John Cheyo |
Mbunge wa zamani Bariadi Mashariki John Cheyo amesema ipo haja kwa
Serikali kuboresha baadhi ya mambo ambayo yanaonekana kuwa ni kero kwa
jamii kwenye maeneo ya Bara na Visiwani Zanzibar ili kuimarisha Muungano.
Cheyo amesema katika kipindi cha miaka 53 ya muungano Serikali imefanya
mambo mengi mazuri ingawa yanatakiwa kuimarishwa zaidi.
Cheyo amesema Muungano uliopo unapaswa kuwa wa kiundugu zaidi huku
akiwataka wananchi wa Tanzangika na Zanzibar kusaidiana kwenye masuala
mbalimbali bila kujali itikadi za kisiasa wala makabila yao.
Mwaka huu maadhimisho ya Muungano yatafanyika mjini Dodoma ambako sherehe
zitafanyika Nyerere Square mjini humo ambapo jana Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
alikagua maandalizi ya sherehe hizo hapo kesho.
Mkataba wa Muungano ulitiwa saini na Mwalimu Julius Nyerere na Abeid
Amani Karume, Aprili 22, 1964, Zanzibar.
Ulithibitishwa na Bunge la Tanganyika na Baraza la Mapinduzi Aprili 26,
1964, na Aprili 27, 1964 viongozi hao walikutana katika ukumbi wa Karimjee,
jijini Dar es Dalaam kubadilishana hati za Muungano.
Sheria za Muungano ilitamka kwamba, Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya
Watu wa Zanzibar zililazimika, kuwa dola
ya Jamhuri kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, jina
ambalo lilibadilishwa Oktoba 28, 1964 na kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kwa kupitia sheria ya Jamhuri ya Muungano, sheria namba 61, ya mwaka 1964.
Kwa muda mrefu sasa kumekuwa na mijadala mbalimbali kuhusiana na muundo
wa Muungano, baadhi wakitaka uwe wa zaidi ya serikali mbili, wengine serikali
moja, wapo wanaotaka Tanganyika iwe kivyake na Zanzibar kivyake.
0 Comments:
Post a Comment