Ukweli na Kuheshimiana ni kiini ujenzi wa jamii zetu

Ulimwenguni kwa sasa kumejaa habari potofu na upotoshaji, ni muhimu kuhakikisha kwamba ukweli na kuheshimiana vinakuwa kiini kwa ujenzi wa jamii zetu.

Mapambano dhidi ya Habari za Uongo hayapaswi kukoma

Habari za uongo, habari za uongo zinazosambazwa kwa lengo la kumdhuru mtu au jambo fulani, huifanya jamii kuwa na sintofahamu. Zinaweza kutumika kwa madhumuni ya kiitikadi, kisiasa au hata uhalifu, kama vile ulaghai mtandaoni unaolenga kuiba data ya kibinafsi.

Utandawazi na Athari zake katika Uandishi wa Habari

Katika jamii yetu ya kisasa, ambapo habari ziko kila mahali na zinaweza kupatikana kwa kila mtu, mara nyingi ni ngumu kutofautisha kati ya vyanzo vya kuaminika na habari bandia.

Uandishi wa Habari nguzo msingi mkuu kwa ujenzi wa jamii inayojitambua

JAIZMELA blog ni miongoni mwa vyanzo vya habari, zilizochakatwa kwa kuzingatia miiko ya uandishi wa habari.

Mila na Desturi ni nguzo muhimu

Mila na desturi ni nguzo muhimu sana katika utamaduni wa jamii yoyote ile; mila ni sawa na sheria zisizoandikwa. Mila ni taratibu za maisha na mwenendo zinazofuatwa na jamii fulani katika utendaji kulingana na historia na utamaduni wao. Mila zinatambulisha maadili ya jamii husika, huelezea namna jamii inavyoendesha mambo yake.

Saturday, February 27, 2021

MAKTABA YA JAIZMELA: Paul Rusesabagina ni nani?

 


.........Safari ya Paul Rusesabagina hadi mikononi mwa Kagame

Mwishoni mwa mwezi Agosti mwaka huu nchini Rwanda na ulimwengu kote kuliibuka taarifa za kustaajabisha zilizoihusu serikali ya Rwanda iliyo mikononi mwa Paul Kagame baada ya kukamatwa kwa mwanaharakati Paul Rusesabagina.

Rusesabagina ambaye alianza kuwa maarufu kutokana na uokoaji wake wa mamia ya wanyarwanda wakati wa mauaji ya kimbari mnamo mwaka 1994 kupitia kazi yake ya hotel alikamatwa na vyombo vya usalama vya kimataifa na kumkabidhi mikononi mwa serikali ya Rwanda.

Idara ya Upelelezi nchini Rwanda ilisema kupitia ujumbe wa Twitter kuwa Rusesabagina kuwa yupo mikononi mwa Rwanda kwa ushirikiano wa kimataifa bila kutaja taifa ambalo lilisaidia kukamatwa kwa Rusesabagina.

Waranti ya Kimataifa ilitolewa kwa ajili ya kukamatwa kwake na polisi ya Kigali. Hata hivyo mwanaye wa kiume Tresor Rusesabagina katika taarifa yake kwa vyombo vya habari aliweka bayana kuwa kabla ya kukamatwa kwake mama na dada yake walikuwa wakizungumza na baba yao wakati akiwa safarini huko Dubai.

“Huo ndio muda wa mwisho kabisa ambao aliongea nasi,” alisema Tresor na kuongeza kuwa hajui sababu za baba yake kwenda Dubai. Rusesabagina mwenye umri wa miaka 66 hadi sasa bado yupo mikononi mwa vyombo vya usalama vya Rwanda. Anatuhumiwa kwa makosa ya ugaidi akiwa kama mwanzilishi, kiongozi na mfadhili wa vurugu.

Katika makala haya tutamwangazia Rusesabagina tangu alipoliona jua hadi kukamatwa kwake.

Rusesabagina alizaliwa Juni 15, 1954 huko Murama, Kigali akiwa ni miongoni mwa watoto tisa waliozaliwa kwa baba Mhutu na mama Mtutsi. Wazazi wake walimpeleka kusoma shule iliyokuwepo huko Gitwe ambayo ilikuwa ikiongozwa na Kanisa la Wasabato. Akiwa na umri wa miaka 13 alikuwa amejifunza vizuri Kiingereza na Kifaransa kwa ufasaha. Alimuoa mwanadada aliyefahamika kwa jina la Esther Sembeba mnamo Septemba 8, 1967 na kuwa mkewe wa kwanza. Mwishoni mwa ujana wake Rusesabagina aliona ni vema akawa mtumishi wa kanisa. Yeye na mkewe waliamua kuondoka nchini Rwanda na kwenda zao nchini Cameroon ambako Rusesabagina alisoma katika seminari.

Mnamo mwaka 1978 Rusesabagina na mkewe walirudi nchini Rwanda na kuweka makazi yao Kigali. Wakiwa hapo alikutana na rafiki yake tangu wakiwa watoto Isaac Mulihano ambaye alimwalika Rusesabagina kuomba kazi katika hoteli moja iliyofahamika kwa jina la Hôtel des Mille Collines. Akiwa hapo alipata fursa ya kuwa kiongozi na miaka michache baadaye alipelekwa Uswisi na akiwa huko alihudhuria masomo zaidi ya hoteli pia jijini Brussels, Ubelgiji.

Kutokana na umbali kama ambavyo wahenga walivyosema ‘Fimbo ya Mbali haiui Nyoka’, penzi lake na Esther liliingia ruba ambapo walitalikiana mnamo mwaka 1981. Rusesabagina akajikuta akipata majukumu makubwa zaidi ya kulea watoto wake watatu ambao ni Diane, Lys na Roger.

Kama ujuavyo maisha ni safari ndefu isiyo na mwisho, mnamo mwaka 1987 alialikwa kwenye harusi moja ambako huko alikutana na mwanadada Tatiana, ambaye alikuwa na heshima zake na muuguzi wa Kitutsi huko Ruhengeri. Rusesabagina hakujivunga kuonyesha hisia zake za upendo. Alitumia kila njia kumpata Tatiana.

Taarifa kutoka nchini Rwanda zinasema Rusesabagina aliwahi kutoa rushwa kwa wamiliki wa hoteli vilevile kwa Wizara ya Afya ili ufanyike uhamisho wa kikazi wa Tatiana kutoka Ruhengeri hadi makao makuu jijini Kigali. Miaka miwili baadaye azma yake ilifanikiwa kwani alimwoa Tatiana ambaye aliwaasili watoto na baadaye akampata mtoto waliyempa jina la Tresor.

Mnamo mwaka 1992 Rusesabagina alipandishwa cheo na kuwa Meneja Mkuu Msaidizi wa Hotel ya Diplomates ambayo ina uhusiano naile ya Mille Collines.

 

RUSESABAGINA NA MAUAJI YA KIMBARI 1994

Wakati vurugu za Rwanda zilipoanza, Rusesabagina alikuwa  masomoni jijini Nairobi nchini Kenya pia Uswisi na baadaye Ubelgiji. Serikali ya Wahutu iliyokuwa mikononi mwa  Rais Juvenal Habyarimana ilijikuta ikipata shinikizo kali kutoka kwa vikosi vya kijeshi ya Watutsi. Mapanga yaliagizwa na kuingizwa jijini Kigali na kukabidhiwa kwa Interahamwe. Watutsi walianza kupinga madai ambayo yalitangazwa na kituo cha redio cha RTLM kuwa Watutsi wanapanga kuwaangamiza wahutu wote nchini humo.

Manmo Aprili 6, 1994 Rais Habyarimana akiwa kwenye ndege akitokea Tanzania alipoteza maisha baada ya ndege yake kutunguliwa wakati ilikuwa ikikaribia kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kigali. Katika ndege hiyo kulikuwa na Rais wa Burundi Cyprien Ntaryamira, Kiongozi wa Kijeshi wa Rwanda Chief of Staff Deogratias Nsabimana na Luteni Elie Sagatwa ambaye alikuwa Mkuu wa Idara ya Usalama ya Rais.

Tangu walipouawa kutofautiana kwa mitazamo miongoni mwa serikali na wananchi kulianzisha vuurugu hizo ambapo Aprili 7, 1994 aliuawa Waziri Mkuu Agathe Uwilingiyimana na Mlinzi wa Rais; pia walinzi 10 wa amani wa Umoja wa Mataifa raia wa Ubelgiji waliuawa. Interahamwe ikaanza kuwawinda Watutsi na kuanza kuwaua na ukawa mwanzo wa mauaji ya kimbari.

Japokuwa Rusesabagina alikuwa Mhutu mkewe Tatiana alikuwa Mtutsi hivyo watoto nao walikuwa na damu za pande zote mbili. Hivyo kutokana na kutokuwa na uwezo wa kutoroka kwenye ukanda huo wa vita na familia yake, Rusesabagina aliichukua familia yake hadi hotelini alikokuwa akifanya kazi kwa ajili ya usalama. Katika hoteli hiyo mameneja wengine walitoroka kuepuka kuuawa.

Rusesabagina akawapigiwa simu wamiliki wa hoteli ambao ni Sabena walimtumia barua kuwa atasalia hapo kama kaimu meneja mkuu wa Mille Collines. Hata wakati Wahutu walipotishia kuivamia hotel hivyo Rusesabagina alisimama kidete kuhakikisha watoto na mkewe wanawakua salama.

Alifanya mipango ya kuwatorosha kwenda nchi nyingine huku yeye akibaki kuisimamia hoteli hiyo na wakimbizi baadhi.

Rusesabagina alikaririwa mnamo Machi 1, 2005 akisema, “ Kila mmoja wetu alikuwa anajua kuwa tutakufa, hilo halikuwa na swali. Swali pekee lilikuwa ni kwa namna gani. Watatukata vipande vipande? Wakiwa na mapanga yao watakukata mkono wako wa kushoto. Kisha kutoroka na kuonekana tena masaa machache baadaye na kuukata mkono wako wa kulia. Kisha mguu wa kushoto n.k Watafanya hivyo hadi unakufa.”

Hata hivyo licha ya hofu yote hiyo Rusesabagina, mkewe na watoto na baadhi ya wakimbizi walifanikiwa kuingia nchini Tanzania na shukrani za pekee ziwaendee RPF iliyokuwa mikononi mwa Paul Kagame. Baada ya kuishi miaka miwili, Rusesabagina aliomba makazi nchini Ubelgiji kasha kuondoka na familia yake jijini Brussels. Wakiwa huko walipokea vitisho hali ambayo iliwafanya waombe kuishi Texas nchini Marekani licha ya kwamba wanaendelea kuisimamia nyumba yao huko Ubelgiji.

Rusesabagina alijizolea umaarufu mkubwa na kutunukiwa tuzo mbalimbali kutokana na filamu ya Hotel Rwanda ya mwaka 2004 ambayo alicheza kama Don Cheadle. Rusesabagina alikuwa na makazi huko Brussels, Ubelgiji na San Antonio, Texas nchini Marekani. Rusesabagina ana uraia wa Ubelgiji na Marekani. Rusesabagina alianzia taasisi ya kujitolea ya Hotel Rwanda Rusesabagina  ili kupambana dhidi ya ukiukwaji wa haki za binadamu. Madai yote yanayomkabili dhidi ya serikali ya Paul Kagame ameyakataa.

Makala haya yametayarishwa na Jabir Johnson kwa msaada wa mitandao, vitabu na maktaba mbalimbali na kuchapishwa Septemba 2020 katika gazeti la LaJiji nchini Tanzania.

Rwanda yakubali kuilipa ndege iliyombeba Rusesabagina

 

Rwanda imekubali kuwa ndiyo iliyolipa ndege iliyokuwa imembeba Paul Rusesabagina, mpinzani wa utawala wa Kigali ambayo ilimtoa Dubai na kumpeleka mjini Kigali Rwanda mwishoni mwa mwezi Agosti 2020.

Kulingana na runinga ya Al Jazeera, Waziri wa sheria wa Rwanda Johnston Busingye yalikubali kuwa Rwanda iliilipa ndege hiyo, baada ya kuonyeshwa video ambapo yeye na washauri wake wa masuala ya mahusiano ya umma ambayo aliitumia televisheni ya Al Jazeera kimakosa.

"Serikali ililipa ," Busingye alimuambia mtangazaji wa kipindi cha UpFront Marc Lamont Hill.

"Kulikuwa na mtu aliyekuwa anafanya kazi na Rusesabagina kwa muda mrefu, ambaye alikuwa akifanya kazi na idara yetu ya upelelezi wa makosa ya uhalifu, ambaye alikubali kumlaghai na malipo yalitumiwa kusaidia kufanikisha kumleta Rusesabagina hadi Rwanda," aliongeza. "Serikali haikuhusika kumsafirisha. Ilimlipa huyu mwanaume aliyetaka kumleta nchini Rwanda ."

Kabla ya mazungumzo na Al Jazeera, video hiyo inamuonyesha Waziri wa sheria wa Rwanda akishauriwa na wataalamu wawili wa taasisi ya Chelgate ya Bwongereza alipokuwa akijiandaa kuzungumza na waandishi wa habari na video hiyo ilitumwa kimakosa kwa waandaaji wa kipindi cha UpFront cha Al Jazeera, kulingana na televisheni hiyo.

Wahandisi isaidieni Tanzania

Januari 20, 1961 mwanasiasa wa zamani wa Marekani aliyefahamika kwa jina la John F. Kennedy aliapishwa kuwa rais wa 35 wa taifa hilo kubwa duniani. JFK kama wengi walivyokuwa wakimwita alikuwa miongoni mwa marais waliopendwa na watu wa taifa lake.

Aliuawa Novemba 22, 1963, akiwa ni miongoni mwa marais wa Marekani waliouawa wakiwa madarakani. JFK ni rais wa nne wa Marekani kuuawa akiwa madarakani, lakini mauaji yake ni ya kwanza kurekodiwa kwenye mkanda wa video.

Wengi wanakataa kuamini kuwa mauaji hayo ni njama iliyofanywa na mtu mmoja pekee mwanajeshi wa kikosi cha majini, Lee Harvey Oswald, aliyekuwa na umri wa miaka 26 wakati huo, aliyeelekeza bunduki nje ya dirisha moja kwenye chumba kilichokuwa ghorofa ya sita na kuufyatulia risasi msafara wa rais.

Hata hivyo nukuu zake nyingi zimekuwa maarufu lakini hii imezidi zote, “Usiulize ni nini nchi yako inaweza kukufanyia, uliza nini unaweza kufanya kwa nchi yako,” Hii ni nukuu yake ya kwanza baada ya kuapishwa kushika wadhifa wa kuliongoza taifa hilo ambalo aliliongoza kwa miaka miwili kwa tiketi ya chama cha Democratic.

Mhandisi ni mtaalam aliyehitimu na elimu ya juu ya kiufundi. Jina la taaluma lina mizizi ya zamani. Neno "mhandisi" linatokana na Kilatini ingenium, ambayo inamaanisha kuwa na uwezo wa kubuni.

Wahandisi wa kwanza walihusika tu katika ujenzi na uendeshaji wa magari ya jeshi. Hii iliendelea kwa muda mrefu sana, hadi karne ya 16 wahandisi wa umma walionekana kujenga madaraja, na uhandisi wa umma ulizaliwa.

Wahandisi wa kwanza walitokea Urusi shukrani kwa Peter the Great, ambaye alituma vijana wenye talanta kusoma nje ya nchi.

Kawaida katika taratibu za ukamilifu wa mradi wa ujenzi kuanzia hatua ya awali kabisa, baada ya mbunifu majengo kumaliza kazi ya kuandaa michoro yake mhadisi ndiye mtaalamu wa pili kuweka utaalamu wake.

Ifahamike kuwa mhandisi ni mtaalamu mbunifu wa uimara wa jengo na mkandarasi ni mjenzi wa jengo akifanyika kazi vilivyobuniwa na wahandisi na wabunifu majengo.

Sasa huyu anayejulikana kama Structural Engineer ndiye Mhandisi hasa na huwajibika kwa uhandisi wa ubora na uimara wa jengo kwa kufanya mahesabu ya uimara (strength), uzito, nguvu na namna vitakavyokabiliana bila kuleta madhara kwenye jengo linalotarajiwa kujengwa.

Dunia inaadhimisha wiki ya wahandisi kila Februari 22 hadi 28 kila mwaka ambapo wahandisi hukutana na kubadilishana ujuzi wao na kusaidiana kutatua changamoto zinazowakabili.

Licha ya faida yake uhandisi una hasara yake; Ubaya wake ni pamoja na ugumu wa mafunzo, ambayo inalingana na jukumu kubwa la taaluma, umakini mkubwa na uvumilivu wa hali ya juu unahitajika.

Nchi ya Tanzania ni miongoni mwa mataifa yenye watu ambao wamesomea fani hii na wanaendelea kusomea fani hii; Rai kwa wasomi wa medani ya uhandisi; someni kwa manufaa ya taifa hili badala ya kuwaza kwenda nje kufanya kazi katika mataifa ya mengine.

Pia umakini mkubwa katika medani hii unatakiwa ili kuifanya kuwa na faida kubwa kuliko hasara kwani hata mataifa kama Urusi tunayoyaona yameendelea kiviwandani ni kutokana na fani hii ya uhandisi kupewa uzito wa kutosha kwa watu wake.

Kuna baadhi ya watanzania ambao wanasoma Urusi na wengine walishawahi kusoma. Jambo la msingi ni kwa wasomi hao kuwaza wataifanyia nini Tanzania. Je wanawaza kuiingiza porini au wanawaza kuifanya kama mataifa mengine makubwa.

Serikali hadi sasa inaendelea kuweka mazingira mazuri kwa ajili ya wanaosoma fani ya uhandisi isitoshe Rais John Pombe Magufuli ni miongoni mwa waliosoma fani hii na kila mmoja ameshuhudia tangu alipokuwa Waziri wa Ujenzi wakati ule hadi sasa anavyojitahidi kuweka mazingira mazuri kwa ajili ya kuifanya Tanzania iwe ya viwanda; kwa maneno mengine ni kwamba uchumi wa kati utaimarika na kuvuka viwango vyake endapo viwanda vitakuwapo vya kutosha.

Wakati dunia ikiadhimisha siku ya Wahandisi ni vema wahandisi wetu hapa nchini wakajitafakari upya wanawaza nini juu ya Tanzania yao.

Kocha wa Gymnastic John Geddert ajiua baada ya kushtakiwa kwa unyanyasaji

 

Kocha wa zamani wa Timu ya Olimpiki ya Marekani John Geddert amejiua mwenyewe ikiwa ni saa chache baada ya kushtakiwa kwa unyanyasaji wa kingono na biashara haramu ya binadamu.

Geddert aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 63 alikuwa kocha mkuu wa timu ya wanawake ya Jimnastiki katikamichuano ya Olimpiki mwaka 2012. Alifanya kazi kwa karibu na daktari wa timu Larry Nasar ambaye alishtakiwa kwa kuwanyanyasa wanamichezo.

Mwanasheria Mkuu wa serikali wa Michigan Dana Nessel amethibitisha kutokea kwa kifo hicho kwamba kilitokea jana Alhamisi mchana. Nassar alishtakiwa kwenda jela hadi miaka 300  mnamo mwaka 2018 baada ya kukutwa na hatia ya kuwanyanyasa wasichana 250.

Black Satelaite yatinga nusu fainali AFCON U-20 kibishi

Michuano ya soka kwa vijana chini ya umri wa miaka 20 barani Afrika imeendelea tena jana jijini Nouakchott katika viwanja mbalimbali kukishuhudiwa Ghana na Uganda zikitinga hatua ya nusu fainali.

Mlinda mlango wa Ghana Danlad Ibrahim alikuwa shujaa wa mchezo dhidi ya Simba Wadogo Wasioshindika  Cameroon baada ya kuokoa mkwaju wa penati kwenye ushindi wao wa matuta 4-2. Mchezo huo ulimalizika kwa sare ya 1-1 licha ya kuongezwa dakika 30 kufikia dakika 120.

Cameroon ilipata uongozi katika dakika ya 102 baada ya Mila kukwamisha mpira wavuni. Uongozi huo ulidumu kwa sekunde 70 nyota wa Black Satelaite Boateng kuisawazishia timu yake.

Katika changamoto ya mikwaju ya penati nyota wa Cameroon Goni Ali aligongesha mwamba huku Kevin Prince Mila akishuhudia mkwaju wake ukiokolewa na Danlad. Nyota wa Ghana Daniel Afriyie, Frank Kwabena, Ivan Anokye na Percious Boah walifunga penati zao.

Katika mchezo mwingine kulishuhudiwa Uganda ikiwaadhibu Burkina Faso kwa changamoto ya mikwaju 5-3 ya penati kwenye mchezo uliochezwa katika dimba la Cheikha Boidiya.

Mlinda mlango wa Uganda Komakech aliokoa mkwaju wa Yacouba Djiga na kuwasaidia Viboko hao wa Uganda kutinga nusu fainali. Uganda itacheza nusu fainali yake siku ya Jumatatu itakapowakabili Tunisia ambao wameitandika Morocco kwa changamoto ya mikwaju ya penati 4-1 huku Gambia ikishinda kwa mabao 3-0 dhidi ya Afrika ya Kati.

Friday, February 26, 2021

Thierry Henry abwaga manyanga CF Montreal

 

Mchezaji wa zamani wa Arsenal, Barcelona na timu ya taifa ya Ufaransa Thierry Henry amebwaga manyanga ya kuinoa timu ya Ligi Kuu ya Marekani ya CF Montreal kwasababu zake binafsi.

Henry mwenye umri wa miaka 43 yupo katika orodha ya makocha wanaowania na klabu ya Bournemouth  iliyopo Championship nchini England.

Alikuwa kocha wa Montreal tangu Novemba 2019. Henry amekaririwa akisema kuwa kuwa mbali na familia yake ndio sababu kubwa inayomfanya aachie nafasi hiyo kwa moyo mzito. “Kutokana na maradhi yanayoihangaisha dunia kwa sasa imekuwa vigumu kuwaona watoto wangu,” alisema Henry.

Nyota huyo amesema atarudi jijini London huku akitoa shukrani zake za dhati kwa Montreal kwa fursa muhimu  ya kuiongoza klabu hiyo kufika hatua ya mtoano kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2016. Kabla ya kwenda Montreal alikuwa msaidizi wa kocha wa Ubelgiji Roberto Martinez na baadaye alihudumu miezi mitatu akiwa na Monaco ya Ufaransa msimu wa 2018-19.

Mkurugenzi wa Montreal Olivier Renard amemshukuru Henry kwa muda wote aliokuwapo na klabu hiyo na ushirikiano aliouonyesha.

MAKTABA YA JAIZMELA: Roberto Carlos aitwa timu ya taifa

Februari 26, 1992 nyota wa zamani wa soka wa Brazil Roberto Calos aliitwa kwa mara ya kwanza katika kikosi cha timu ya taifa hilo. Alizaliwa Aprili Mosi, 1973 mjini Sao Paulo.

Aliitwa katika kikosi hicho akiwa na umri wa miaka 19 ambako alidumu hadi mwaka Kombe la Dunia la mwaka 2006. Akiwa na Seleccao alihudumu katika mechi 125 na kutupia mabao 11. Alikuwa katika nafasi ya ulinzi upande wa kushoto.

Jina lake kamili ni Roberto Carlos da Silva Rocha. Alianza maisha yake ya soka kama mshambuliaji lakini baadaye alionekana mzuri zaidi kama beki wa kushoto. Carlos amekuwa akitajwa kuwa katika historia ya soka, ni beki namba moja wa kushoto ambaye akili yake inawaza kushambulia zaidi.

Katika soka alipewa jina la utani la “The Bullet Man” kutokana na kuwa na miguu yenye nguvu, iliyopiga mipira ya faulo kwa ustadi mkubwa, faulo zake zilipimwa kuwa zilikuwa na uwezo wa kwenda kilometa 169 kwa saa.

Gwiji huyu alijulikana kwa stamina, kasi ya kukimbia, uwezo wa kumimina mipira yenye macho kutokea pembeni, kurusha mipira mirefu, na paja lake lilikuwa na ukubwa wa inchi 24 sawa na  sentimita 61. Mwaka 1997, licha ya kuwa beki, Carlos alifanikiwa kuwa mchezaji bora namba mbili wa dunia. Huyu ni mmoja wa mabeki bora zaidi wa kushoto waliowahi kutokea ka­tika soka.

Alipata umaarufu mkubwa akiwa na kikosi cha Real Madrid. Akiwa na timu ya  Carlos alihudumu katika michuano mikubwa na mechi za kirafiki. Alihudumu katika Kombe la Dunia mnamo mwaka 1998, 2002 na 2006; pia katika Copa America mara nne, Kombe la Shirikisho la FIFA mnamo mwaka 1997 na Michuano ya Olimpiki mwaka 1996.

Akiwa na Real Madrid, alijulikana na kupewa sifa ya kwamba akiwa upande wa kushoto anaweza kucheza mwenyewe namba tatu na 11, kwa maana ya kukaba na kushambulia. Kocha wa zamani wa Real Madrid, Vicente del Bosque, aliwahi kusema: “Ana uwezo mkubwa wa kulinda na kushambulia mwenyewe eneo lote la kushoto.”

Carlos aliichezea Los Blancos kwa misimu 11 ya mafanikio; alishinda mataji manne ya La Liga, na matatu ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Mnamo Aprili 2013, alitajwa na Gazeti la Marca la nchini Hispania, kuwa mmoja wa wachezaji 11 bora wa kigeni katika klabu ya Real Madrid kwenye historia ya miamba hiyo.