Thursday, March 7, 2024

TFF/KRFA yakabidhi mipira 1000 Halmashauri sita Kilimanjaro

 

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu akiwa na Maafisa Taaluma, Michezo na Utamaduni wa Halmashauri sita mkoani Kilimanjaro pamoja na wabunge, wakuu wa wilaya katika Hafla ya kupokea mipira 1000 kutoka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupitia Chama cha Soka mkoa wa Kilimanjaro (KRFA) mnamo Machi 7, 2024. (Picha na: JAIZMELA)

Chama Cha Soka Mkoa Wa Kilimanjaro (KRFA) kimekabidhi mipira 1000 kwa maafisa Taaluma na Maafisa Michezo na  utamaduni wa wilaya sita mkoani hapa ikiwa ni sehemu ya mradi wa kukuza vipaji vya wanafunzi wa Shule za Msingi.

Halmashauri za Mwanga, Moshi Mjini, Moshi Vijijini, Same, Hai na Rombo zimenufaika na mradi huo wa Shirikisho la Soka Tanzania ukiwa ni mwanzo wa kuinua vipaji ili kuirudisha katika ramani ya soka.

Hafla hiyo ya kukabidhi mipira hiyo ya soka kwa ajili ya wanafunzi wa shule za msingi katika wilaya hizo imefanyika katika Ofisi za Mkuu wa Mkoa na kushuhudiwa  na wabunge pia wakuu wa wilaya mkoani hapo.

Akizungumza kabla ya kukabidhi mipira hiyo Mwenyekiti wa KRFA  Isaac Munisi ametoa shukrani zake kwa Shirikisho la Soka Tanzania pia Shirikisho la Soka Dunia (FIFA) kwa kuiona Tanzania na mkoa wa Kilimanjaro miongoni mwa mikoa 14 nchini ambayo imebahatika kupata ufadhili huo.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu amesema hayo ni maandalizi mazuri kuelekea Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) ambapo Tanzania itakuwa mwenyeji wa michuano hiyo mnamo mwaka 2027.

Mbunge wa Moshi Mjini Priscus Tarimo amesema ujio wa  mipira hiyo ni kutokana na ushawishi wa Rais Samia Suluhu Hassan ambao umeleta uenyeji wa Afcon 2024 na Rais wa TFF Wallace Karia kwa kuuona mkoa wa Kilimanjaro.

Licha ya miundombinu ya viwanja na uhaba wa walimu wa michezo katika shule za msingi, mradi huo utasaidia kuvikumbusha vitengo mbalimbali katika serikali kuangazia mwendelezo wa kuinua vipaji vya soka.

Aidha Afisa Taaluma wa Manispaa ya Moshi Naomi Mhando amesema Shirikisho la Soka Tanzania limekuwa chachu ya kufanya vizuri na mwamko umekuwa mkubwa.

Mkuu wa Divisheni ya Elimu ya Msingi wilaya ya Mwanga Robert Tarimo ameongeza kuwa msingi mzuri wa mchezaji unawekwa tangu akiwa mtoto hivyo mipira hiyo itawasaidia kuendelea vipaji vilivyomo wilayani humo.




 

0 Comments:

Post a Comment