Saturday, March 2, 2024

Balozi Mwamweta: Kurudisha Masalia na Malikale za Tanzania kunahitaji watalaam kwa manufaa ya Watanzania

Kikundi cha Ngoma za Wachagga wa Kidia, Old Moshi wakitumbuiza mnamo Machi 1. 2024 katika kuukaribisha ugeni kutoka Shirikisho la Ujerumani uliofika katika Usharika wa Kidia ambako Hafla ya Uzinduzi wa Kitabu kilichoandikwa kwa msaada wa Kumbukumbu za Mmisionari Bruno Guttman aliyehudumu eneo hilo karne moja iliyopita. (Picha na: JAIZMELA)

 

Watanzania wametakiwa kuwa na uvumilivu wakati juhudi zikiendelea ili kurudisha Masalia na Mali Kale zilizochukuliwa na kupelekwa ughaibuni wakati wa tawala mbalimbali za kikoloni wakiwamo Ujerumani.

 

Akizungumza baada ya uzinduzi wa kitabu na wavuti ya “Mangi Rindi  wa Moshi: Maisha ya Shujaa na Mtawala wa Kiafrika;” hafla iliyofanyika katika Usharika wa Kidia, Old Moshi siku moja kabla ya Maadhimisho ya Miaka 122 tangu kuuawa kwa Mangi Meli Balozi wa Tanzania katika Shirikisho la Ujerumani Hassan Iddi Mwamweta alisema juhudi kubwa zinaendelea kufanywa baina ya serikali mbili ili kufikia makubaliano yenye nia njema ya kuzirudisha malikale hizo.

 

“Jambo hili limeshatolewa maelekezo na viongozi wetu wa kitaifa, ningependa niwaeleze watanzania mimi kama balozi jambo hili ni pana kuliko wakati mwingine kuliko linavyoweza kutafsirika, ni ajenda pana inayohitaji watalaamu ili kufanya majadiliano yenye tija kwa manufaa ya watanzania wote,” alisema Balozi Mwamweta. 

 

Waziri wa nchi katika Wizara ya Mambo ya Nje ya  Shirikisho la Ujerumani Katja Keul alimwelezea Gutmann kuwa alipendwa sana na Wachagga wa Old Moshi kwasababu alitambua kuwa malengo makuu ya ukoloni yalikuwa ni kuharibu mila na desturi zao hivyo akaambatana nao kuzilinda kwa gharama yoyote ile.

 

“Alitambua kuwa utawala wa kikoloni ulikuwa na nia ya kuharibu tamaduni za kichagga, mila na desturi zao. Hivyo alikuwa (Gutmann) na nia ya kuzitunza kwa namna alivyoziona kuwa ni za kipekee. Watu wa Jamii ya Kichagga walimuamini. Kwa msaada wa mkewe na watu wengine aliokua nao wakati ule aliandika mengi kwa lugha ya Kijerumani,” alisema Keul.

 

Aidha Keul alisema kuyatafsiri maandiko hayo kwa lugha za kiingereza kisha kwa Kiswahili kumetengeneza njia ya kuyafahamu kwa urahisi kuhusu utamaduni wa Kichagga ulioandikwa na Mmisionari Gutmann.

 

“Sasa kwa kuyatafsiri katika lugha ya Kiswahili kunatoa nafasi ya kuyafahamu mengi yanayowahusu Wachagga,” aliongeza Keul.

 

Hata hivyo Waziri nchi katika Wizara ya Mambo ya Nje ya  Shirikisho la Ujerumani hakusita kuwapongeza wote waliofanikisha kufikia hatua ya kutafsiri kazi za Mmisionari Gutmann ikiwamo Chuo Kikuu cha Tubingen cha Ujerumani, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Kilimanjaro Heritage Society.

 

“Shukrani za Kipekee kwa mjukuu wa Gutmann, ndugu Tilmann Prufer kwa kusaidia mradi huu kufanikiwa, ninaamini utakuwa na msaada mkubwa katika siku zijazo na kuzishikamanisha kikamilifu Tanzania na Ujerumani. Miradi kama hii inasaidia kuhamasisha kuhusu upatikanaji wa historia zetu na miradi mingi zaidi itaendelea kuja,” alisisitiza Katja Keul.

 

Katja Keul alikuwa mgeni rasmi katika Uzinduzi wa Kitabu cha “Mangi Rindi  wa Moshi: Maisha ya Shujaa na Mtawala wa Kiafrika;” kiliandikwa kutokana na nyaraka mbalimbali za Mmisionari Kijerumani  Bruno Gutmann aliyeishi Kidia, Old Moshi.

 

Naibu waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Renasi Mnata alisema kutafsiri kumbukumbu hizo kwa lugha adhimu ya Kiswahili maana yake ni kuwa utajiri umerudi nyumbani.

 

“Kuandika historia na utamaduni kwa Kiswahili maana yake utajiri huo umerudi nyumbani, sasa tujivunie utajiri huo na tusome vitabu hivyo ili kuelewa yale ambayo yawezekana katika umri wetu hatukupata kuyaona,tujivunie utajiri huo na tuendelee kufanya kazi na serikali yetu,” alisema Dkt. Mnata.

 

Akizungumza katika uzinduzi wa kitabu hicho Mjukuu wa Gutmann, Tilman Prufer alisema walipofikia hata Gutmann mwenyewe huko aliko atakuwa anajisikia furaha

 

“Ni heshima kubwa kwamba kufika hapa, na hata Gutmann huko mbinguni atakuwa anajisikia furaha kwa tulipofikia,” alisema Prufer.

 

Kwa upande wake Mhadhiri wa Akiolojia na Turathi Dkt. Silayo wa Idara ya Akiolojia ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alisema maandiko ya Gutmann yaliyoandikwa kwa kijerumani kuhusu Wachagga yamefungua njia yakujua mafundisho mbalimbali ya tamaduni za jamii hiyo iliyopo Kaskazini mwaka Tanzania

 

“ Umefika wakati utajiri huu urudi wa Wachagga ili uweze kutufundisha kizazi cha sasa hivi kutueleza wazee wetu walikuwa wanafanya nini na wanaishi vipi,” aliongeza Dkt. Silayo.

 

Mchungaji Sayuni Shao, wa Usharika wa Kidia alisema Gutmann alifanya kazi ya ziada kuwaunganisha wachagga wa Old Moshi kiasi ambacho kimesaidia hata neno la Mungu kupata tafsiri ya lugha za asili ikiwamo Kichagga.

 

Miongoni nyaraka za Gutmann za mwanzoni mwa msimu wa machipuko mnamo mwaka 1928 anaeleza kuhusu wavamizi dhalimu  na wenye tamaa kutoka barani Ulaya walioingia Afrika, hususani katika robo ya mwisho ya karne ya 19 kuwa hawakujali sana Utamaduni wa Watu wa Afrika na kwamba kwao watu weusi walikuwa washenzi ambao ingeliwafaa kufuata taratibu na njia za maisha za mabawana wao wapya kwa haki na desturi.





 

0 Comments:

Post a Comment