Tuesday, April 25, 2017

Wafanyakazi Wagonjwa wa muda mrefu Rufaa Mbeya wapata msaada

Wanamtandao walipozuru mojawapo ya nyumba ya Mfanyakazi wa Hospitali ya Kanda Rufaa Mbeya kumjulia hali baada ya utaratibu wa kuwatembelea kuanzishwa na Mkurugenzi wa Hospitali hiyo Dkt. Godlove Mbwanji.
Katika kuhakikisha kuwa wagonjwa wa muda mrefu wanapata faraja, Umoja wa wanamtandao wa Hospitali ya Kanda ya Rufaa Mbeya umeanzisha utaratibu wa kuwatembelea wagonjwa hao kuwajulia hali kila mwezi.
Dkt. Godlove Mbwanji ambaye ni mwasisi wa mpango huo akiungana na wanamtandao hao wamewatembelea wagonjwa ambao ni wafanyakazi hospitalini hapo lakini kutokana na maradhi kuwashika kwa muda mrefu wameshindwa kufika maeneo ya kazi.
Wanamtandao hao waliopo kwenye mitandao ya kijamii waliunga mkono wazo la mwasisi huyo na kulifanyia kazi kwa vitendo ambapo walikutana majuma kadhaa yaliyopita na kuazimia kuwa na utaratibu huo ambao watakuwa wakipeleka vitu mbalimbali vya kuwatia moyo ikiwamo sukari, chumvi, sabuni na matunda.
Miongoni mwa wagonjwa wa kwanza kukutwa na utaratibu huo ni pamoja na mama Kaseko, Mr, Katembo, Mama Mwankotwa na Mama Pondo.
Kwa upande wa wagonjwa hao walikiri kushtushwa na ujio wa wanamtandao hao lililongozwa na Mkurugenzi wa Hospitali hiyo Dkt. Mbwanji kwa kuendelea kuwajali na kuwathamini hali inayoonyesha hata walipokuwepo kazini hospitali hapo walikuwa wakiishi kwa upendo.
Kwa upande wake Dkt. Mbwanji alisema ni mara chache kuona mgonjwa akipewa kipaumbele hususani kwa wale wanaougua muda mrefu lakini alisukumwa kuanzisha utaratibu huo wa kuwatembelea wafanyakazi wa hospitali hiyo ambao ni wagonjwa wa muda mrefu na kwamba mpango huo ni endelevu.

Wanamtandao hao walisisitiza kuwa mpango ulianzishwa na Dkt. Mbwanji ni mfano kwa taasisi nyingine namna ya kuwajali wafanyakazi wao katika raha na shida.
Dkt. Mbwanji na mojawapo ya mgonjwa ambaye ni mfanyakazi wa Hospitali ya kanda Rufaa Mbeya hivi karibuni alipomtembelea kumjulia hali.

0 Comments:

Post a Comment