Mwili wa Marehemu Hassan Ali ukiwa chini kabla ya kuondolewa na Jeshi la Polisi Tanzania mnamo Novemba 14, 2024 katika eneo la Nelson Mandela, Pasua mjini Moshi. |
Mwanaume anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 40 amefariki dunia kwa kujinyonga katika mti eneo la Nelson Mandela mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro, kwa kile kinachosadikika kuwa ni kujinyonga kwa kamba za katani pembezoni mwa uwanja wa Nelson Mandela; Pasua mjini Moshi.
Tukio hilo ni la tatu katika eneo hilo la Pasua kwa mwaka huu
la watu kuchukua uamuzi mbaya wa kujinyonga kutokana na sababu mbalimbali.
Mashuhuda wa tukio hilo wameiambia EATV kuwa marehemu
alikutwa asubuhi ya Novemba 14, 2024 akiwa amelala chini baada ya tawi la mti
kukatika na kumbwaga chini huku wengine wakidai chanzo cha umauti ni kukata
tamaa ya maisha na mahusiano ya kimapenzi.
Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro lilifika eneo la tukio
baada ya wananchi kutoa taarifa kuhusu kukutwa kwa mwili huo katika eneo la
Nelson Mandela ambapo mwili wa marehemu ulihifadhiwa katika Hospitali ya KCMC
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro SACP Simon Maigwa alitoa wito kwa wananchi.
"Jeshi la Polisi linatoa rai kwa wananchi kutoa taarifa mapema kwenye taasisi zenye mamlaka ya kushughulikia migogoro ya ndoa ili kuepeusha misongo ya mawazo inayopelekea kutoa maamuzi magumu ikiwa ni pamoja na kusababisha mauaji na kujitoa uhai," alisema SACP Maigwa.
Hata hivyo baadhi ya wakazi mjini Moshi wametoa maoni ili kupata mwarobaini wa changamoto ya kuchukua maamuzi magumu kutokana na kuhisi
kuwa maisha yao hayana maana yoyote au hawaoni sababu ya kuendelea kuishi.
Suala la kujinyonga linaendelea kuwa changamoto kubwa katika
jamii nyingi, likihusisha masuala ya kiuchumi, kijamii, na kisaikolojia.
Credit to: Yesse Tunuka, Ombeni Mjema, Johnson Jabir; JAIZMELA