Sunday, June 30, 2024

Mikopo ya Halmashauri kuanza kutolewa tena Julai 1, 2024

Diwani wa Kata ya Korongoni, Moshi, Bi. Heavenlight Kiyondo akiwa na mjukuu wake nyumbani kwake. Diwani huyo amekuwa mstari wa mbele kuwahamasisha wanawake na vijana kwenda kukopa katika Halmashauri mikopo isiyo na masharti magumu ili kujiepusha na mikopo itakayowapeleka kwenye mateso wakati wa kuirudisha. Julai 1, 2024 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilisema itaanza tena kutoa mikopo hiyo katika halmashauri zote nchini. (Picha na JAIZMELA).


Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa, sura ya 290 ilifanyiwa marekebisho mwaka 2018 ili kuweka masharti kwa Halmashauri zote nchini kutenga fedha kwa ajili ya mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Kufuatia marekebisho hayo Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ilitunga kanuni zinazoanisha masharti ya utozaji na usimamizi wa mikopo inayotolewa na Halmashauri kwa vikundi hivyo.

Kanuni ya 4 ya Utengaji wa Fedha za Mikopo inamweka bayana Halmashauri inatakuwa na wajibu wa kutenga asilimia 10 ya Mapato yanayotoka katika vyanzo vyake vya ndani kwa ajili ya kutoa mikopo kwa vikundi  vya wanawake asilimia 4, vijana asilimia 4, na watu wenye ulemavu asilimia 2.

Mnamo Aprili 13,2023 katika Bunge la 12 Waziri Mkuu wa Jamhuri Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa alitangaza usitishwaji wa mikopo hiyo ili kupisha utaratibu mwingine wa utoaji wa mikopo.

Baada ya mwaka mmoja, mnamo Aprili 16, 2024 Waziri wa TAMISEMI Mohammed Mchengerwa alitangaza kurejesha kwa mikopo hiyo wakati akisoma bajeti yake ya mwaka 2024/25.

Jumatatu ya Mei 13, 2024 Naibu Waziri TAMISEMI Zainab Katimba wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum Josephine Gezabuke aliwaondoa hofu wanawake, vijana na watu wenye ulemavu na kwamba mikopo hiyo rasmi itaanza kutolewa Julai Mosi 2024.

Katimba alisema Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia kutolewa tena mikopo hiyo, bayana sababu iliyofanya isitishwe kuwa marejesho kwa vikundi vilivyokuwa vikidaiwa yalikuwa yanaendelea.

Shilingi bilioni 227.96 zinatarajiwa kutolewa kwa vikundi hivyo nchi nzima huku shilingi bilioni 63.67 zikiwa ni fedha za marejesho kwa mikopo ilitotolewa kabla ya kusimamishwa.

0 Comments:

Post a Comment