Tuesday, October 25, 2016
Kizimbani kwa wizi wa magodoro Aga Khan
NA JABIR JOHNSON
WATU wawili wamepandishwa kortini katika mahakama ya Wilaya ya
Ilala jijini Dar es Salaam kujibu mashtaka kwa kosa la wizi wa vitu mbalimbali
vya Hospitali ya Aga Khan yakiwamo magodoro 20.
Wakisomewa mashtaka yao jana na Mwendesha Mashtaka Grace Mwanga
mbele ya Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo ilidaiwa washtakiwa Jimmy Rupia (47) na
James Makoye (37) walitenda makosa mawili eneo la Aga Khan Julai 20 mwaka huu.
Mwendesha mashtaka alidai kosa la kwanza lilikuwa ni kuvunja ghala
la vifaa vya hospitali wakiwa na nia ya kuiba kinyume na Kifungu cha Sheria Na.
296 (a) na kosa la pili ni kuiba magodoro 20, mahema matatu na mashine ya
kubembea kinyume na Kifungu cha Sheria Na. 258 na 265.
Aliongeza kuwa mali zote zilizoibwa zilikuwa na jumla ya thamani
ya Sh. 10,900,000 mali ya hospitali hiyo.
Washtakiwa wote wawili walikana mashtaka yao na kutakiwa kutimiza
masharti ya dhamana kwa kutoa ahadi ya Sh. 3,000,000 na wadhamini wawili
wanaotambulika; hata hivyo walikosa wadhamini na kurudishwa rumande.
Kesi hiyo itatajwa tena Novemba 7
mwaka huu.
Kizimbani kwa kubaka
ILALA, DAR ES
SALAAM
MKAZI wa Majohe Plaza jijini Dar es Salaam Ally Ramadhani
(23) amepandishwa kizimbani kwa kosa la kumbaka msichana wa miaka 17.
Akisomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Flora Mjaya,
mwendesha mashtaka Ashura Mnzava alidai Mei 5 mwaka huu eneo la Kinyerezi
mshtakiwa alitenda kosa hilo huku akijua ni kinyume cha sheria.
Mnzava aliongeza mshtakiwa alikiuka Kifungu cha Sheria Na.
130(1)(2)(e) na 131(1) sura ya 16 kilichofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Mshtakiwa alikana kutenda kosa hilo.
Hakimu alisema dhamana kwa mshtakiwa ipo wazi endapo atakuwa
na wadhamini wawili wa kuaminika na ahadi ya Sh. 3,000,000; hata hivyo
alishindwa kutimiza masharti ya dhamana.
Kesi itatajwa tena Novemba 7 mwaka huu.
Monday, October 24, 2016
Dk. Mashinji Oktoba 23
Alichokisema Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA), Dk.Vincent Mashinji baada ya uchaguzi wa meya wa Kinondoni,
Oktoba 23, 2016 kuhusu kufungua kesi mahakamani.
“Chadema hakitakuwa
chama cha kulalamika…hatutakuwa walalamishi tena tutakusanya ushahidi…Hii sio
Tanzania tulioitarajia. Ilikuwa ni wanasiasa sasa ni zamu ya wanahabari.”
“CHADEMA ilianzisha
Operesheni Umoja wa Kupambana Udikteta Tanzania (UKUTA), hatuwezi kukaa kimya
tena, Nyerere alikataza Vijana kuwa wanyonge na waoga, hakutaka Taifa la watu
waoga, na sisi tunasema mwisho wa uoga umekwisha, tutakwenda Mahakamani kwa sababu
kilichotokea kwenye Uchaguzi wa Meya wa Manispaa Kinondoni ni uhuni, kanuni na
taratibu zinavunjwa waziwazi.”
“Wanafahamu kwamba vyombo vya habari vya
Kimataifa hawawezi kuvibana. Sisi tunakwenda mahakamani pili ili kuondoa
ukakasi huu. Watumishi wa umma hamna amani tena tutapigania Katiba ya Wananchi.”
Hata hivyo Mashinji alieleza tija ya kufungua kesi
mahakamani kutokana na kwamba hadi sasa wamefungua kesi nyingi.
“Kesi nyingi
tumefanikiwa…unapofungua kesi mahakamani inaonyesha kuwa unaheshimu utawala wa
sheria, pili unaweka msingi wa siku zijazo watu watakuja kujua wenzetu kumbe
walifanya hivi; tatu unapokuwa unatafuta tafsiri ya mahakama unakuwa huru zaidi
katika maamuzi yako binafsi na mwisho ni kwa tija ya wananchi.”
Sunday, October 23, 2016
Sita kortini kwa unyang’anyi
NA MWANDISHI WETU
WATU sita wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya
Ilala jijini Dar es Salaam kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha.
Mbele ya Hakimu Mkazi John Msafiri, Mwendesha Mashtaka
Sylivia Mitanto alidai Ramadhani Athumani (18), Jabil Muhando (17), Khalifan
Humba (16), Nurdin Muhando (17), Abdul Omary (15) na Hamad Mohamed (15)
walitenda makosa mawili ya unyanganyi wa kutumia silaha Septemba 13 mwaka huu
eneo la Vingunguti kwa Simba.
Mitanto aliongeza washtakiwa hao walii simu ta kiganjani
aina ya Tecno M3 yenye thamani ya Sh. 130,000; Nguo za Mazoezi zenye thamani ya
Sh. 60,000; mkanda mweusi wenye thamani ya Sh. 150,000 na fedha taslimu Sh. 30,000 vyote vikiwa na thamani ya Sh.
370,000 mali ya Laika Mboya.
Katika kosa la pili washtakiwa walimwibia Tabu Juma simu
aina ya Samsung yenye thamani ya Sh. 350,000 na katika makosa yote kabla na
baada ya kuiba waliwatishia kwa panga ili kujipatia mali hizo.
Washtakiwa walikana mashtaka yao huku wakishindwa kutimiza
masharti ya dhamana.
Kesi itatajwa tena Novemba 2 mwaka huu.Friday, October 21, 2016
Dereva wa daladala jela miaka 7
ILALA, DAR ES SALAAM
MAHAKAMA ya Wilaya Ilala jijini Dar es Salaam imemhukumu dereva wa
daladala mkazi wa Ubungo wa External Mohamed Amir Ramadhani kwa wizi wa Sh.
6,700,000.
Akisoma hukumu hiyo jana Hakimu Mkazi Catherine Kiyoja alisema ushahidi
wa mahakama umethibitisha bila shaka yoyote kuwa mnamo Mei 5, 2015 eneo la
Gongo la Mboto aliiba begi lililokuwa na fedha taslimu milioni sita na laki
saba.
Kiyoja aliongeza kuwa Mohamed alifanya wizi huo kwa kuvunja kioo cha
gari Na. T768 CJX aina ya Toyota Harrier mali ya Ally Ngaboli kinyume na
Kifungu cha Sheria Na. 258 na 265 cha Kanuni ya Adhabu
Kiyoja alisema shahidi wa kwanza akiwa Gongo la Mboto eneo la Majumbasita
alipaki gari lake ili kununua matunda aliporudi alikuta wamevunja kioo.
Hakimu alisema mashahidi wengine waliiambia mahakama kuwa walishuhudia
wizi huo na kumsaidia shahidi namba moja kumkamata mwizi kisha kumfikisha kituo
cha polisi kwa hatua zaidi.
Awali mwendesha mashtaka Florida Wenceslaus aliiomba mahakama kuwa
mshtakiwa apewe adhabu kali ili iwe fundisho kutokana na kutokuwa na historia
ya makosa ya jinai.
Akijitetea Mohamed aliiomba mahakama impunguzie adhabu kutokana na kuwa
ni mgonjwa wa kifafa, familia yake inamtegemea wakiwamo watoto anaowasomesha na
kuwalipia ada pia baba yake ni mzee na mama yake ni mgonjwa wa shinikizo la
damu na kisukari.
Hata hivyo kujitetea kwake hakumzuia Hakimu kumtupa jela miaka saba.
Thursday, October 20, 2016
‘Scorpion’ afunguliwa upya mashtaka, abadilishiwa hakimu
NA
JABIR JOHNSON
Salum Njewete 'Scorpion' akitolewa nje ya ukumbi wa mahakama ya Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam jana chini ya ulinzi mkali baada ya kusomewa mashtaka upya. |
MSHTAKIWA
wa kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha Salum Njwete (34) ‘Scorpion’ amefutiwa shtaka lake la awali na Mahakama ya
Wilaya Ilala, jijini Dar es Salaam jana kisha kesi yake kuanza upya.
Hata
hivyo kuanza kwa shtaka lake jipya kumeenda sanjari na kubadilishwa hakimu wa
kuisikiliza kesi hiyo.
Mwendesha
Mashtaka Munde Kalombola mbele ya Hakimu Mkazi Adelf Sachore aliiomba
mahakamani kuwa upande wa mashtaka hawezi kuendelea kusikiliza kesi hiyo kwa
mujibu wa kifungu cha Sheria Na. 91(1) cha Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
Hakimu
aliridhia ombi la mwendesha mashtaka kufuta shtaka lililokuwa likimkabili
Scorpion.
Shtaka
jipya ambalo Scorpion anashtakiwa nalo ni unyang’anyi wa kutumia silaha
alilolitenda Septemba 6 mwaka huu Buguruni Shell kisha kumchoma na kisu
mlalamikaji Said Ally Mrisho machoni, mabegani na tumboni.
Awali
Mwendesha Mashtaka Chesensi Gavyole mbele ya Hakimu Mkazi Flora Haule alidai
mahakamani hapo kuwa mshtakiwa alimpora mlalamikaji ambaye hakuwepo mahakamani
hapo vitu vya thamani na fedha taslimu vyote vikiwa na jumla ya Sh. 476,000.
Mshtakiwa
alikana kuhusika na kosa hilo.
Hakimu
alisema kwa mujibu wa Kifungu cha Sheria Na. 148(5)(a)(i) cha Mwenendo wa
Makosa ya Jinai Sura ya 20 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002, mshtakiwa
hawezi kupata dhamana hivyo atarudishwa mahabusu.
Ikumbukwe
Septemba 23 mwaka huu, Scorpion alipandishwa mahakamani hapo na kufunguliwa
shtaka la unyang’anyi wa kutumia silaha chini ya kifungu cha Sheria Na. 287A
cha makosa ya jinai.
Ilidaiwa
mahakamani hapo kuwa Scorpion aliyejipatia umaarufu ‘Mtoboa Macho’ mnamo
Septemba 6 mwaka huu maeneo ya Buguruni Shell jijini hapa alimvamia na kumpora
mali na fedha taslimu muathirika Said Ally Mrisho kisha kumchoma na kisu katika
macho, mabegani na tumboni huku akijua kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Kesi
hiyo ilikuwa chini ya Hakimu Mkazi Adelf Sanchore na Mwendesha Mashtaka Munde
Kalombola ambao wameisimamia hadi Oktoba 19 mwaka huu.
HALI ILIVYOKUWA MAHAKAMANI
Umati
wa watu walikusanyika tangu asubuhi kusubiri kusikilizwa kwa kesi hiyo ambapo
Karandinga la Magereza lilitinga mahakama hapo saa 2:09.
Scorpion
alishuka kutoka kwenye karandinga hilo saa 2:19 asubuhi akiwa katika kanzu
nyeupe na barghashia yenye rangi nyeupe, njano na bluu.
Kilichowastaajabisha
watazamaji wakati anashuka alikuwa akitabasamu chini ya ulinzi
mkali.
Baadhi
ya watazamaji walifura kwa hasira, wengine wakiendeleza minong’ono ya kulaani
kitendo hicho.
Saa
3:10 asubuhi kesi hiyo ilitua mezani Hakimu Mkazi Adelf
Sachore chini ya Mwendesha Mashtaka Munde Kalombola.
Ilitumia
dakika tano tu kusikilizwa hadi kufutwa kwake.
Jambo
la kushangaza lilikuwa pale wakati mwendesha mashtaka alipokuwa akitamka
Kifungu cha Sheria Na. 91(1), wingu lenye manyunyu ya mvua lilishuka
kwa ghafla kisha umati wa watu uliokuwa madirisha kufuatilia mwenendo wa kesi
hiyo kutafuta mahali pa kujisitiri.
Hata
hivyo alipomaliza kusoma na Hakimu Sachore kuridhia kufutwa kwa kesi hiyo
manyunyu hayo yalikata ghafla na miale ya jua ikaendelea kupenyeza katika miili
ya watu.
Baada
ya kesi hiyo kufutwa Scorpion alirudishwa mahabusu kisha majira ya saa 6:19
mchana kukiwa na jua kali alipandishwa mbele ya Hakimu Mkazi Flora Haule chini
ya Mwendesha Mashtaka Chesensi Gavyole kusomewa mashtaka mapya.
Kabla
ya kusomewa mashtaka hayo Scorpion alifunguliwa pingu alizofungwa mikononi
mwake na Askari Polisi huku umati mkubwa ukifuatilia kwa karibu.
Ilimchukua
dakika nne tu hakimu kuisikiliza kesi hiyo, kisha Scorpion akaondolewa mbele ya
korti na kurudishwa mahabusu.
Wednesday, October 19, 2016
‘Panya Road’ afufuka mochwari
TEMEKE, DAR ES
SALAAM
MKAZI wa Buza wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam Isaack
Ernest (16), miongoni mwa wahalifu wa kundi la ‘Panya Road’ amefufuka katika
Chumba cha Kuhifadhi Maiti cha Hospitali ya Temeke siku chache baada ya
kufikishwa hapo kama maiti.
Tukio hilo la aina yake lililotokea siku chache baada ya
kijana huyo kufikishwa hospitalini hapo kutokana na kupata kipigo kutoka kwa
wananchi wenye hasira kali baada ya kuhusika matukio ya kuiba, kujeruhi na kuharibu
mali.
Oktoba 15 mwaka huu katika maeneo ya Sabasaba, Mbagala
vijana sita walikamatwa na kushambuliwa na wananchi kwa tuhuma za kupora watu
waliokuwa wakipita maeneo hayo.
Kikundi hicho cha vijana kilichojitambulisha kwa jina la
Taifa Jipya kilianza kufanya uhalifu huo baada ya kumalizika kwa Tamasha la
Kuinua Vipaji vya Muziki liliandaliwa na Clouds FM katika viwanja vya Zakheim
jijini hapa.
Katika tukio hilo mkazi wa Yombo na mwanafunzi wa Shule ya
Sekondari ya Nuruakim Kelvin Nyambocha (14), aliuawa kwa kuchomwa moto huku
watano wakijeruhiwa vibaya kutokana na kipigo hicho.
Aidha miongoni mwao mkazi wa Kilungule Seleman Hamis (16),
alifariki dunia akiwa katika chumba cha upasuaji mdogo katika Hospitali ya
Wilaya ya Temeke huku mkazi wa Buza kwa Lugenge ambaye ni fundi gereji Faraji
Suleiman (19) alihamishiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu
zaidi ambako yupo hadi sasa.
Akisimulia mkasa huo jana jijini hapa katika Kituo cha
Polisi cha Chang’ombe Isaack (miongoni mwa waliopokea kichapo na kudhaniwa kuwa
amekufa kisha kupelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya
Wilaya ya Temeke) akiwa mikononi mwa polisi jinsi alivyoshawishiwa kujiunga na ‘Panya
Road’ hadi kukutwa na masahibu hayo
anasimulia kuhusu namna ‘Panya Road’ walivyomshawishi
kujiunga nao.
“Mimi nakaa Buza, Jumamosi tulikuwa Zakheim kulikuwa na shoo
tulikwenda na wenzangu wakati wa kuondoka, wakaniambia kama kula tunakula mimi
nikawaambiaje, kula mi sijiwezi kama kula kuleni,” alisema Isaack kuongeza
“Wakaanza kuniambia kuwa mimi nina under fear (ninaogopa),
na wakasema na tukila hatukugei mali nikwaambia kama kula kuleni mi sijiwezi…mi
nikapita njia nyingine na wenyewe kivyao, kila walipopita walikuwa wanaiba.”
Pia kijana huyo mwanafunzi wa kidato cha tatu katika
sekondari ya Lumo jijini hapa anaendelea kusema, “Walivyopita njia nyingine
mmoja wakamwitia kelele za mwizi, akapigwa asa mi nikawa nipo ng’ambo nyingine,
nikamwona mwingine wengine wakavuka ng’ambo nilikuwapo mimi na kutangulia
wengine wakaangukia bondeni, sasa nikaonekana mimi wakaniitia kelele za mwizi
kustuka nikajikuta nipo mochwari.”
Isaack anahitimisha kwa kusema, “Mpaka dakika hii nipo
hapa…sitarudia vitendo vya wizi kwani nilishawakataa na kwasababu mimi bado
mwanafunzi…bado napenda maisha yangu.”
Kwa upande wake mzazi wa Isaack ambaye ni mjumbe wa Serikali
ya Mtaa wa Buza anasema hakuwahi kumuona kijana wake akijihusisha na masuala ya
wizi kwani katika mtaa wao wamekuwa wakishirikiana na Jeshi la Polisi
kuimarisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao.
JESHI LA POLISI
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi mkoa wa
Temeke Gilles Muroto alisema kijana alizindukia mochwari yupo mikononi mwao na
baada ya mahojiano ya muda mrefu amewasaidia kujua mtandao wa kundi lao.
“Kijana huyu ametusaidia kuwapata vijana wengine kumi na
tunao tunatarajia kuwapandisha mahakamani kujibu mashtaka yao,” alisema Muroto.
Aidha Muroto alisema katika msako walioufanya wamewakamata
vijana 16 wakiwa na mapanga na bendera ya kundi lao iliyochorwa na kuandikwa ‘Taifa
Jipya…Makali yanaendelea…”
Hata hivyo kamishna huyo alisema wamewaita wazazi wa watoto
hao na wamefika katika makao makuu ya Kipolisi Temeke jana ambao watapandishwa
mahakamani muda wowote wiki hii kutokana na kukiuka sheria ya watoto ya mwaka
2009 kifungu cha saba hadi tisa.
Aidha Muroto alisema kifungu cha 14 cha sheria hiyo kinatoa
adhabu kwa mzazi atakayeshindwa kutekeleza hayo atafikishwa mahakamani na
akitiwa hatiani atapewa adhabu ya kifungo cha miezi sita jela au faini ya Sh.
Milioni 5.
Imeandikwa katika Gazeti la Tanzania Daima ISSN 0856 9762 Toleo Na. 4337 Jumatano Oktoba 19, 2016 Uk. 2
‘Scorpion’ kupandishwa korti leo
NA MWANDISHI WETU
Salum Njewete |
MSHTAKIWA wa unyang’anyi wa kutumia silaha Salum Njwete (34) maarufu
Scorpion anatarajiwa kupandishwa tena katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala jijini
Dar es Salaam leo.
Scorpion anapandishwa kortini kwa mara ya tatu baada ya kesi yake
kuahirishwa Oktoba 7 mwaka huu baada ya upande wa mashtaka kuiambia mahakama upelelezi wa kesi hiyo bado
haujakamilika.
Awali ilidaiwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashtaka wa serikali Munde
Kalombola mbele ya Hakimu Adelf Sachore kuwa Septemba 6 mwaka huu katika maeneo
ya Buguruni Shell jijini Dar es Salaam mshtakiwa alimvamia na kumchoma visu
kwenye macho, tumboni na mabegani Said Mrisho kinyume na Kifungu cha Sheria
Na.287A sura ya 16 ya makosa ya jinai.
Mwendesha mashtaka alidai mshtakiwa alimpora mkufu wa fedha gramu 38
wenye thamani ya Sh. 60,000; kidani cha mkononi chenye thamani ya Sh. 85,000 na
fedha taslimu Sh. 331,000.
Kesi hiyo ilitajwa kwa mara ya kwanza Septemba 23 mwaka huu.
Imeandikwa katika Gazeti la Tanzania Daima ISSN 0856 9762 Toleo Na. 4337 Jumatano Oktoba 19, 2016 Uk. 6
Imeandikwa katika Gazeti la Tanzania Daima ISSN 0856 9762 Toleo Na. 4337 Jumatano Oktoba 19, 2016 Uk. 6
Tuesday, October 18, 2016
Jela miaka 30 kwa kubaka mlemavu
ILALA, DAR ES SALAAM
MAHAKAMA ya Wilaya Ilala jijini hapa imemhukumu kifungo cha miaka 30
jela mkazi wa Pugu Bangulo Mathayo Mtanga (20) kwa kosa la kumbaka binti wa
miaka 14.
Akisoma hukumu hiyo jana, Hakimu Mkazi Florah Haule alisema kesi hiyo
ilifika mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Julai 21, 2015 na mshtakiwa alitenda
kosa hilo Mei 28, 2015 eneo la Bangulo kwa msichana huyo ambaye ni bubu na
kiziwi.
Aidha Hakimu aliongeza kusema ushahidi wa maandishi aliokiri katika
mahojiano yake na Polisi baada ya kukamatwa, mashahidi wanne na PF3
viliithibitishia mahakama pasipo shaka kuwa mshtakiwa alitenda kosa.
Awali Mwendesha Mashtaka Chesensi Gavyole alidai mahakamani hapo kuwa,
mshtakiwa hana rekodi ya makosa ya jinai
hivyo adhabu kali itolewe kwa kitendo alichokifanya.
Aidha Agosti 11 mwaka huu mshtakiwa alidai katika utetezi wake kuwa
mama wa mlalamikaji ni jirani yake na kwamba muathirika aliwahi kumkuta
chumbani kwake na akamuuliza alichokifuata kuwa ametumwa na mama yake hela,
akamtaka aondoke na iwe mwisho.
Mshtakiwa aliongeza haikuishia hapo baada ya majuma mawili muathirika
alimkuta tena chumbani alipomwamuru atoke alianza kulia na siku moja iliyofuata
akiwa kazini alifuatwa na polisi na kuambiwa kuwa amebaka.
Akiwa kituo cha polisi aliambiwa atoe laki tano ili kumaliza kesi hiyo
lakini hakuwa nayo wakamtaka laki mbili lakini nayo hakuwa nayo hadi kufikia
anahukumiwa hakuweza kutoa chochote.
Monday, October 17, 2016
Shahidi wa tukio la wizi Tabata Bima asimulia
ILALA, DAR ES SALAAM
SHAHIDI namba moja wa tukio la unyang’anyi wa kutumia silaha
lililotokea Tabata Bima jijini Dar es Salaam Antimi Kimati ameiambia Mahakama ya
Wilaya ya Ilala kuwa alimwona mtuhumiwa namba moja Amir Mohamed ‘Songambele’
akiwa na bunduki siku ya tukio.
Kesi hiyo ilifika mahakamani hapo Aprili 21 mwaka huu na kufunguliwa
jalada CC. 88/2016
Washtakiwa wanne Songambele (52), Juma Kassim Mwishehe (50), Hassan
Seleman Said (45) na Denis Charles
Chacha (32) walipandishwa kortini kujibu mashtaka yanayowakabili.
Kesi hiyo inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Catherine Kiyoja ilianza kwa
Mwendesha Mashtaka Florida Wenceslaus kuiomba mahakama kuanza kusikiliza
ushahidi wa unyang’anyi wa vocha zenye thamani ya laki tatu (300,000) na fedha taslimu milioni mbili
na laki nane (2,800,000) mali ya Matola Asenga katika tukio lililotokea Januari
31 mwaka huu.
Pia Mwendesha Mashtaka aliiomba mahakama kupokea vithibitisho ambavyo
ni vitambulisho na maandishi ya awali ya kukiri kwao kutenda tukio hilo
walipohojiwa na polisi.
Baada ya kuapa kuwa atasema kweli kuhusu tukio hilo, Hakimu alimtaka
shahidi huyo kuanza kutoa ushahidi wake.
Shahidi huyo aliiambia mahakama kuwa wakati tukio lilipokuwa likitokea
alikuwa ni mfanyakazi wa Grocery iitwayo Container Pub iliyopo Tabata Bima.
Akiwa na wenzake katika kontena akiendelea kupanga vinywaji kwenye
friji ghafla alisikia mlio wa risasi, alipoangalia nje, watu wote walikuwa
chini ya ulinzi mmoja tu akiwa amesimama na bunduki.
Antimi alidai kwasababu taa zilikuwa zikiwaka aliiona sura ya
aliyeshika bunduki, alipoinua uso wake walitazamana uso kwa uso ndipo
aliponyooshewa mtutu wa bunduki na kupiga risasi aliyoikwepa na kuishia kutoboa
TV.
Alipodondoka Antimi alidai alitembelea magoti na kupita kwa kutumia
mlango wa nyuma ambako alijificha.
Hata hivyo Machi 7 mwaka huu, aliitwa na Mkuu wa Kituo cha Polisi
Tabata ili kuwatambua watuhumiwa wa ujambazi kama kuna miongoni mwao
aliyehusika na tukio la Januari 31 mwaka huu, ndipo alipomtambua mtuhumiwa
namba moja wa kesi hiyo ya unyang’anyi.
Kesi hiyo itasikilizwa tena Oktoba 31 mwaka huu ambapo inatarajiwa
kuendelea kusikiliza ushahidi.
Thursday, October 13, 2016
Dk. Didas Masaburi is no more
CHANIKA, DAR ES SALAAM
Meya wa zamani wa Jiji
la Dar es Salaam, Dk. Didas Masaburi amefikwa na umauti jana majira ya saa tatu
na nusu usiku katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alipokuwa amelazwa.
Taarifa za kifo chake
zimethibitishwa na ndugu yake, Dk. Makongoro Mahanga ambaye alieleza kuwa
familia ipo katika taratibu za awali za msiba huo na kwamba leo watatoa taarifa
rasmi na taratibu nyingine.
“Taarifa za kifo cha
Dk. Masaburi ni za kweli ingawa sijaenda hospitali, ninafanya mawasiliano na
familia lakini taarifa kamili kuhusu msiba zitakuwa zikitolewa na msemaji wa
familia ambaye tutamteua usiku huu, na kesho (leo) tutaeleza kiundani,” Alisema
Dk. Mahanga jana usiku.
Kwa upande wake Diwani
wa Kata ya Mwananyamala, Songoro Mnyonge (CCM) alisema kifo cha mwanasiasa huyo
ni pigo kwa chama pamoja na wakazi wa Dar es Salaam.
“…alikuwa Muhimbili
kwa siku kama tano pale ICU…tunamuombea mwenzetu ambaye ametangulia mbele ya
haki,” liliandika gazeti la Mtanzania ISSN 0856 5679 Toleo Na. 8334 Uk. 3
Marehemu pia aliwahi
kuwa Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA).
Aidha asubuhi ya leo
Ikulu ya Rais John Magufuli imetuma salamu za rambirambi kwa wafiwa.
Masaburi atakumbukwa
kauli tata kwani Agosti 6, 2011 aliingia kwenye malumbano na wabunge wa jiji la
Dar es Salaam ambao walimtaka ajiuzulu wadhifa wake wa Umeya kutokana na
kukiuka taratibu katika uuzwaji wa Shirika la Usafir Dar es Salaam (UDA)
Kutokana na hali hiyo
Dk. Masaburi kama wengi walivyokuwa wakimfahamu alijibu mapigo dhidi ya wabunge
hao ambapo alisema baadhi yao wanashindwa kufikiria kwa kutumia vichwa na
badala yake wanafikiri kwa kutumia ‘makalio’.
Muuza maji jela kwa kuiba mti
NA
MWANDISHI WETU
MAHAKAMA ya Mwanzo ya Ilala imemhukumu Muuza maji mkazi wa
Keko jijini Dar es Salaam Emmanuel Issa (38) kifungo cha miezi minane jela kwa
kosa la kuiba miti 12 aina ya mchikichi.
Akisoma hukumu hiyo Hakimu Asha Mpunga alisema mshtakiwa
alitenda kosa hilo Agosti 22 mwaka huu katika mtaa wa Ohio kwenye Hoteli ya
Serena.
Aidha Mpunga alisema ushahidi unaonyesha mtuhumiwa aliuiba miti
huo huku akijua kufanya hivyo ni kosa kisheria na kwamba mti huo ulikuwa na
thamani ya Sh. 1,800,000.
Awali mshtakiwa aliiomba mahakama isimpe adhabu kutokana na
kuwa bado ni mtafutaji.
Kwa upande wake karani wa mahakama hiyo Kassim Mtanga alidai
mshtakiwa hana kumbukumbu ya makosa hivyo adhabu atakayopewa iwe fundisho kwake
na kwa jamii.
Katika kesi nyingine Hamis Mtembezi (36) amehukumiwa kwenda
jela mwaka mmoja baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kujeruhi kinyume cha
sheria.
Hakimu alisema mshtakiwa alimjeruhi Samweli Wambura kwa
kumkata na kisu eneo la mkononi Agosti 1 mwaka huu.
Awali wakati alipofikishwa kwa mara ya kwanza alikana
kutenda kosa hilo.
Aidha mshtakiwa Jerry Mushi (22) amehukumiwa kwenda jela
mwaka mmoja kwa kosa la kujeruhi na akimaliza atapaswa kulipa Sh. 250,000.
Mpunga alisema mshtakiwa akiwa eneo la Bilicanas, Ilala
Julai 31 mwaka huu alimjeruhi mlalamikaji Juma Hamis sehemu za tumbo kwa
kumkata na chupa na kumsababishia maumivu.
Hakimu alisema ushahidi wa PF3 ulithibitisha kuwa mshtakiwa
alimjeruhi mlalamikaji sehemu za tumbo.
Awali kabla ya kusomewa hukumu yake mshtakiwa alijitetea
kuwa ni baba wa familia na watoto wawili na wanamtegemea.
Wednesday, October 12, 2016
Miaka 30 jela kwa unyang’anyi
NA MWANDISHI WETU
MKAZI wa Kinondoni kwa Manyanya
Stephano Focus ‘ Malenga Tyson’ (29) amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela na
Mahakama ya Wilaya ya Ilala jijini hapa baada ya kukiri kosa la unyang’anyi wa
kutumia silaha.
Akisoma hukumu hiyo jana Hakimu
Mkazi Adelf Sachore alisema mshtakiwa alitenda kosa hilo kinyume na kifungu cha
Sheria Na. 287A (16) cha Kanuni ya Adhabu kilichofanyiwa marekebisho na Sheria
Na. 3 ya mwaka 2011 Septemba 4 mwaka huu eneo la Jangwani.
Hakimu aliendelea kusema mshtakiwa
kabla na baada ya kufanya unyang’anyi katika duka la simu alimtishia mmiliki
Tosha Sudi kwa panga ili kujipatia mali hizo.
Aidha Sanchore alizitaja mali
zilizoibwa na mshtakiwa kuwa ni simu aina ya Huawei G750 yenye thamani ya Sh.
500,000; Nokia yenye thamani ya Sh. 45,000; TECNO nne zenye jumla ya thamani ya
Sh. 230,000; Samsung X5 nne zenye jumla ya thamani ya Sh.3,500,000 zote kwa
pamoja zikiwa na jumla ya thamani ya Sh. 4,275,000.
Awali kabla ya kusomewa huku
mshtakiwa aliiomba mahakama imkumbushe shtaka lake ndipo Hakimu alipomsomea na
mshitakiwa kukiri kosa licha ya Septemba 26 mwaka wakati kesi hiyo ikitajwa kwa
mara ya kwanza kukana.
Kwa upande wake Mwendesha Mashtaka
SP Munde Kalombola aliiomba mahakama licha ya kukiri kwake kutenda kosa hilo na
kuirahisishia mahakama kazi yake haimaanishi apunguziwe adhabu bali kutokana na
uzito wa kosa lenyewe mshtakiwa anapaswa kupewa adhabu kali ili iwe fundisho
kwake na jamii kwa ujumla.
Monday, October 10, 2016
HUKUMU YA AJABU; Ahukumiwa kifungo cha maisha mara mbili na miaka 14
NA JABIR JOHNSON
MAHAKAMA ya Wilaya ya
Ilala jijini hapa imemhukumu mkazi wa Mbagala Kingugi Erick Mdem (39) kifungo
cha maisha mara mbili na miaka 14 kwa makosa matatu tofauti likiwamo kumlawiti
mwanaume mwenzake.
Katika kesi hiyo
washtakiwa Mdem na Juma Richard (31) walikutwa na hatia huku kila mmoja
akikabiliwa na adhabu yake.
Akisoma hukumu wiki
lililopita mahakamani hapo Hakimu Mkazi Said Mkasiwa aliwatia hatia washtakiwa
wote huku mshtakiwa namba moja akitupwa jela kifungo cha maisha mara mbili na
miaka 14 kwa kuwamo katika kila kosa.
Mkasiwa alisema
mshtakiwa namba mbili atatumikia jela miaka 14 pekee kwa kosa kukutwa na
makubaliano yaliyokuwa kwenye maandishi baina ya Mdem na mlalamikaji kulipana Sh.
1,000,000 ili wasisambaze tukio la kulawitiwa kwake kwenye mitandao hususani
‘whatsapp’.
Katika maelezo ya
awali, Hakimu alisema walipofika katika gesti ya Maembe walimkuta mlalamikaji
ambaye ushahidi ulithibitisha kuwa ulikuwa ni mtego ambao uliokuwa umeandaliwa
na washtakiwa wawili Erick Mdem na Juma Richard (31).
Washtakiwa hao
walimvua nguo zote na kumlawiti huku wakichukua picha za video za tukio hilo
kisha wakachukua vitu vyake vyote ikiwamo laptop na fedha taslimu Sh. 100,000.
Baada ya hapo
walimtaka awape Sh. 1,000,000 ili wasizisambaze video waliyomchukua wakati
wakimlawiti, wakati mlalamikaji akiwa katika harakati za kutafuta kiasi hicho cha fedha alijikuta
akiletewa video na ndugu yake ikionyesha tukio zima na vitendo vya
udhalilishaji alivyofanyiwa.
USHAHIDI ULIKUWAJE?
Hakimu alisema
ushahidi wa PF3 ulidhihirisha bila shaka
katika sehemu za haja kubwa kulipatikana mikwaruzo sehemu hizo
zilizotokana na kuingiliwa na uume.
Maandishi yaliyokuwa
na vitisho vya kusambaza kwenye mitandao endapo hatawapa kiasi hicho cha fedha
Pia ushahidi wa
mhudumu wa gesti hiyo nao ulidhihirisha mahakama pasipo shaka kuwa walimkuta
mteja wao ambaye ni mlalamikaji bila nguo hivyo waliamua kumsitiri kwa kumpa
suruali.
Ushahidi wa video ya
tukio hilo ulipelekwa katika kitengo cha picha cha Jeshi la Polisi Tanzania na
kubaini kuwa washtakiwa ndio waliofanya kazi ya uchukuaji wa picha dhidi ya
mlalamikaji.
Aidha Mkasiwa alisema
katika utetezi mshtakiwa namba moja ambaye ni Erick alikana kufanya matukio
hayo huku akidai kuwa siku ya tukio alikuwapo katika eneo hilo.
Kwa upande wa
Mwendesha Mashtaka Sylivia Mitanto alidai kuwa washtakiwa wote wawili hawana
kumbukumbu ya makosa waliyowahi kuyafanya siku za nyuma lakini makosa
waliyoyafanya yanastahili adhabu kali ili iwe fundisho kwa jamii.
SEPTEMBA 19, 2014
Kesi hiyo ilifika kwa
mara mahakamani hapo Septemba 19, 2014 ambapo washtakiwa wawili Erick na
mwenzake walikabiliwa na makosa matatu
ambapo kosa la kwanza lilikuwa ni wizi na kuleta vurugu kinyume na kifungu cha 285 na 286 vya kanuni
ya adhabu kuwa mnamo Agosti 23, 2014 wakiwa Maembe Bar na Gesti ya Kiwalani
Yombo waliiba Laptop aina ya HP yenye thamani ya Sh. 350,000, Simu aina ya
TECNO yenye thamani ya Sh. 150,000, jozi moja ya viatu yenye thamani ya Sh.
8,000, fedha taslimu Sh. 100,000 vyote vikiwa na jumla Sh. 608,000.
Kosa la pili lilikuwa
ni kulawiti kinyume na maumbile kinyume na kifungu Na. 154(1)(a) na (2) na kosa
la tatu lilikuwa ni kuhitaji fedha Sh. Milioni moja kutoka kwa mlalamikaji kwa
njia za vitisho kinyume na Kifungu cha Sheria Na. 289 cha kanuni ya adhabu ili
kutosambaza video za udhalilishaji waliomfanyia.
Askari wa Jeshi la Magereza Tanzania wakiwa katika karandinga la
jeshi hilo muda mfupi kabla ya kuondoka na washtakiwa wa makosa mbalimbali
kurudi magereza kuendelea na adhabu
|
Karandinga la Magereza likiwapeleka watuhumiwa wa makosa
mbalimbali kuendelea na adhabu walizopata.
|
Friday, October 7, 2016
‘Scorpion’ mtoboa macho kizimbani
NA JABIR JOHNSON
Salum Njewete 'Scorpion' akipelekwa katika karandinga la Jeshi la Magereza baada ya kesi yake kuahirishwa kutokana na upelelezi kutokamilika. |
MWALIMU wa sanaa za
mapigano Salum Njewete (34) maarufu Scorpion na mkazi wa Yombo Machimbo amepandishwa katika mahakama ya
Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam kujibu mashtaka yanayomkabili likiwamo la wizi wa kutumia
silaha.
Shauri hilo lilifika
mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa tena ambako upande wa mashtaka uliiambia mahakama upelelezi wa kesi hiyo
bado haujakamilika.
Awali ilidaiwa mahakamani
hapo na Mwendesha Mashtaka wa serikali Munde Kalombola mbele ya Hakimu Adolf
Sanchore kuwa Septemba 6 mwaka huu katika maeneo ya Buguruni Shell jijini Dar
es Salaam mshtakiwa alimvamia na kumchoma visu kwenye macho,tumboni na mabegani
Said Mrisho kinyume na Kifungu cha Sheria Na.287A sura ya 16 ya makosa ya
jinai.
Mwendesha mashtaka alidai
mshtakiwa alimpora mkufu wa fedha gramu 38 wenye thamani ya Sh. 60,000; kidani
cha mkononi chenye thamani ya Sh. 85,000 na fedha taslimu Sh. 331,000.
Kesi hiyo ilitajwa kwa
mara ya kwanza Septemba 23 mwaka huu.
Hakimu aliahirisha kesi
hiyo hadi Oktoba 19 mwaka huu.
Hali ilivyokuwa
mahakamani
Mapema juzi akiwa
amevalia T-shirt nyekundu na suruali aina ya ‘Jeans’ alishuka katika karadinga
la Magereza chini ya ulinzi mkali huku akificha sura yake kuogopa
kamera za waandishi wa habari.
Umati mkubwa wa watu
ulifurika katika viwanja vya mahakama ya Ilala kumshuhudia mshtakiwa ambaye
minong’ono ya hadhira ilikuwa ikimtaja kama ‘mtoboa macho’.
Majira ya saa nane za
mchana mshtakiwa alirudishwa rumande huku kukiwa na hadhira ndogo ya watu.
Wakati akitolewa mahabusu
kurudishwa rumande Scorpion alitaka kuiahadaa hadhira kwa kubadilisha nguo zake
kuogopa kamera za waandishi wa habari (kama inavyoonekana pichani).