili zake anaweza kufanya hivyo?”

Umbuje aliongeza, “Polisi wanaendelea na uchunguzi wao,…kwa kweli wananichafua…halina ukweli wowote…ndio mimi, ndio Baba Mukhsin.”

Aidha Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani Boniventure Mushongi alisema, “Sina taarifa hizo kwa sasa nipo huku Mkata nikirudi nitazifuatilia taarifa hizo kutoka kwa wenzangu…”

0 Comments:

Post a Comment