Marehemu Jonathan S. Makanyaga (6) mwanafunzi wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Mrupanga, UruKusini wilayani Moshi enzi za uhai wake.
Sintofahamu imeendelea kutanda kuhusu maziko ya mwanafunzi wa darasa la kwanza aliyefariki dunia mnamo Machi 11, 2024 akipatiwa matibabu katika hospitali ya KCMC mjini Moshi wakati akipatiwa matibabu kutokana na kipigo alichokipata mnamo Februari 28, 2024.
Marehemu anayefahamika kwa jina la Jonathan Stefano Makanyaga amefariki dunia akiwa na umri wa miaka sita mwanafunzi wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Mrupanga, Uru Kusini wilayani Moshi kwa kile kinachodaiwa kipigo kutokana na kuchelewa shuleni hapo na walimu waliokuwapo mafunzoni.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro (SACP) Simon Maigwa ameiambia EATV kuwa uchunguzi kuhusu mwili wa marehemu ulishafanyika na familia ilishakabidhiwa kwa ajili ya maziko.
Mkanganyiko umejitokeza mnamo Machi 16, 2024 wakati ambapo marehemu alitakiwa kuzikwa hadi saa 11:00 jioni hakukuwa na dalili zozote za kufanyika maziko huku kaburi likiwa tayari limechimbwa na kukamilika majira ya saa nane mchana.
Akizungumza na EATV Mzee Jerome Urio amesema kwa taratibu za uchagani kama Marehemu amefia nyumbani basi maziko huweza kufanyika muda wowote ule huku akifariki dunia mbali na hapo basi kaburi likishachimbwa ni lazima kuzikwa siku hiyo hiyo kuanzia saa 7 za mchana na kabla ya saa 11 jioni.
Mpaka sasa haijulikani marehemu huyo atazikwa lini huku sintofahamu ikitanda katika kitongoji cha Mrukutini huko Uru Kusini umbali wa kilometa moja mpaka ilipo shule aliyokuwa akisoma marehemu Jonathan.
0 Comments:
Post a Comment