Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro Nurdin Babu muda mchache baada ya ufunguzi wa mkutano wa 26 wa KCBL uliopitisha mageuzi ya benki hiyo na kuwa Beki ya Ushirika Tanzania (CBT). |
Watanzania nchini wametakiwa kuitunza Benki ya Ushirika Tanzania (CBT) kwa kujiepusha na mikopo isiyo na tija maarufu kama mikopo kausha damu.
Akizungumza kwenye mkutano wa 26 wa Benki ya Ushirika Kilimanjaro, uliobadilisha benki hiyo na kuwa Benki ya Ushirika Tanzania Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu alisema KCBL imejitahidi kufanya mageuzi makubwa ya kimfumo kwa manufaa ya watanzania.
“Benki ya KCBL imefanya mageuzi makubwa katika kipindi hiki kifupi tangu kuanzishwa kwake, sasa inatoa bidhaa lukuki ya mikopo ya biashara, kilimo na pembejeo za kilimo na uzalishaji wa kahawa, njoooni wekezeni hapa,” alisema Babu.
Aidha mkuu huyo wa mkoa kwa niaba ya Waziri wa Kilimo Hussein Bashe aliongeza kuwa taifa kwa ujumla lina matumaini mapya kwa wanaushirika hivyo sio vizuri kujiingiza katika mikopo itakayokuwa na hasara. “Taasisi, makampuni na watu binafsi wanahamasishwa kununua na kumiliki hisa, kiwango cha chini ni hisa 400 ambazo ni sawa na shiligi laki mbili tu,” alisema Babu.
Kwa upande wao wanahisa walitoa wito kwa watanzania wanaopenda kujichukulia mikopo kausha damu waachane nayo kwani inaweza kuwapa msongo wa mawazo
Awali Katibu Tawala wa Mkoa Tison Nzunda alisema taasisi mbalimbali zinapaswa kuinga mkono CBT ili iweze kuimarika kiuchumi ili kutoa huduma bora kwa wanachama wao. “Kwa muda mrefu vyama vya vya uushirika viliendelea kupata changamoto mbalimbali lakini kazi ya serikali ni kuimarisha viongozi wa vya ushirika,” alisema Nzunda.