Sunday, June 30, 2024

Dkt. Nchimbi anavyowatazama Tundu Lissu, Mbowe


Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi  (CCM) Taifa; Dkt. Emmanuel Nchimbi katika mkutano wa Hadhara katika mji wa BomaNg'ombe wilayani Hai Juni 4,  2024 (Picha na Jabir Johnson/JAIZMELA)


Katika miongoni ya mikutano ya hadhara iliyowastaajabisha wengi na hawakutegemea kama ingalikuwa hivyo ni ule wa Juni 4, 2024 uliofanyika katika mji wa Bomang;’ombe, wilayani Hai mkoani Kilimanjaro.

Mkutano huo ulihutubiwa na Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara yake mkoani Kilimanjaro alikopita kuzungumza na watanzania kuhusu mambo mbalimbali yanayofanywa na chama hicho.

Kiini cha makala haya ni pale hasa alipogusia suala la demokrasia ndani na nje ya Tanzania. Dkt.Nchimbi alivuta usikivu wa watanzania waliomiminika hapo wake kwa waume kumsikiliza na wengine walipata fursa ya kuwasilisha kero zao.

Alianza hivi, ““Hivi ninyi mkiamka na kukuta mtu anafagia uwanja wa nyumba yao unakasirika? Ukiwa na nguo chafu halafu ukamkuta mtu amezifua na kuzianika unakasirika,”

Dkt. Nchimbi anavuta funda la mate na kuendelea, “Tundu Lissu na Mbowe wanakisaidia CCM kufagia uwanja, wanatufulia nguo, tunawashukuru sana kwa kututendea wema huo wa kufanya kazi za CCM ya kuitangaza demokrasia ya nchi yetu  hakuna sababu ya kugombana nao mnapokutana nao.”

Hapo ndipo mwanasiasa huyo mkongwe aliyelelewa vema ndani ya chama hicho na kufikia kuwa Katibu Mkuu wa CCM aliponifanya nirudie hotuba na maneno ya mwasisi wa chama hicho ambaye ni Baba wa Taifa la Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika kitabu chake cha Binadamu na Maendeleo alichokiandika mnamo mwaka 1974.

Mwalimu Nyerere aliandika, “`Kuna mambo mawili ya lazima katika demokrasia, ukiyakosa hayo demokrasia hakuna. La kwanza: Ni kwamba kila mtu lazima aweze kusema kwa uhuru kabisa na maneno ya kila mtu lazima yasikilizwe.

Nyerere aliongeza, “Hata kama maneno ya mtu huyo hayapendwi kiasi gani, au walio wengi wanamdhania amepotoka kiasi gani si kitu, kama mtu anapendwa kwa wema wake au hapendwi kwa visa vyake hayo yote si kitu.”

Pia Mwalimu Nyerere alisisitiza, “Majadiliano lazima yaruhusiwe kuendelea kwa uhuru kabisa, hiyo ni sehemu ya maana ya uhuru wa mtu binafsi.”

Dkt. Nchimbi aliwavutia wengi sana katika hotuba yake hiyo kwa watanzania miongoni mwa maneno yake yatakayokumbukwa kuhusu demokrasia katika taifa la Tanzania.

Katibu Mkuu huyo alisisitiza sana, ndani na nje ya chama kutogombana na wapinzani kwani kwa namna moja au nyingine ni kumwangusha Rais Samia Suluhu Hassan katika majukumu yake ya kuijenga Tanzania mpya inayojali demokrasia na uhuru wa kila mmoja pasipo kuvunja sheria.

“Rais Samia amedhamiria kusimamia misingi ya Chama chetu ya kuimarisha  demokrasia ndani ya chama na nje ya chama chetu. Wana-CCM wawe na haki ya kuchagua na kuchaguliwa  na haki hiyo inapatikana bila masharti yoyote,” aliongeza Dkt. Nchimbi.

Dkt. Nchimbi aliweka bayana kuwa wapinzani wakuu wa CCM ambao ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wangekuwa na wanahitaji kulipwa angewalipa kiasi cha kutosha cha fedha kwa kuendelea kuitangaza demokrasia ndani na nje ya nchi.

“Wapinzani wanatusaidia sana kufanya kazi, ya kuiambia dunia kwamba Tanzania kuna demokrasia ya kutosha wakati mwingine wanafanya kazi yetu, Mimi nikiwaona Freeman Mbowe na Tundu Lisu wakitoka jasho kwenye maandamano moyoni mwangu nasema mnatusaidia kazi Baba!!na wangekuwa wanahitaji malipo ya kufanya hiyo kazi Walahi ningewalipa, ingekuwa wanahitaji malipo ningewwalipa.

Madhumuni ya ziara ya Dkt. Nchimbi mkoani Kilimanjaro ni; Kuangalia Utekelezaji wa Ialni ya CCM, Ilani ni mkataba kati ya Wananchi na Chama, tulipofanya uchaguzi mwa 2020 yako malengo ya miaka mitano ya CCM iliyoyaweka.

Imeandikwa na Jabir Johnson

+255 693 710 200

0 Comments:

Post a Comment