Ukweli na Kuheshimiana ni kiini ujenzi wa jamii zetu

Ulimwenguni kwa sasa kumejaa habari potofu na upotoshaji, ni muhimu kuhakikisha kwamba ukweli na kuheshimiana vinakuwa kiini kwa ujenzi wa jamii zetu.

Mapambano dhidi ya Habari za Uongo hayapaswi kukoma

Habari za uongo, habari za uongo zinazosambazwa kwa lengo la kumdhuru mtu au jambo fulani, huifanya jamii kuwa na sintofahamu. Zinaweza kutumika kwa madhumuni ya kiitikadi, kisiasa au hata uhalifu, kama vile ulaghai mtandaoni unaolenga kuiba data ya kibinafsi.

Utandawazi na Athari zake katika Uandishi wa Habari

Katika jamii yetu ya kisasa, ambapo habari ziko kila mahali na zinaweza kupatikana kwa kila mtu, mara nyingi ni ngumu kutofautisha kati ya vyanzo vya kuaminika na habari bandia.

Uandishi wa Habari nguzo msingi mkuu kwa ujenzi wa jamii inayojitambua

JAIZMELA blog ni miongoni mwa vyanzo vya habari, zilizochakatwa kwa kuzingatia miiko ya uandishi wa habari.

Mila na Desturi ni nguzo muhimu

Mila na desturi ni nguzo muhimu sana katika utamaduni wa jamii yoyote ile; mila ni sawa na sheria zisizoandikwa. Mila ni taratibu za maisha na mwenendo zinazofuatwa na jamii fulani katika utendaji kulingana na historia na utamaduni wao. Mila zinatambulisha maadili ya jamii husika, huelezea namna jamii inavyoendesha mambo yake.

Friday, January 26, 2024

Katja Keul kutoka Ujerumani kuhudhuria maadhimisho ya miaka 122 ya Mangi Meli Makindara

Waziri wa Mambo ya Nje ya Nchi na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kutoka nchini Ujerumani Katja Keul, kutoka nchini Ujerumani, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya kumbukizi ya miaka 122 ya shujaa wa Wachagga Mangi Meli Makindara, aliyeuawa kwa kunyongwa na Wakoloni wa Kijerumani Machi 2 mwaka 1900 na kisha fuvu la kichwa chake kuchululiwa na Wajurumani hao.

Mratibu wa Taasisi ya Utalii ya Old Moshi Cultural Tourism Gabriel Mzei Orio, ameyasema hayo jana, wakati akizungumza na Tanzania Leo Mjini Moshi Mkoani Kilimanjaro kuhusiana na maadhimisho hayo, ambayo yatafanyika  MAchi 2, mwaka huu katika eneo la Kolila Wilaya ya Moshi mkoani humo.


“Machi 2, ya kila mwaka huwa ni kumbukizi ya kuwakumbuka viongozi wa kimila na wasaidizi wao waliouawa kwa kunyongwa akiwemo, shujaa wa jamii ya Wachagga Mangi Meli Makindara, aliyeuawa kwa kunyongwa na kukatwa kichwa chake  na wakoloni wa Kijerumani,”amesema Orio.


Amesema katika kumbukizi hiyo pia Waziri wa Maliasili na Utalii Angellah Kairuki anatarajiwa kuungana katika tukio hilo, machifu kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini, ndugu, jamaa pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali kutoka Ujerumani na Tanzania watashiriki katika kumbukizi hiyo.


Aidha amesema kamati ya maandalizi kwa ajili ya kushughulikia tukio hilo inaendelea kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Ofisi ya mkuu wa Wilaya ya Moshi, Mkuu wa Mkoa, Umoja wa Machifu wa Mkoa wa Kilimanjaro pamoja na familia za ndugu wa viongozi waliouawa.


“Katika tukio hili litatanguliwa na dua itakayofanyika katika mnara kilipolazwa kiwiliwili cha Mangi Meli Makindara na kufuatiwa na uwekaji wa mashada ya maua pamoja na salamu fupi kutoka kwa viongozi mbalimbali na wageni waalikwa.”


Kwa upande wake Katibu wa Umoja wa Machifu mkoa wa Kilimanjaro Joseph Mselle, amesema maadhimisho  ya kumbukizi hizo ni sehemu ya kuwaenzi viongozi na mashujaa 17 ambao walikuwa viongozi wa mila na desturi pamoja na wasaidizi wao waliuawa  kikatili wakati wakipambana kuwatetea wananchi wao.


“Mkoa wa Kilimanjaro tuna kila sababu ya kushiriki katika kumbukizi hizi kwa utulivu mkubwa kwa kuwaombea viongozi hawa ili yanayotokea ya kiimani anayetakiwa kusamehewa asamehewe huko aliko.”amesema Mselle.


Katika kipindi cha ukoloni, wakoloni walifanya mambo mengi, katika nchi walizokuwa wakizitawala, Ujerumani ni nchi mojawapo iliyokuwa na makoloni Barani Afrika, mpaka kushindwa vita vya kwanza vya dunia na pia ilishiriki katika maovu  hayo;


Mfano ni kuwanyonga viongozi na watu waliokuwa wakiwasaidia viongozi hao, na kukata vichwa vyao na kuvipeleka Ujerumani  kwa ajii ya kuvifanyia utafiti na ubaguzi wa rangi, suala hili liliwafanya watu wengi kuwa na mitazamo tofauti kuhusu Ujerumani mpaka leo hii.


Tukio lililofanywa na Wajerumani ukiacha tu kuwanyonga na kukata vichwa vyao, pia walikuwa wakichemsha maji ya moto na kuviweka vichwa hivyo kwenye maji ya moto na kuondoa zile nyama ili wapate lile fuvu, tukio ambalo lilikuwa la kikatili sana.




Wakandarasi watakiwa kuzingatia mikataba ya miradi ya Maendeleo


Wakandarasi wa miradi mbalimbali nchini wametakiwa kuzingatia mikataba waliyowekeana saini na serikali katika kuhakikisha miradi inamalizika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa kwa manufaa ya wananchi na taifa kwa ujumla.

 

Akizungumza katika hafla ya kushuhudia utilianaji saini mikataba ya upelekaji wa huduma za maji kwenye kata za Marangu Mashariki, Marangu Magharibi, Kibosho Kati na Kirima yenye jumla ya shilingi bilioni 2.76 Mkuu wa Wilaya ya Moshi Kisare Makori

 

“Rais Samia Suluhu Hassan ameelekeza nguvu kubwa sana katika kutoa huduma kwenye jamii ikiwamo barabara, maji, elimu na afya; Huduma ya upatikanaji wa maji safi na salama imepewa kipaumbele kikubwa sana,sisi tumekuwa tukipata fedha nyingi sana kwenye maeneo mengi kwa ajili ya miradi ya maendeleo,” alisema Makori

 

“Kwa mwaka huu wa fedha 2023/2024 tumepokea bilioni 1.5 kwqa ajili ya mradi mkubwa wa maji wa Ukaoni, Kibosho Kati na Kirua Vunjo Kusini; Kukamilika kwa mradi huu kutakwenda kupunguza adha ya upatikanaji wa maji safi na salama na takribani watu 15,000 watanufaika,” aliongeza Makori.

 

Katika hafla hiyo wakandarasi walipata fursa ya kuzungumza mbele ya Mkuu wa Wilaya Kisare Makori kuhusu namna watakavyotekeleza miradi waliyopata kwenye maeneo husika.

 

Mkurugenzi wa Kampuni ya Miniac Construction Ltd Ramadhani Sangiwa amesema kamati za ulinzi na usalama ngazi ya vijiji na kata zitoe ushirikiano katika kulinda vifaa vya miradi.

 

Kwa upande wake Diwani wa Kibosho Kati Bahati Mamboma ambaye mradi wa maji utatekelezwa kwa manufaa ya wakazi 8,000 amesema kwa sasa maji hayatoshelezi wakazi hao hivyo kukamilika kwa mradi huo kutaifanya kata yake kuondokana na changamoto hiyo. 


Kwa niaba ya madiwani wa halmashauri ya Moshi Vijijini Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Morris Makoi amewataka wakandarasi kuzingatia suala la utunzaji wa mazingira katika maeneo ya mradi.

 

Katibu wa Chama cha Mapinduzi  (CCM) wilaya ya Moshi Vijijini Ramadhani Mahanyu amewataka wakandarasi waishirikishe jamii ili kuondokana na sintofahamu ambayo mara kadhaa imefanya miradi baadhi isifanikiwe kama ilivyotakiwa

 

Maelekezo ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ni kufikisha asilimia 85 ya upatikanaji wa maji kwa maeneo ya vijijini ifikapo mwaka 2025. Kwa sasa upatikanaji wa huduma ya maji kwa maeneo ya Moshi Vijijini ni asilimia 84.5 ambapo miradi hiyo itakapokamilika itaongeza upatikanaji wa huduma ya maji na kufikia asilimia 88 ifikapo Juni 2024.






Thursday, January 25, 2024

Taifa Stars yatolewa, yapata funzo Afcon 2023



TIMU ya Soka ya Tanzania "Taifa Stars" imeshindwa kuendelea na michuano ya 34 ya Mataifa ya Afrika (AFCON) baada ya sare dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo hivyo kuvuna alama mbili tu. 


Matokeo hayo yaliinyima Taifa Stars kuingia katika hatua ya 16 Bora baada ya kufungwa katika mchezo wa kwanza wa Kundi F dhidi ya Morocco kwa mabao 3-0 kisha kutoa sare ya 1-1 na miamba ya soka Zambia (Chipolopolo). 


Taifa Stars inaungana na TIMU nyingine nane ikiwamo miamba Tunisia, Gambia, Msumbiji, Guinea Bissau kufungasha virago na kurudi nyumbani kujiandaa na AFCON ijayo. 


Aidha katika Mashindano hayo jina la Saimon Msuva limeingia katika Kumbukumbu za AFCON baada ya kufunga bao pekee kwa Taifa Stars katika michuano hii mwaka huu inayoendelea katika viwanja sita katika ardhi ya Cote D'Ivoire.


 Watanzania walitamani kuiona bendera ya Tanzania ikipepea tena katika hatua zinazoendelea lakini haikuwa hivyo licha ya kupata funzo kwamba mafanikio ni hatua na hatua inatengenezwa. 


 Vidole vya lawama vinaendelea kunyoshwa kwa baadhi ya wachezaji na viongozi Jambo ambalo sio sawa kwani ndio uwezo ulipoishia ni vema kuganga yajayo na mapya. 


 Katika michuano hiyo mwaka huu uwezo wa kila mmoja ulionekana hususani katika umiliki wa mpira na kudhihirisha kuwa Taifa Stars sio vibonde katika kundi F. 


 Stars ilimiliki kwa asilimia 48 dhidi ya Morocco, asilimia 52 dhidi Zambia na asilimia 54 dhidi ya DR Congo. Hilo ni jambo zuri na linapendeza huku tukitakiwa kuboresha.


 Kutengeneza wachezaji walio bora kwa ajili ya AFCON zijazo itatusaidia kupata tunachokitaka, kwani safari hii imedhihirisha wazi kuwa tunapaswa kujipanga kwani kuna Mabadiliko makubwa yamefanyika kwa kila Taifa.


 Mojawapo ni kutengeneza wachezaji wenye Kasi ili kufika kwa wakati kwenye matukio ndani ya uwanja, wachezaji wetu walikuwa wanafika kwa kuchelewa hivyo kufanya makosa mengi. 


 Pia watanzania wanapaswa kuujua mpira na kuuelewa badala ya kuzitupa lawama kwa makosa madogo madogo ya ndani ya uwanja. 


 Wachezaji mnaochipukia waangalieni wenzenu, AFCON hii, mmewaona wengi wanacheza nje ya nchi zao hivyo basi bila kutoka hatuwezi kutengeneza Taifa Stars.

 Hongera Taifa Stars, Tunashukuru kwa kutuwakilisha AFCON 2023 

 +255 768 096 793

Wednesday, January 24, 2024

Wafanyabiashara Kilimanjaro waonywa kuficha sukari, Wananchi kilio kizito bei ya sukari

Sukari ipo na sisi kama serikali ya mkoa tukimkamata mfanyabiashara yeyote ameficha sukari, tutachukua sukari yake, huwezi kuwaonea wananchi. Tutapita kwenye maduka kukagua wanaojipangia bei yao na kuwaumiza wananchi."- NURDIN BABU, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro
 

Wakazi wa Manispaa ya Moshi wanaendelea kupambanana changamoto ya bei ya sukari ambapo hadi sasa kilogramu imekuwa ikiuzwa kati ya shilingi 3,000 hadi 5,000.

Hatua hiyo imewafanya baadhi ya wakazi wa manispaa hiyo kutafuta njia mbadala ya namna ya kuipata sukari kwa ajili ya matumizi ya familia zao.

Wakizungumza na gazeti hilo wakazi hao wamesema bei ya sukari ipo juu hatua ambayo imekuwa ikiathiri familia zao ambazo zilizoea kuitumia sukari katika chai au uji kwa ajili ya watoto wanaosoma shule.

“kilo ya sukari ilikuwa inauzwa Sh 3,000 hadi 3,200, lakini kwa sasa unapokwenda unauziwa Sh 4,500 hadi 5,000, hivyo hakuna bein elekezi ambayo unaweza kuipata sukari,” alisema Gadson Sadick Mdee, mkazi wa Majengo, Moshi.

Aidha mkazi huyo aliwanyooshea kidole cha lawama wafanyabiashara wanaokiuka taratibu za serikali ambapo imeweka bei elekezi ya bidhaa hiyo.

“Changamoto ya sukari imekuwa ni kubwa kwa wakazi wa moshi, unakuta bei elekezi ya serikali ni tofauti na pale unapokwenda madukani kununua. Kama ulizoea kununua sukari kwa mteja wa duka ambaye umemzoea , unapokwenda kununua na kumkuta hana bidhaa hiyo, unapoenda sehemu nyingine unauziwa kwa bei ya kulanguliwa na si kwa bei ambayo tumekuwa tumeizoea,” aliongeza
Mdee.

Hata hivyo kuwafanya watoto wao waridhike na kifungua kinywa wamekuwa wakinunua muwa kisha kuukamua na kuongeza maji kidogo na majani yanachanganywa ili kutengeneza chai.

“Tumelazimika kutafuta njia mbadala kwa ajili ya kuwafanya watoto wetu waridhike waweze kwenda shuleni. Tumekuwa tukinunua muwa tunaukamua tunachanganya maji na majani ya chai kidogo unamdanganyia mtoto anakunywa anakwenda shuleni.

Saimon Msumari, mkazi wa Kata ya Mawenzi katika Manispaa ya Moshi alisema miwa hiyo wamekuwa wakiipata kutoka wilayani Mwanga, Hai na Moshi Vijijini  na imekuwa rahisi kuliko kununua sukari kilogram moja.

“Tumerudi kule kwenye miaka ya 70 hadi 80 tuliwahi kutumia miwa na kwa sasa miwa na yenyewe imepanda bei, tunaitumia tunaikamua ili mtoto asubuhi aweze kupata chai. Miwa kwa sasa hivi imepanda bei  kutoka Sh 1,000 hadi 1,500,” alisema Msumari   

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu aliwataka wafanyabiashara kuacha mara moja mchezo wa kuficha sukari na kisha kuipandisha kinyemela

Sukari ipo na sisi kama serikali ya mkoa tukimkamata mfanyabiashara yeyote ameficha sukari, tutachukua sukari yake, huwezi kuwaonea wananchi. Tutapita kwenye maduka kukagua wanaojipangia bei yao na kuwaumiza wananchi. Wafanyabiashara msitake kugombana na serikali kwa sababu ya sukari,” alisema Babu.

Monday, January 22, 2024

Makonda: CCM sio Chama cha kusubiri Uchaguzi


Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo Paul Makonda amewataka wananchi kutambua kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) sio Chama kinachosubiri kuzungumza na wananchi wakati wa Uchaguzi.


Komredi Makonda amesema CCM Iko katika ziara ya mikoa 20 huku mkoa wa Kilimanjaro ukiwa wa Nne katika kusikiliza kero na changamoto zinazowakabili wananchi na kuwaeleza wananchi kazi ambazo zimefanywa na Serikali ya Awamu ya sita ya  Rais Samia Suluhu Hassan.

 

Aidha akiwa wilayani Same katika ziara yake akitokea mkoa wa Tanga, Komredi Makonda amewaonya Watendaji Wazembe , Wababishaji na wale wanaonyanyasa wananchi,  kuwa watawashughulikia kikamilifu kwa kuwatambua kwa majina yao.


Komredi Makonda amesema watendaji wa serikali katika idara muhimu kama Afya, Maji, Ardhi  na Umeme watashughulikiwa ipasavyo kwa majina wao.


Pia Mbunge wa Same Magharibi Dkt. David Mathayo amesema anamshukuru  Rais Samia  kwa jinsi alivyowasaidia wananchi wa Kata ya Hedaru kutatua changamoto ya Kituo cha afya.


Hata hivyo Dkt. Mathayo ameomba mji wa Hedaru upandishwe hadhi ya kuwa mji mdogo kutokana na idadi ya watu inavyozidi kuongezeka kwa idadi ya watu siku baada ya siku.


Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu amesema kwa kipindi cha miaka miwili na nusu ya uongozi wa rais mkoa umepata Sh bl 821  kwa zaidi ya miaka 25  mkoa haujawahi kupata fedha hizo.






Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Komredi Paul Makonda akiwa Same, mkoani Kilimanjaro katika ziara yake ya siku mbili kati ya mikoa 20 nchini Tanzania.






Tuesday, January 16, 2024

Pandashuka Mirathi ya Paul Kyauka Njau, zamrudisha tena Catherine Kyauka mahakamani ili kupata haki yake

Pandashuka za kesi ya Mirathi Na.5 ya mwaka 2002 zimesababisha mrithi wa Mirathi hiyo kupambana kupata haki yake kwa mwaka wa 20 sasa.


Mrithi wa Mirathi ya Marehemu Paul Kyauka Njau, Bi. Catherine Kyauka amejikuta katika sintofahamu ya kupata haki yake huku akitakiwa kuondoka katika nyumba anayoishi kwa kigezo kwamba sio mrithi halali wa Mali za marehemu.


Nyumba Na. 17/18 aliyopo Bi Catherine ipo mtaa wa Market (maarufu Market Street-Kiusa) mjini Moshi ambapo Oktoba 27, 2023 mbele ya Jaji Andrea Kilimi wa Mahakama Kuu, Wakili Msomi Stella Simkoko akiwa upande wa Bi. Catherine aliiomba mahakama isimtoe mwanamke huyo katika nyumba hiyo akirejea kesi mbalimbali mpaka shauri la msingi liwe limefungwa ndipo utaratibu mwingine uendelee.


Upande unaotaka Bi. Catherine aondolewe ukisimamia hukumu zilizotolewa mnamo mwaka 2010 na 2014 na Jaji Edward Rutakangwa, wamekuwa wakiishinikiza mahakama imwondoe mwanamke huyo licha ya Rufaa zake zote kushindwa.


Hata hivyo mwanamke huyo ameendelea kusimama kidete ambapo mnamo Desemba 12, mwaka  2023 aliwasilisha ombi dogo mbele ya Jaji Adrian Kilimi wa Mahakama Kuu Moshi la kutaka asiondolewe katika nyumba anayoishi mpaka kesi ya msingi itakapofungwa.


Bi. Catherine akiwasilisha na Wakili Msomi Stella Simkoko aliiambia mahakama kesi ya msingi itakapofungwa ndio itafanya kila upande upate haki, hasa ikizingatiwa watoto wa mke wa pili na watatu wa marehemu hawakuhusishwa kwenye kikao cha kufanya uteuzi wa Mirathi ya marehemu Paul Kyauka Njau.


Ombi hilo mbele ya Mahakama Kuu Moshi limekuja wakati ambapo faili la kesi ya Mirathi Na. 5 ya mwaka 2002 la Marehemu Paul Kyauka Njau likiwa halionekani hatua ambayo inafanya kesi hiyo kushindwa kufikia maamuzi.


Upande wa wanaoshinikiza mahakama kutupilia mbali suala la mrithi wa Mirathi ya Marehemu Paul  ambaye ni baba yake mzazi wa Bi. Catherine uliongozwa na Wakili Msomi D. Gadau ambaye aliiomba mahakama  impe muda wa kuwasilisha vielelezo kwa njia ya mtandao.


Ombi la Wakili Msomi Gadau lilikubaliwa na pande zote ambapo Jaji Kilimi alitaja tarehe za kuwasilisha vielelezo na kabla ya Februari 26, 2024 ataendesha shauri hilo kwa njia ya mtandao.


Aidha Jaji Kilimi alitaka siku ya hukumu mnamo Februari 26,2024, upande wa wanaoshinikiza mahakama usimpe haki ya urithi Bi. Catherine uwepo mubashara ili kujiridhisha na baadhi ya masuala yanayoleta utata katika kesi hiyo.


Kesi hii Na. 5 ya mwaka 2002 imechukua muda mrefu takribani miongo miwili hivyo kuipa wakati mgumu mahakama kuamua nani anayestahili kuwa mrithi halali wa mali za marehemu Paul K. N


Kesi hiyo ilifunguliwa mnamo Oktoba 27, 2003 na kuendeshwa na Jaji Edward  Rutakangwa wa Mahakama Kuu Moshi, ambaye ndiye aliyetoa hukumu ya kuwa baadhi ya warithi akiwamo Bi. Catherine wasiwemo katika nyumba Na. 17/18 'K' mnamo 2010 na 2014.

Marehemu Paul Kyauka Njau alifariki dunia mnamo Februari 17, 2002 katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC mjini Moshi mkoani Kilimanjaro na kuzikwa Februari 23, 2002 kijijini kwake Ndima, Mrao-Mashati wilayani Rombo akiacha kiasi cha zaidi shilingi milioni 80 na mali kama magari,  mitambo mbalimbàli, viwanja na nyumba vyenye wastani wa zaidi ya shilingi milioni 400.


Aidha katika Kikao cha ukoo wa marehemu kilichoketi Mnamo Juni 23, 2002 kikiwa na madhumuni ya uteuzi wa mfuatiliaji wa mirathi hiyo kilianisha watoto wa marehemu walio hao wakati huo kufikia 15 huku wengine saba wakipoteza maisha hivyo kufikia jumla ya watoto aliowazaa marehemu enzi za uhai wake kufikia 22.


Mke mkubwa ambaye ni Mjane wa marehemu Pauli K.N, mama Kresensia Pauli Kyauka alikataa kuwa mfuatiliaji wa mirathi hiyo mbele ya wajumbe 49 waliohudhuria kikao hicho cha ukoo kwa kutaja sababu za yeye kuwa mzee na ugonjwa hivyo mtoto mkubwa Febronia Pauli Kyauka na mwingine aliyefahamika kwa jina la Emmanoel Pauli Kyauka Njau walipendekezwa kufuatilia.


Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa marehemu alizaa watoto 22 kutoka kwa wake watatu ambao ni Kresensia P.K.N, Kristina na Pulkeria P.K.N ambapo katika ufuatiliaji wa mirathi baadaye Febronia alifariki Dunia na jukumu lote kusalia kwa Emmanoel.


Mke mdogo wa tatu ambaye ni Pulkeria alifanikiwa kuzaa na marehemu Pauli watoto saba akiwamo Catherine ambae amejitosa kutaka haki itendeke kwa watoto wote wa marehemu na sio upande mmoja pekee.


Mnamo Desemba 12, 2023 wakati Jaji Kilimi wa Mahakama Kuu ya Moshi alitaka wakati wa uwasilishaji wa vielelezo vya ombi lao kwa njia ya mtandao, alitaka wahusika akiwa Emmanoel P.K.N wawepo na awaone mubashara kupitia intaneti kwa kuwa mnamo Januari kabla ya kufikia maamuzi mnamo Februari 26 ataendesha kwa njia ya mtandao.


Marehemu Pauli Kyauka Njau aliacha mali zinazokadiriwa kuwa zaidi ya milioni 400 ambazo zimekuwa na sintofahamu nyingi kwa muda mrefu sasa, hivyo kuipa ugumu mahakama kufikia mwafaka wa shauri hilo

Monday, January 15, 2024

Dkt. Emmanuel Nchimbi ateuliwa kuwa Katibu Mkuu CCM Taifa, aziba nafasi iliyoachwa na Chongolo

 


Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Taifa imemteua Dkt.Emmanuel Nchimbi kuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).  Dkt. Nchimbi anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Daniel Chongolo ambaye alijiuzulu.

 

Desemba 3, 2016, Nchimbi aliteuliwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli kuwa Balozi, baadaye alipangiwa kituo cha kazi Nchini Misri na kisha Agost 11, 2023 Rais Samia alimrejesha nyumbani.  Leo Januari 15, 2024, Dkt. Nchimbi ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi akichukua nafasi ya Chongolo aliyejiuzulu nafasi hiyo.


WASIFU WA DKT. EMMANUEL NCHIMBI

Dkt. Emmanuel Nchimbi alizaliwa Desemba 24, 1971 mkoani Mbeya, (atafikisha miaka 54 Desemba mwaka huu). Elimu yake ya Msingi aliianzia jijini Dar es Salaam katika Shule ya Msingi Oysterbay kati ya mwaka 1980 – 1986.

 

Baba yake mzazi, Mzee John Nchimbi kutoka wilayani Songea ni askari mstaafu wa Jeshi la Polisi na wakati anastaafu alikuwa Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara. Mzee Nchimbi pia amewahi kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) kwa vipindi viwili kupitia kundi la majeshi na baadaye katibu wa CCM wa mkoa, alikoma kushiriki masuala ya kisiasa mfumo wa vyama vingi ulipoanzishwa.

 

Dk Nchimbi alijiunga na elimu ya sekondari kwenye Shule ya Sekondari Uru kati ya mwaka 1987 – 1989 (kidato cha I – III) halafu akahamia Shule ya Sekondari Sangu na kukamilisha kidato cha nne mwaka 1989 – 1990.

 

Nchimbi alisoma Shule ya Sekondari ya Forest Hill, Mbeya masomo ya kidato cha V na VI mwaka 1991 – 1993. Alijiunga katika Chuo cha IDM Mzumbe (Morogoro) na kuhitimu Stashahada ya Juu ya Utawala (mwaka 1994 – 1997).

 

Wakati anahitimu IDM, pia alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) na mwaka uliofuatia (1998), alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM).

 

Dk Nchimbi amewahi kuajiriwa na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kati ya mwaka 1998 – 2003.

 

Alisoma shahada ya uzamili ya usimamizi wa biashara Chuo Kikuu cha Mzumbe mwaka 2001 – 2003 akibobea kwenye maeneo ya (benki na fedha).

 

Dk Nchimbi aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Bunda (mwaka 2003 – 2005) na (mwaka 2008 – 2011) alisoma na kufanikiwa kuhitimu shahada ya uzamivu (PhD) katika Chuo Kikuu cha Mzumbe.

 

Dk Nchimbi amemuoa Jane na wana watoto watatu.

 

MBIO ZA UBUNGE

Dkt. Nchimbi alirudi nyumbani kwao (Songea Mjini) kuanza harakati za ubunge tangu alipokuwa anaongoza UVCCM. Ilipotimu mwaka 2005, aliingia kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi akakutana na Edson Mbogoro wa Chadema aliyekuwa mpinzani wake mkuu. Dk Nchimbi alisaidiwa na mtandao mkubwa wa CCM na kupata ushindi wa asilimia 67.6 dhidi ya asilimia 30.5 za Mbogoro.

 

Mara tu baada ya kuwa mbunge, Rais Kikwete alimteua kuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, hii ilikuwa Januari 2006, alidumu kwenye wizara hiyo hadi Oktoba 2006 alipohamishiwa kwenye Wizara ya Kazi, Ajira na Vijana – hapa pia alikuwa Naibu Waziri tangu Oktoba 2006 hadi Februari 2008 kisha Wizara ya Ulinzi na Kujenga Taifa ambako pia alikuwa Naibu Waziri hadi Novemba 2010.

 

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, Dk Nchimbi alijitosa tena Jimbo la Songea Mjini. Kampeni za 2010 zilimnyima usingizi pamoja na kuwa chama chake kilikuwa kimechukua asilimia zaidi ya 90 ya vijiji, vitongoji na mitaa mwaka 2009.

 

Kama kawaida, alipambana tena na Mbogoro wa CHADEMA na kumshinda kwa mara ya pili, japo safari hii Dk Nchimbi akipoteza takriban ushindi wa asilimia 10 ukilinganisha na mwaka 2005. Katika uchaguzi huo, alipata asilimia 59.9 dhidi ya 37.48 za Mbogoro.

 

Upandaji vyeo wa Nchimbi uliendelea, Rais Kikwete alimpa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo akiwa Waziri kamili, alidumu hapo hadi Mei 2012 alipohamishiwa Wizara ya Mambo ya Ndani kabla ya kujiuzulu Desemba 2013.

 


JAIZMELA yazindua LOGO ya mwaka 2024

 


LOGO ni nembo. ni kitu cha muhimu sana katika biashara yako, watu wengi hawajui maana ya kuwa na logo. Logo ni utambulisho wa brand yako au ni utambulisho wa kile unachokifanya.


Nembo au logo ni picha ya msingi ya bidhaa na kampuni yako. Utambulisho wa biashara, kampuni yako au bidhaa unaonyeshwa kupitia nembo yako, ambayo ni pamoja na jina la kampuni yako. Hivyo, nembo ni moja kati ya mambo makuu ambayo yanafanya biashara yako kukumbukwa na kutambulika. mfano hapo chini nimekuwekea baadhi ya logo, pamoja sijaandika ni logo za kampuni gani lakini umesha fahamu ni za kampuni gani.


Logo ni utambulisho wa biashara yako yaani mtu hata kama hakufahamu wewe anakua kesha fahamu biashara yako kwa kuwa logo inauza au inafanya mauzo bila wewe kuwepo. Mfano kuna watu wanatumia logo ya mtu maarufu kuuza bidhaa zake na wewe unaponunua unanunua kwa sababu unanunua bidhaa inayofahamika, mfano vifaa vya yamaha bei yake ni kubwa tofauti na vifaa vingine kutokana na umaarufu wake. Logo yako ikiwa maarufu hata kama utaondoka duniani bado watoto wako wataendelea kuuza bidhaa kwa kutumia logo yako.


Logo inaweza kuwa maarufu kuliko wewe mwenyewe.