Mkurugenzi wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), Primus Kimaryo, amesisitiza umuhimu wa uanzishwaji wa matamasha ya kahawa katika kusaidia wakulima wa zao hilo kupata mbinu bora za kilimo.
Akizungumza katika uzinduzi wa Kahawa Festival 2024, mnamo Septemba 4, 2024 Kimaryo alieleza kuwa matukio haya ni fursa ya kipekee kwa wakulima kujifunza na kuboresha uzalishaji wao.
Kimaryo alisema kuwa
matamasha yanatoa jukwaa kwa wakulima kukutana na wataalamu wa kilimo, ambapo
wanaweza kupata mafunzo kuhusu mbinu za kisasa za kilimo, usimamizi wa
mashamba, na teknolojia mpya.
"Tunaamini kuwa elimu ni
msingi wa maendeleo. Wakulima wanapojifunza mbinu bora, wanakuwa na uwezo wa
kuongeza uzalishaji na kuboresha ubora wa kahawa yao," alifafanua.
Alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wakulima, serikali, na wadau wengine katika sekta ya kahawa. "Tunaweza kufanikisha mabadiliko makubwa kwa kushirikiana. Matamasha haya ni fursa ya kuungana na kujadili changamoto na fursa zinazokabili sekta ya kahawa," alisema Kimaryo.
Kimaryo aliongeza kuwa matamasha yanaweza kusaidia kuboresha soko la kahawa nchini.
"Kwa kutoa elimu na mafunzo, wakulima wataweza kuzalisha kahawa bora, ambayo itavutia wanunuzi na kuongeza thamani ya bidhaa zetu katika masoko ya ndani na nje," alisema.
“Uanzishwaji wa matamasha ya
kahawa ni hatua muhimu katika kusaidia wakulima kupata mbinu bora na kuboresha
uzalishaji wa kahawa nchini.
Kimaryo, alisisitiza kuwa
elimu na ushirikiano ni muhimu katika kuimarisha sekta ya kahawa na kuhakikisha
kuwa wakulima wanapata faida inayostahili kutokana na kazi zao.
Kwa upande wake, Mwenyekiti
wa Kahawa Festival, Denis Mahulu, alisema idadi ya watu wanaoshiriki kuonyesha
bidhaa zinazotokana na zao la kahawa inazidi kuongezeka kila mwaka ambapo
washiriki kutoka maeneo mbalimbali, wamekuwa wakishiriki kuonyesha ubunifu na
ubora katika bidhaa zao.
Mahulu alisema kwamba ongezeko la washiriki hao ni dalili nzuri ya ukuaji wa sekta ya kahawa, kupitia Tamasha la Kahawa Festival-2024, wakati tamasha hilo linaanzishwa mwaka 2019 washiri walikuwa 25 na kwa sasa washiriki wako zaidi ya 40, ambapo tamasha hilo, linatoa fursa kwa wakulima na wazalishaji wa kahawa kuungana, kubadilishana mawazo, na kujifunza mbinu bora za kilimo na usindikaji.
Mgeni rasmi wa ufunguzi wa
Kahawa Festival 2024 alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Moshi James Kaji ambaye
alisisitiza uanzishwaji wa mashindano ya michezo kama vile riadha ili
kuimarisha unywaji wa kahawa na kupanua wigo wa zao hilo kwa kila mdau nchini
na kimataifa.
Kauli Mbiu ya Kahawa Festival
2024 inasema; “Ushirikiano wa dau kwa Pamoja katika uendelezaji wa tasnia ya
Kahawa.”
CREDIT TO: Johnson Jabir, (JAIZMELA Correspondent.)
0 Comments:
Post a Comment