Saturday, August 31, 2024

Chuo cha Montessori, Ushirika wa Neema, Moshi chaadhimisha miaka 154 ya kuzaliwa

Maria Tecla Montessori, 1870-1952 (Picha na Mtandao/Luce)

 “Niliondoka Italia mnamo mwaka 1934, wakati ambao shule zote nilizoanzisha zikiwa zimefungwa, Niliishi uhamishoni barani Ulaya mpaka mwaka 1939 na baadaye nikaenda kuishi nchini India kwa miaka saba (7) kwa miaka mitano nilitiwa kizuizini kama adui wa Waitaliano, sikuweza kusafiri, lakini raia wa India walinijia siku moja na nikafanikiwa kuwafundisha walimu 1500.”

Maria Tecla Artemisia Montessori alikuwa akizungumza na vyombo vya habari nchini Italia akitokea India mnamo mwaka 1940.

Wanafunzi wa Chuo cha Montessori, Ushirika wa Neema mjini Moshi wakiwa na Mkuu wa Chuo hicho Sister Christine Nakey katika kuadhimisha miaka 154 tangu kuzaliwa kwa Dkt. Maria Montessori mnamo Tarehe 31 Agosti 2024. (Picha Na. JAIZMELA/Kija Kisena)

Agosti 31, 1870 katika mji wa Chiaravalle uliopo katika mkoa wa Marche nchini Italia alizaliwa mwanamke wa kwanza nchini humo kuwa daktari wa magonjwa ya watoto na magonjwa ya akili Maria Montessori.

Wakati akizaliwa katika mji huo hakuna aliyewahi kudhani kama siku moja Maria Montessori angekuwa miongoni mwa watu mashuhuri waliowahi kuwepo ulimwenguni na kutoa msaada mkubwa sana hadi sasa.

Katika ugunduzi wake alibaini kuwa watoto waliovia akili wanaweza kufunzwa kwa kutumia vifaa vya kuchezea wanavyovipenda. Aliamini kuwa tatizo la kuvia akili ni la kielimu na sio la tiba.

Maria Montessori aliamini kuwa elimu ya mtoto ni lazima ianze mapema sana kwa sababu umri wa mtoto  kati ya kuzaliwa  hadi miaka sita ni muhimu sana kwa ujenzi wa haiba yake.

Ili mtoto aweze kujifunza kwa ufanisi zaidi ni muhimu kwa mzazi au mwalimu kutumia michezo na vitendo vinginevyo katika kufundisha,hii itamsaidia mtoto katika kujifunza kujifunzia stadi mbalimbali za utendaji .

Maria Montessori   anajulikana sana kwa kuwa mtu aliyeanzisha njia ya kuwafundisha watoto wadogo.

Maria Monterssori ameacha alama duniani ikiwamo mjini Moshi mkoani Kilimanjaro ambako Chuo cha Mafunzo ya Ualimu Montessori Ushirika wa Neema kilichopo Manispaa ya Moshi, kimeadhimisha miaka 154, tangu kuzaliwa kwa Dkt. Maria Montessori.

Akizungumza katika maadhimisho hayo Mkuu wa Chuo hicho Sister Christine Nakey, amewataka wazazi na walezi  kuwajali watoto wenye changamoto mbalimbali za kimaisha ikiwemo wenye ulemavu kutokana na ukweli kuwa na wao wana nafasi katika kuchangia maendeleo ya nchi.

Wito umetolewa kwa Wizara ya Elimu nchini Tanzania kuwa na kitengo ambacho kitatumia mitaala ya mwanzilishi Maria Montessori katika kujifunza.

Kwa upande wao wanafunzi wanaosoma katika Chuo hicho wamesema elimu ya Montessori inaenda sambamba na vitendo hivyo kumjenga mwanafunzi kujiamini na kupambana na mazingira yanayomkabili hata baada ya kuhitimu mafunzo.

Maria Montessori atazidi kukumbukwa na kuenziwa kwani alipendekeza mwalimu atumie vifaa vingi katika ufundishaji, vifaa hivyo viwe ni vile vinavyokuza tabia ya udadisi na ugunduzi,vinavyompa nafasi ya utendaji na vinavyomwezesha kufanya majarabio,kutatua vikwazo,ujasiri,kuuliza na kujibu maswali,kupenda kufaulu, kujiendeleza na kumpa msukumo wa kujitegemea katika utendaji.

Alifariki dunia mnamo Mei 6, 1952 magharibi mwa Uholanzi katika mji wa Noordwijk  akiwa na umri wa miaka 81 na alizikwa huko huko Noordwijk.










0 Comments:

Post a Comment